Ticker

6/recent/ticker-posts

SHUGHULI ZA KILIMO NA UFUGAJI KARIBU NA VYANZO VYA MAJI NI KINYUME CHA SHERIA -NDUGU KAIM



Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2023, Ndugu Abdalla Shaibu Kaim amewaonya wananchi kutokufanya shughuli yoyote ikiwemo kilimo na ufugaji karibu na vyanzo vya maji kwani ni kinyume cha sheria na ni uharibifu wa Mazingira.

Ameongeza kwa kusema kuwa hairuhusiwi kwa mtu yeyote kufanya shughuli zozote za kibinadamu ndani ya mita 60 kutoka kwenye vyanzo vya maji.

Ameyasema hayo wakati wa ziara ya Mwenge wa Uhuru Kitaifa ya kukagua utekelezaji wa mradi wa utunzaji Mazingira unaotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwenye mradi wa maji Kigamboni.

“Hatua hii ni muhimu kwa ajili ya kulinda na kuviendeleza vyanzo vya maji pamoja na uoto wa asili ikizingatiwa kuwa maji ni uhai. Sambamba na kuunga mkono juhudi za Serikali za upandaji miti rafiki yenye kutunza mazingira katika vyanzo vyetu vya maji." amesisitiza Ndugu Kaim.

"Sheria, miongozo na kanuni zipo wazi kwani tunafanya hivyo kwa ajili ya kutunza vyanzo vya maji kwa kuwa maji ni uhai," ameeleza.

"Niwapongeze DAWASA kwa jitihada kubwa mnazozifanya za kulinda na kuendeleza Mazingira kwa kutunza vyanzo vya maji, mnafanya kazi nzuri, niwapongeze sana." ameeleza Ndugu Kaim.

Kwa upande wake Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Ndugu Kiula Kingu amesema kuwa katika jitihada za kutunza na kuendelea vyanzo vya maji katika mradi wa maji Kigamboni, Mamlaka imefanikisha kupanda miti ya matunda na kivuli takribani miti 3,300.

"Huu ni mpango endelevu ambapo katika awamu ya kwanza tumeanza kupanda miti 1,800 kwenye eneo la tenki kubwa la maji." amesema.

Amebainisha kuwa mpango wa upandaji miti Kigamboni ulitekelezwa kwa kushirikisha wananchi wa maeneo jirani kwa kuwapa elimu ya umuhimu wa utunzaji wa Mazingira ili waweze kutunza na kunufaika na mazao ya miti hii.

"Utunzaji wa Mazingira ni mojawapo ya kipaumbele cha Mamlaka kwa kuwa tunaelewa uendelevu wa huduma ya maji unategemea usalama wa vyanzo vya maji, hivyo DAWASA imeweka nguvu kubwa katika kuhakikisha vyanzo vya maji ikiwemo vya Mto Ruvu na visima virefu vinalindwa ipasavyo." ameeleza Ndugu Kingu.

Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa zimeongozwa na kauli mbiu Tunza Mazingira, okoa vyanzo vya maji kwa Ustawi wa viumbe hai kwa uchumi wa Taifa.

Post a Comment

0 Comments