Na Said Mwishehe,Michuzi TV
KAMISHNA wa Idara ya Kitaifa ya Mipango kutoka Wizara ya Fedha na Mipango Dk.Mursal Milanzi pamoja na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi Kadari Singo wameeleza kwa kina mchakato unaendelea katika kuhakikisha mpango wa Dira ya Maendeleo mwaka 2050 inatekelezwa na kuleta matokeo chanya kwa Watanzania.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa kikao kilichowatanisha wadau mbalimbali wakiwemo walioandaa mpango wa Maendeleo mwaka 2025 na wanaotarajia kuandaa mpango wa mwaka 2050, Kamishna wa Kitaifa Idara ya Mipango kutoka Wizara ya Fedha Dk .Milanzi amesema baada ya kuzinduliwa rasmi kwa dira ya mpango huo wa maendeleo na Makamu wa Rais Aprili 3 mwaka huu sasa imewapa nafasi ya kuendelea na michakato mingine inayofuata
Dk.Milanzi ambaye pia ndio Mwenyekiti wa Sekretarieti ambayo inafanya maandalizi ya dira ya maendeleo 2050 ameeleza kwamba mchakato uliopo sasa ni kushirikisha wadau mbalimbali lakini kabla ya kushirikisha wadau ni vizuri wakajifunza pia kwa yale ambayo yametokea kwenye dira inayotokelezwa kwa Sasa ya 2025.
"Kwa hiyo tumekutana hapa kubadilisha uzoefu na wenzetu wale walioshiriki kwenye dira ya 2025, kama mnavyojua dira ya 2025 ilianza kutekelezwa mwaka 2000 lakini ilikuwa imezinduliwa rasmi mwaka 1999 na baada ya hapo kuna mambo mengi yamefanyika hapo katikati ambayo ndio yalikuwa matamanio katika dira ya 2025
"Kwa hiyo ukiangalia kwenye sekta, kwa mfano tunapozungumzia sekta ya afya tunaona maendeleo ambayo yamepatikana hasa upatikanaji wa huduma za afya kuwa karibuni na wananchi,hilo ni tokeo mojawapo kwamba limesababishwa na utekelezaji wa dira ya 2025.Lakini kwenye upande wa elimu upatikanaji wa huduma za elimu kwa kiasi kikubwa umeongezeka.
"Kama mnavyofahamu tulikuwa na vyuo vichache lakini sasa tunavyuo vikuu vingi,shule za sekondari zilikuwa chache lakini sasa tuna shule za sekondari karibia kila Kata na ukiangalia upande wa miundombinu tunaangalia tulikotokea sasa hivi tunabarabara nyingi za lami ambazo zinaunganisha Mkoa kwa Mkoa na nyingine Wilaya kwa Wilaya.
"Hayo ni baadhi ya mafanikio ambayo tumeyapata kutokana na utekelezaji wa dira ya 2025, tunafahamu sio kila kitu kilichopangwa kutekelezwa kimetekelezwa na hii ni kutokana na changamoto nyingine za ndani ya nchi na nyingine zinazotokana na matukio yanayotoka nje kwa mfano tukiangalia matukio makubwa kwa mfano COVID ni jambo la karibuni.
"Lakini ni vitu vichache ambavyo vinasababisha kuchelewa kwa utekelezaji wa dira na matukio kama hayo yamekuwa yalitokea miaka ya nyuma ila COVID imetokea juzi lakini matukio yanayofanana na hayo yametokea huko nyuma na kuchelewesha utekelezaji wa dira.Pia kuna masuala mazima ya utekelezaji wa viwango vya bajeti ya maendeleo,tunafahamu Serikali imekuwa ikiongeza bajeti ya maendeleo kila mwaka,"amesema
Amefafanua lakini ukiangalia katika sekta kwa mfano zilikuwa ziko kidogo lakini imekuwa ikiongezwa kutokana na mapato yanavyopatikana na kwamba hakuna kiasi kikubwa cha bajeti lakini wamekuwa wakiongeza kila mwaka kuhakikisha mipango ya maendeleo inatekelezwa kama ambavyo imepanga
Dk.Milanzi amesema wanaamini sehemu kubwa ya utekelezaji wa dira ya 2025 itakuwa imepatikana kufikia 2025 ,sasa kwa yale ambayo wanayaona kama ni changamoto kwa sasa ndio wanakwenda kuyaingiza kwenye dira mpya." Kwa hiyo kama kuna mahala tuliona hatukufanya vizuri sasa ni fursa ya kujifunza kwanini hatukufanya vizuri.
"Na pale ambapo tulifanya vizuri sasa ni wakati wa kujifunza kwanini tulifanya vizuri na tunapokwenda kwenye dira ya 2050 tunaona tunajifunza kwenye yale mazuri tunaendelea nayo lakini yale ambayo hatukufanya vizuri tunajifunza tumekosea wapi ili tuweze kuingiza kwenye dira hii ambayo tunaitengeneza sasa.
"Naamini maendeleo ambayo yametokea kwa sasa yatatupa nafasi ya kukimbia kimaendeleo ukilinganisha na hii dira ya 2025 ambayo tunaendelea kuitekeleza kwa mfano ukiangalia Sayansi na Teknolojia ni jambo ambalo limekimbia sana kimaendeleo hapa katikati, kwa hiyo utekelezaji wa dira ya 2025 wote ni mashuhuda Sayansi na teknolojia kwenye mifumo ya ICT ilikuwa chini duniani na hasa nchi zetu za Afrika.
"Lakini kwa sasa kuna maendeleo makubwa, ukimuuliza mtu mwaka 1999 Smart Phone ilikuwa wapi hapa Tanzania unaweza kuitafuta na pengine haikuwepo .Hivi sasa tuna kompyuta,smart phone ambazo zote hizi zinatusaidia kupata taarifa na kumbukumbu za kujifunza namna gani wenzetu walivyoendelea na sisi tunafanye nini katika hiyo nyanja ya maendeleo,"amesema.
Hivyo Dk.Milanzi utekelezaji wa Dira ya 2050 upo uwezo wa kukimbia zaidi kuliko walivyokuwa kwenye utekelezaji wa mpango wa mwaka 2025 ,hayo ni maono yake , kikubwa ambacho wanataka kukiangalia au kikuendeleza ni uwekezaji katika rasilimali watu ambacho ni muhimu kwasababu huko ndiko wanakopatikana watu wenye ujuzi na uelewa wa kutosha kusaidia kusimamia masuala ya maendeleo
Pia wanafikiria wakifanya mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kuufanya kuwa wa kisasa na hapo wamaana kwamba sekta zote za kiuchumi lazima zibadilike zikimbie kwa kasi zaidi lakini ziwe za sasa."Kwa mfano hatuwezi kuzungumza kilimo kwenye miaka 25 ijayo tukataka kiwe sawa na kile kilimo ambacho kimefanyika miaka 25 iliyopita.
"Kwa hiyo ili tufanye kuongeza tija ya kilimo kuwa cha kisasa,kutumia mbegu za kisasa,umwagiliaji ndiko tunakoelekea kwamba tunaweza kupata maendeleo makubwa iwapo tutaelekea upande huu lakini pia hata sekta ya viwanda tuna umuhimu mkubwa wa kufunganisha na kilimo.Tukiweza kufanya kilimo kuwa cha kisasa,kufanya viwanda kuwa vya kisasa na elimu kuwa ya kisasa tutakwenda kwa kasi zaidi kuliko tulivyokuwa tunafanya huko nyuma
"Hivyo vipaumbele vyetu ni sekta za uzalishaji lakini tuzifanye kuwa za kisasa lakini hizi sekta za kijamii kama elimu na afya maana huo ndio mtaji wa binadamu,"amesema na kusisitiza Watanzania wako tayari katika kushiriki kwenye mipango ya maendeleo
"Watanzania wamekuwa wakipiga kilele kuhusu maendeleo kikubwa ni namna gani tunawaongoza kuelekea kwenye maendeleo,kwa hiyo tukiwa na dira ambayo iko wazi na kila Mtanzania akawa anaielewa dira vizuri naamini kabisa watasaidia kwenye kukimbiza huu mchakato wa maendeleo na maendeleo ni kwa ajili ya watu kwa hiyo lazima washiriki ipasavyo kwenye kujiletea maendeleo."
Kuhusu mkakati iliyoko kutekeleza mpango wa 2025 amesema Iko mingi lakini miongini mww mikakati hiyo upo wa kutoa taarifa kwa wananchi na hivi karibuni wataanza kupata meseji kutoka kwenye simu zao na tayari wameshawasiliana na TCRA lakini n Kampuni za simu."Tutaanza kupata meseji za kuwashiwishi wananchi mshiriki kwenye huo mchakato kwa hiyo tunaomba msikasirike kwa kupata hizo meseji.
"Kwani lengo letu ni kuhakikisha kila mdau anashiriki kwasababu njia ambayo tungeweza kuitumia ni ile ya kutembelea baadhi ya mikoa tu na kuzungumza na watu na nchi yetu ni kubwa sana ina watu milioni 61 kwa vyovyote vile hatuwezi kufikia kila mtu,kwa njia nyingine ni hiyo ya kupata meseji kwa njia ya simu,lakini kuna tovuti ambayo ukiinga unatuma ujumbe wako, tunayo mikakati midogo midogo mbalimbali kuhakikisha kila mtu anashiriki.
Kwa upande wake Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi Kadari Singo amesema wamewakutanisha wadau mbalimbali na kama inavyofahamika Serikali iko katika mpango wa kuandaa dira ya maendeleo 2050 lakini katika miaka 25 iliyopita imekuwa na mpango wa Maendeleo wa mwaka 2025.
" Sasa katika kuandaa mpango mwingine wa maendeleo wa miaka 25 utakaoanza kutumika kuanzia mwaka 2026 mpaka mwaka 2050 , kwa hiyo taasisi ya Uongozi imeona umuhimu wa kukutanisha wadau walioanda dira ya mpango wa maendeleo 2025 na watakaoandaa mpango wa 2050 , hii ni kuhakikisha tunajaribu kufanya uchambuzi wa mafanikio katika utekelezaji lakini changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji.
"Lakini changamoto katika uandaaaji, hii ni mipango mikubwa na maamuzi ya kitaifa kwa hiyo haiwezi kuchukuliwa kirahisi rahisi ndio maana tumeleta wadau mbalimbali. Taifa lolote duniani linakuwa na mipango ya muda mfupi,wa kati na muda mrefu ,huu ni mpango wa muda mrefu ambao maamuzi yake yataathiri vizazi vijavyo ,wengi wetu inawezekana wakati wa mpango wa 2050 unamalizika hatutakuwepo lakini watoto ni wanufaika wakubwa.
"Lazima tufikirie mazingira ambayo yatawakumbuka watoto miaka 25 mengine ijayo ,kwa hiyo kitu inahitaji utaalamu wa hali ya juu,kinahitaji kuhusisha wadau mbalimbali,kuhusisha wananchi na ikiwezekana kuhusisha hata vyombo vya kimataifa katika ushauri mbalimbali.
"Kwa hiyo taasisi ya Uongozi iliona ni vema wadau wakutane wabadilishane tu mawazo lakini wazungumze kwa huru kipi ambacho wanaona kinafanya kazi na kipi hakifanyi kazi katika utekelezaji au uandaaji wa mipango hii ya maendeleo."
Meza kuu ikiongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Bw. Kadari Singo, (walioketi katikati) kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt.Natu El-maamry Mwamba, ikiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Timu ya Wataalamu iliyoandaa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, katika warsha iliyofanyika katika ukumbi wa Julius Nyerere Convenction Centre, jijini Dar es Salaam.
0 Comments