Kassim Nyaki, NCAA
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa NCAA Jenerali Venance Mabeyo (mstaafu) ametoa rai kwa wataalam wa masuala ya uhifadhi kuongeza jitihada na mbinu mbalimbali za kiutafiti zitakazosaidia kupunguza changamoto za mimea vamizi katika maeneo ya hifadhi.
Jenerali Mabeyo ametoa rai hiyo wakati wa ziara ya Bodi hiyo katika Kreta ya Ngorongoro kukagua juhudi zinazofanywa na uongozi wa NCAA kukabiliana na athari za mimea vamizi iliyoathiri baadhi ya maeneo ya hifadhi hiyo.
Akiwa katika eneo hilo Jenerali Mabeyo ameona zaidi ya ekari 257 zilizokuwa na mimea vamizi ambazo tayari zimefyekwa kabla ya mbegu zake kukomaa.
Amebainisha kuwa hapo awali kulikuwa na tatizo la uelewa wa namna ya kupambana na mimea hiyo lakini kwa sasa njia ya kufyeka na kuchoma moto mimea yenye mbegu ambazo hazijakomaa kudondosha ardhini imeonyesha kuzaa matunda kwa kiasi kikubwa.
“Zipo tafiti zimefanyika kutatua tatizo la mimea vamizi na zimeonekana kusaidia lakini kuna haja kuendelea kufanya utafiti zaidi wa kujua ongezeko la mimea vamizi ili tuhakikishe kwamba kwa miaka ijayo tatizo hili tunalimaliza kabisa” amesisitiza Jenerali Mabeyo.
Jenerali Mabeyo ameongeza kuwa Serikali iko makini katika kupambana na swala hilo, na bodi yake itashirikiana na wataalam wa uhifadhi kupunguza changamoto hiyo ili kuendelea kudumisha uhifadhi na kuvutia wageni katika eneo muhimu la Ngorongoro ambalo linategemewa na Serikali kuongeza idadi ya watalii na mapato kwa nchi yetu.
Naibu Kamishna wa Uhifadhi NCAA Elibariki Bajuta ameeleza kuwa katika jitihada za kupambana na mimea hiyo NCAA imenunua vifaa ikiweemo matrekta manne na pia inashirikiana na taasisi mbalimbali kama Chuo kikuu cha Sayansi cha Nelson Mandela, Chuo Kikuu cha Dodoma na Taasisi ya utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI) kwa ajili ya kufanya utafiti zaidi na kuona ni njia gani za ziada zitakazosaidia kumaliza tatizo hili kwa haraka.
“Mpango wetu ni kushirikiana na taasisi za kimataifa na kukusanya nguvu ya pamoja ya kutokomeza tatizo hili na pili kuandaa andiko maalum la kupata fedha ili kushirikiana na watafiti wengine wa kimataifa kufanyia kazi jambo hili na kulimaliza katika miaka michache ijayo.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi anayesimamia Idara ya Wanyamnapori, Nyanda za malisho na Utafiti - Victoria Shayo ameeleza Bodi ya Wakurugenzi NCAA kuwa katika eneo la Kreta ya Ngorongoro eneo lililoathirika na mimea vamizi ni kati ya asilimia 17-20.
Amebainisha kuwa kati ya mwezi Aprili hadi Julai mwaka 2023 wamejipanga kufyeka hekta 1000 ambapo hadi tarehe 3 Mei, 2023 hekta 257 zimefyekwa na hekta 743 zinategemewa kufyekwa katika kipindi cha miezi mitatu ijayo kabla mbegu zilizotoa maua hazijakomaa na kudondoka ardhini.
Kwa upande wake Mtafiti mwandamizi kutoka TAWIRI Dkt. Jerome Kimaro ameeleza kuwa pamoja na utafiti wa kupambana na mimea vamizi, wameanzisha mradi unaoitwa Rangeland Care ambao unalenga kuongeza thamani kwa kuzalisha bidhaa ya nishati mbadala ili kuongeza mnyororo wa thamani kwa kuanza na mimea vamizi aina ya makutian.
0 Comments