Ticker

6/recent/ticker-posts

TMA YATOA TAARIFA MWELEKEO MSIMU WA KIPUPWE, JOTO KIASI

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa taarifa ya msimu wa kipupwe katika kipindi cha Juni hadi Agosti (JJA) 2023 ambacho kinatarajiwa kuwa na hali ya joto kiasi hadi baridi ya wastani katika maeneo mengi ya nchi.

Katika taarifa hiyo iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA Dkt. Ladislaus Chang’a Mei 26,2023 ameeleza kuwa, hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa kuwepo katika maeneo ya Nyanda za Juu Kusini -Magharibi pamoja na ukanda wa Ziwa Victoria huku vipindi vya baridi zaidi vinatarajiwa kujitokeza mwezi Juni.

Amesema katika maeneo mengi ya Kanda ya Ziwa Victoria (Mikoa ya Mwanza, Mara, Geita, Kagera, Shinyanga na Simiyu) wanatarajia kuwepo kwa hali ya baridi ya wastani hadi joto la kiasi.

Dkt. Chang’a amesema kiwango cha joto la chini kinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 13 oC na 19 oC.

Kwa Ukanda wa Pwani ya Kaskazini (Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, maeneo ya kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba) Dkt. Chang’a amebainisha kuwa hali ya joto kiasi hadi baridi ya wastani inatarajiwa katika maeneo mengi.

Kwamba kiwango cha joto la chini kinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 22oC na 26oC kwa maeneo ya mwambao wa Pwani na visiwani na kati ya nyuzi joto 19oC na 22oC katika maeneo ya nchi kavu.

Hata hivyo, amesema maeneno yenye miinuko yanatarajiwa kuwa na kiwango cha nyuzi joto chini ya 19oC.

Amesema kwa Kanda ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki (Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara) hali ya joto kiasi hadi baridi ya wastani inatarajiwa katika maeneo mengi, kiwango hicho kinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 13 oC na 21 oC.

Hata hivyo, maeneno yenye miinuko yanatarajiwa kuwa na kiwango cha nyuzi joto chini ya 13 oC.

Kadhalika kwa Kanda ya Magharibi (Mikoa ya Tabora, Rukwa, Katavi na Kigoma) Dkt. Chang’a ameeleza hali ya joto kiasi hadi baridi ya wastani inatarajiwa katika maeneo mengi ambapo joto la chini linatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 15 oC na 19 oC.

Ameendelea kusema kwa Kanda ya kati (Mikoa ya Singida na Dodoma) hali ya joto kiasi hadi baridi ya wastani inatarajiwa katika maeneo mengi ambapo joto linatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 14oC na 19oC.

Kwa Ukanda wa pwani ya kusini (Mikoa ya Mtwara na Lindi) amesema hali ya joto kiasi hadi baridi ya wastani inatarajiwa katika maeneo mengi ambapo joto linatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 16 oC na 22 oC.

Huku kwa Kanda ya kusini (Mkoa wa Ruvuma) akieleza kuwa hali ya joto kiasi hadi baridi ya wastani inatarajiwa katika maeneo mengi ambapo joto linatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 11oC na 16 oC.

Vile vile kwa Kanda ya Nyanda za juu Kusini-Magharibi (Mikoa ya Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe pamoja na maeneo ya kusini ya Mkoa wa Morogoro amesema hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi ambapo joto linatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 7 oC na 16 oC.

Hata hivyo, anasema katika maeneo ya miinuko kiwango hicho kinatarajiwa kuwa chini ya nyuzi joto 7 oC.

Akizungumzia kuhusu mwenendo wa upepo kwa kipindi cha Juni hadi Agosti Mwaka huu Dkt. Chang’a amesma kwa kawaida msimu wa Kipupwe hutawaliwa na upepo wa Kusi.

Hata hivyo, ameeleza msimu wa JJA, 2023 unatarajiwa kuwa na upepo utakaovuma kutoka Kusini-mashariki na Mashariki (Matlai) katika Ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi na maeneo ya nchi kavu.

“Kwa ujumla, upepo wa wastani unatarajiwa kushamiri katika maeneo mengi nchini,” ameeleza Dkt. Chang’a.

Kuhusu mwelekeo wa mvua kwa kipindi cha Juni hadi Agosti Dkt. Chang’a amesema kwa kawaida kipindi cha JJA kinatawaliwa na hali ya ukavu katika maeneo mengi ya nchi.

Hata hivyo, ameeleza upepo kutoka Kusini-Mashariki hadi Mashariki unatarajiwa kuleta unyevunyevu kutoka katika Bahari ya Hindi ambao unaweza kusababisha vipindi vya mvua katika maeneo machache ya ukanda wa pwani (mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani ikijumuisha visiwa vya Mafia, Morogoro, Dar es Salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba

Post a Comment

0 Comments