Ticker

6/recent/ticker-posts

DKT. RUTAYUGA AHIMIZA VYUO KUTOA KOZI ZENYE MANUFAA YA HARAKA KWA JAMII

Katibu Mtendaji wa NACTVET Dkt. Adolf Rutayuga amevitaka vyuo mbalimbali hapa nchini kuacha kutoa kozi za mazoea ambazo zinajirudia katika vyuo vingi na badala yake watoe kozi zinazoweza kuleta manufaa ya haraka kwa jamiii ili kujenga uchumi endelevu.

Dkt. Rutayuga ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya awamu ya tatu kwa wamiliki na wakuu wa vyuo binafsi vya Mafunzo ya Ufundi Stadi toka Kanda ya Magharibi na Kanda ya Ziwa leo tarehe 15 Juni, 2023 mjini Morogoro.

Lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wamiliki na wakuu wa vyuo kuweza kutoa mafunzo yenye ubora na yanayokidhi mahitaji ya jamii na soko la ajira nchini.

“Tanzania tumekua tukitoa kozi zilezile za zamani kama vile Mpiga chapa (Typist), Ushonaji, Umeme wa Majumbani na nyinginezo,lakini naomba sasa tuziangalie jamii zinazotunguzuka na kuona ni jinsi gani tunaweza kutoa kozi ambazo zinaweza kuzisaidia jamii zetu kuboresha kile wanachokifanya kuwa na tija na kuongeza kipato”. Alisema Dkt. Rutayuga.

“Tujiulize kwa pamoja je kuna chuo chochote kinachofundisha wafugaji jinsi ya kuweza kuhifadhi majani kipindi cha Masika ambayo yangeweza kuwasaidia wakati wa ukame au mafunzo ya kuwawezesha wakulima kupunguza matumizi ya madawa kwenye bidhaa za Mbogamboga na Matunda ili kulinda afya za walaji”. Aliongezea Dkt. Rutayuga.

Pamoja na hayo, Dkt. Rutayuga amewataka wadau wote wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi kushirikiana ili kujenga nguvukazi yenye ujuzi na umahiri na kuwaaasa wamiliki na wakuu wa vyuo kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali iliyowekwa na NACTVET ikiwa ni pamoja na kufanyia kazi mapungufu mbalimbali yaliyoainishwa katika vyuo vyao kwa maendeleo ya Ufundi Stadi nchini.

Vilevile ameahidi kuendelea kukutana na vyuo hivyo ili kujengeana uwezo, ujuzi na uelewa wa pamoja juu ya masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwekeana mikakati ya namna ya kuratibu Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi nchini.

Prof. Idrissa P. Mshoro ametoa mafunzo kwa wamiliki na wakuu wa vyuo hao juu ya uongozi katika kufanikisha ubora na ufanisi wa utoaji mafunzo katika vyuo. Miongoni mwa watumishi wa NACTVET walioshiriki ni pamoja na Dkt. Alex Nkondola, Mkurugenzi (Huduma za Taasisi), Dkt. Amani Makota, Mkurugenzi (Huduma za Uendeshaji Vyuo), Bi. Faraja Makafu (Meneja Kanda ya Magharibi) na Bi. Shani Mwambwene (Meneja Msaidizi - Kanda ya Ziwa).

Post a Comment

0 Comments