Ticker

6/recent/ticker-posts

UFUNGUZI WA MKUTANO MKUU WA MWAKA WA TLS

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa Chama Cha Mawakili Tanganyika (TLS) na Kamati ya Mawakili kuchukua hatua kali za kinidhamu na kisheria dhidi ya mawakili wachache wanaoharibu heshima ya taaluma ya sheria kwa kukosa uadilifu na maadili mema.

Makamu wa Rais amesema hayo leo tarehe 11 Mei 2023 wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC).

Amesema kumekuwa na tuhuma kwa baadhi ya Mawakili kujihusisha na vitendo vya rushwa na udanganyifu kwa maslahi yao binafsi ikiwemo kuwasaliti wateja kwa kupokea rushwa kutoka upande wa pili na kuharibu kesi.

Makamu wa Rais ametoa rai kwa TLS kuhakikisha inashirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria kutoa elimu kwa umma kuhusu suala la mihuri ya kielektroniki ili kuondokana na suala la vishoka na mawakili wanaotumia mihuri isiyo halali kufanya kazi za uwakili.

Pia ameziagiza taasisi zote za serikali pamoja na taasisi binafsi kuhakikisha zinatumia mihuri ya kielektroniki ili kuondokana na kadhia hiyo.

Halikadhalika Makamu wa Rais amesema ni wajibu wa sekta na taasisi za sheria kuendelea kuchambua, kubaini na kutoa mapendekezo ya sheria zinazotakiwa kufanyiwa marekebisho au kuandikwa upya hapa nchini.

Amesema ni vema kuweka nguvu zaidi katika kutoa elimu ya sheria kupitia mihadhara, redio, televisheni na mitandao ya kijamii ili kuondoa adha ya watu wengi wanaopoteza haki zao kwa kukosa uelewa wa sheria.

Ametoa rai kwa mawakili wasomi wote nchini, pamoja na taasisi husika, kuendelea na moyo wa kurejesha kwa jamii kwa kujitolea kuwasaidia wananchi wasio na uwezo wa kulipia gharama za kesi mahakamani.

Makamu wa Rais amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ina dhamira ya dhati ya kuhakikisha wananchi wake wanatendewa haki kwa mujibu wa sheria na kuishi kwa amani na utulivu katika nchi yao.

Ameipongeza TLS kwa kuunga mkono kampeni ya Mama Samia ya msaada wa kisheria “Mama Samia Legal Aid Campaign” pamoja na kuanzisha Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi wa Migogoro ya aina mbalimbali nje ya Mahakama, kitaifa na kimataifa (Tanzania International Arbitration Centre – TIAC).

 Amesema hatua hiyo ni muhimu katika kupunguza gharama, mrundikano wa mashauri, muda wa kutatua migogoro na kuvutia uwekezaji nchini.

Kwa upande wake Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro ametoa wito kwa wanachama wa TLS kushiriki kikamilifu katika mchakato wa katiba mpya pamoja na mchakato wa mabadiliko ya sheria zinazohusiana na siasa, uchaguzi na demokrasia kwani wapo wanachama wenye uzoefu mkubwa katika maeneo hayo.

Amesema wanachama hao ni wadau muhimu katika kuhakikisha inapatikana katiba mpya itakayoweza kusaidia taifa miaka mingi ijayo hivyo amewakaribisha katika kutoa ushauri pamoja na ushirikiano kwa kuwa serikali ipo tayari katika kutumia uzoefu na ujuzi wa wanachama wa chama hicho.

Awali akitoa taarifa ya utendaji wa Chama Cha Mawakili Tanganyika, Rais anaemaliza muda wake wa chama hicho Profesa Edward Hoseah amesema uongozi wa TLS umeweka muhimu na kipaumbele katika kuwa na ushirikiano wenye kujenga na serikali pamoja na wadau ambao umekuwa na manufaa makubwa kwa pande zote mbili.

Aidha ameongeza kwamba ushirikiano huo umefanya chama hicho kushiriki katika mbaoresho mbalimbali ya sheria hapa nchini, kushiriki katika tume mbalimbali za zinazoundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo kikosi kazi cha kutathimini hali ya siasa na demokrasi nchini pamoja na tume ya maboresho ya mfumo wa taasisi za haki jinai.

Pia Prof. Hoseah ameishukuru serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwezesha Chama hicho kupata ada za leseni na mahafali ambazo zilikua hazifiki katika chama hicho kinyume na sheria.

Amesema ushirikiano wa kujenga kati ya TLS na serikali umewezesha kupatikana kwa kiwanja katika eneo la mtumba mkoani Dodoma pamoja na kupungua kwa wimbi la kukamatwa kwa mawakili hapa nchini.

Dhima ya Mkutano huo wa Mwaka wa TLS ni “Upatikanaji wa Haki Tanzania: Wajibu wa Sekta/Taasisi za Sheria katika Utoaji na Upatikanaji wa Haki kwa Wananchi.”(Accessing Justice in Tanzania: The Role of the Legal Sector Institutions in Delivery and Access to Justice).

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC) leo tarehe 11 Mei 2023.
.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akiagana na Rais anayemaliza muda wake wa Chama Cha Mawakili Tanganyika (TLS) Profesa Edward Hoseah mara baada ya kuhitimisha hafla ya Ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC) leo tarehe 11 Mei 2023.




Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akiwa na Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro, Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongela, Rais wa TLS anaemaliza muda wake Profesa Edward Hoseah katika picha ya pamoja na wageni waalikwa na wadhamini wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) mara baada ya ufunguzi wa Mkutano huo unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC) leo tarehe 11 Mei 2023.

Post a Comment

0 Comments