Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango amesema zinahitajika juhudi za pamoja za ndani ya nchi , za kikanda na kimataifa katika kuweka mikakati na kutafuta njia madhubuti za kulinda na kuhifadhi bahari na rasilimali zake kwa kusimamia matumizi endelevu ya bahari.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Bahari Duniani yaliofanyika Jijini Dar es salaam leo tarehe 08 Juni 2023. Amesema inapaswa kuwepo kwa uwiano sawia kati ya hali ya bahari na kuimarika kwa uchumi kwani Afya ya Bahari na mifumo imara ya kiikolojia ya baharini ni muhimu kwa uchumi wa buluu ambao ni sehemu ya ajenda ya nchi kufikia maendeleo endelevu.
Makamu wa Rais amesema umuhimu wa kulinda bahari na rasilimali zake unatokana na faida lukuki zinazopatikana zikiwemo Bahari kuchukua zaidi ya asilimia 70 ya eneo la dunia, zaidi ya asilimia 50 ya hewa safi ya oksijeni , zaidi ya 90% ya joto la ziada linalosababishwa na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuchukua zaidi ya asilimia 30 ya hewa ya Kaboni inayozalishwa na shughuli za kibinadamu.
Dkt. Mpango ameongeza kwamba tafiti zinaonesha kufikia 2030 Bahari itakuwa ndio nguzo kuu ya uchumi duniani ambapo takriban watu milioni 40 watakuwa wameajiriwa moja kwa moja na viwanda vinavyotumia rasilimali za bahari.
Hali kadhalika amesema zaidi ya asilimia 90 ya usafirishaji wa bidhaa kimataifa hutegemea bahari pamoja na bahari ni makazi ya viumbe hai mbalimbali ambavyo ni chanzo kikuu cha protini kwa zaidi ya watu bilioni tatu duniani.
Makamu wa Rais ameongeza kwamba Tanzania ni mojawapo ya nchi chache duniani zilizojaliwa kuwa na sehemu ya bahari inayokadiriwa kuwa na ukubwa kilometa za mraba zipatazo 64,000, ufukwe wenye urefu wa kilometa 1,424 pamoja na ukanda huru wa kiuchumi (Exclusive Economic Zone) upatao kilometa za mraba 223,000 ambao unaongeza wigo wa shughuli za uchumi wa bahari.
Amesema faida hiyo ya kijiografia ni adimu na adhimu kwani inaipa Tanzania nafasi kubwa ya kufaidi matunda yatokanayo na bahari pamoja na rasilimali zake.
Makamu wa Rais ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana Wizara ya Uvuvi na Taasisi za Utafiti wa Bahari kama Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (TAFIRI), Taasisi ya Sayansi za Bahari iliyoko Zanzibar (IMS) kuhakikisha utafiti wa kina unafanyika kwa wingi zaidi ili kuongeza uelewa wa sayansi ya bahari pamoja na athari za changamoto zilizojitokeza kwa jamii na ikolojia.
Vilevile Makamu wa Rais amesema upo umuhimu mkubwa wa kuhusisha na kushirikishwa kikamilifu kwa jamii za asili ya pwani katika ulinzi wa rasilimali za bahari kwa kuwa wao ndio wafaidika au waathirika wa kwanza wa mazingira ya bahari.
Pia ameagiza Mamlaka zinazohusika na uvuvi na uhifadhi ziongeze jitihada katika kutoa elimu zaidi kwa wavuvi ili washiriki kikamilifu katika uhifadhi wa rasilimali endelevu za bahari na kuondokana na njia zisizofaa za uvuvi.
Aidha Dkt. Mpango ametoa wito kwa vyombo vya habari na wasanii nchini kutambua wajibu walionao katika kusaidia jamii kupata uelewa wa kutosha kuhusu bahari na rasilimali zake kupitia nyenzo mbalimbali kama vile vipindi maalum, makala, mahojiano ya ana kwa ana na kurushwa kwenye redio, televisheni, magazeti na mitandao ya kijamii.
Kwa upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega amesema Wizara hiyo inatoa umuhimu mkubwa katika shughuli za uhifadhi wa rasilimali za bahari na kudhamiria kuilinda bahari na viumbe wake.
Ameongeza kwamba ili kuwa na uvuvi endelevu ni lazima kuwa na maeneo ya uhifadhi baharini ambayo yanalenga katika kulinda, kuhifadhi na kudumisha uvuvi endelevu na kukuza mchango wa sekta ya uvuvi na pato la taifa.
Awali akitoa maelezo kuhusu Siku ya Bahari Duniani, Mwenyekiti wa Bodi wa Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu Nchini Mhandisi Dkt. Boniventura Baya amesema siku hiyo ya kimataifa inaunga mkono suala la utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu na kukuza maslahi ya umma katika ulinzi wa bahari na usimamizi endelevu wa rasilimali zake.
Amesema vita dhidi ya uchafuzi na uharibifu wa bahari inaendelea dunia nzima ikiwemo Tanzania kwa kutambua umuhimu mkubwa wa bahari kwa Maisha ya mwanadamu.
Wazo la kuanzishwa kwa Siku ya Bahari Duniani hlilipendekezwa mwaka 1992 na kutambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa (UN) mwaka 2008.
Kauli Mbiu ya Siku ya Bahari Duniani kwa mwaka 2023 ni “Sayari ya Bahari: Mawimbi Yanabadilika” (Planet Ocean: Tides Are Changing)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akisikiliza maelezo kutoka kwa Jenipher Simbua ambaye ni mtumishi kutoka Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu Tanzania kuhusiana na viumbe mbalimbali wanaopatikana Baharini ikiwemo Samaki adimu aina ya Silicanti wakati wa maonesho ya Siku ya Bahari Duniani yaliofanyika Jijini Dar es salaam. Tarehe 08 Juni 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akihutubia Viongozi, Watumishi, Wadau wa Bahari pamoja na Wananchi mbalimbali wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Bahari Duniani yaliofanyika Jijini Dar es salaam. Tarehe 08 Juni 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa dini pamoja na wawakilishi wa jamii ya watu wanaoishi jirani na bahari wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Bahari Duniani yaliofanyika Jijini Dar es salaam. Tarehe 08 Juni 2023.
0 Comments