Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amekutana na watumishi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Kati jijini Dodoma leo Juni 14, 2023.
Akizungumza na watumishi hao amewahimiza waendelee kufanya kazi kwa kujituma ili kuisaidia Serikali katika jitihada zake za kuhakikisha Sheria ya Mazingira inatekelezwa ipasavyo.
Waziri Dkt. Jafo ametoa wito kwa watumishi hao wawe na moyo wa kuipenda kazi yao na kuleta tija kwa taasisi, Serikali na jamii kwa ujumla ili kuleta matokeo mazuri.
Amesema kuwa raha ya kufanya kazi wafanyakazi wenzako waipende na kuithamini na iwe na ubunifu wa mara kwa mara na si kufanya kazi kwa mazoea.
“Ndugu zangu niwaambie unapokuwa kazini kitu cha muhimu uache legacy na hata wakati ukiwa likizo wenzako washtuke sio wakuulize sio unanda likizo na hakuna anayekuulizia,“ amesisitiza Dkt. Jafo.
Waziri Jafo amesema mahali pa kazi pia ni sehemu ya kuendelea kujifunza maarifa na mbinu mbalimbali za utendaji hivyo watumie kufanya kazi kwa weledi na kuhakikisha thamani ya kazi inaonekana.
Aidha, ametumia nafasi hiyo kuwatia moyo katika kutekeleza majukumu yao ikiwemo operesheni ya kutokomeza mifuko na vifungashio vya plastiki vilivyopigwa marufuku na Serikali ambayo inaendelea kufanyika nchi nzima.
Pia, amewapongeza kwa udhibiti wa uchafuzi wa mazingira kelele na mitetemo inayozidi kiwango katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya starehe nchini ambayo yamekuwa ni changamoto kwa wananchi kutokana na kuwasababisha kero na madhara kiafya.
Amewasihi watumishi wa Kanda ya Kati pamoja na Kanda zingine za NEMC kuendelea kutekeleza Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 kudhibiti uchafuzi wa mazingira unaofanywa kwa njia mbalimbali pamoja na kuwepo kwa vikwazo kutoka kwa baadhi ya watu wasivunjike moyo.
“Ni kweli kazi ya enforcement ni ya lawama sio ya kupigiwa makofi hata kidogo na ni kweli watu wengi ni wagumu kufuata sheria wakikmatwa wanakasirika, hata hivyo nawapongeza mnaendelea kutoa elimu mnapita masokoni huko,“ amesisitiza Dkt. Jafo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akizungumza na watumishi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Kati alipokutana nao katika ofisi hizo zilizopo jijini Dodoma leo Juni 14, 2023.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akiwa katika picha ya pamoja na Meneja wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Kati Dkt. Caren Kahangwa mara baada ya kikao na watumishi wa Baraza hilo Kanda ya Kati leo Juni 14, 2023 jijini Dodoma.
PICHA NA OFISI YA MAKAMU WA RAIS)
0 Comments