Wauguzi wakiwa katika maandamano kuadhimisha Siku ya Wauguzi Duniani yaliyofanyika katika ukumbi wa kambi ya JKT Maramba, Wilaya ya Mkinga.
Wauguzi wakila kiapo mbele ya mgeni rasmi, mkuu wa Mkoa.
********************
Na Hamida Kamchalla, MKINGA.
VIONGOZI wa kisiasa Mkoa wa Tanga wamepigwa marufuku kutoingilia masuala ya taaluma hasa ya uuguzi kwa kuwatolea maneno ya kashfa ikiwa ni pamoja na kuwadhalilisha wanapokuwa kwenye majukumu yao.
Hali hiyo imekuja baada ya wauguzi wa Mkoa wa Tanga kulalamikia kero ya viongozi hao kuwaingilia katika majukumu yao na kusababisha kukosa uhuru na are ya ufanyaji wao wa kazi.
Akiongea na wauguzi hao, mkuu wa Mkoa wa Tanga Waziri Kindamba amesema hakuna kiongozi yeyote wa siasa kugusa sekta ya Afya kwakuwa ipo Bodi yao ambayo inasimamia masuala yao kwa mujibu wa utumishi wa umma.
"Wanasiasa, si mwenyekiti, mtendaji, diwani wala mbunge kwenda kuingilia kazi za uuguzi, napiga marufuku katika Mkoa wa Tanga, taaluma hii ina vyama na bodi zao, acheni mambo ya wauguzi yamalizwe na vyombo vyao vinavyowasimamia" amesema.
Aidha Kindamba amewataka wauguzi kufanya kazi zao kwa weledi kwa kuwapokea na kuwahudumia vizuri wagonjwa ili kuepuka malalamiko ya wananchi lakini pia kuwaahidi kwqmba serikali iko bega kwa bega nao katika kutatua kero zao ikiwa ni kuongezwa posho za muda wa ziada ambazo zipo kikanuni pamoja na nyumba za wauguzi.
"Wauguzi, muwe na mtazamo mzuri wa upokeaji na utaoaji huduma bora na kwa weledi, najua siyo wote lakini wapo wanaolalamikiwa, nendeni mkajitathimini, niwatake wauguzi wote Mkoa wa Tanga wawe na kali nzuri kwa wagonjwa pamoja na wanaosindikiza wagonjwa" amesisitiza.
Awali akisoma risala, Mwenyekiti wa Chama cha Wauguzi Mkoa wa Tanga Abeid Njopa ameiomba serikali kuingilia kati suala la wanasiasa wanaowadhalilisha na kuwatolea maneno ya kashfa wauguzi wanapokuwa wakitimiza majukumu yao.
"Tuna kero ya wanasiasa, wenyeviti, watendaji, na hata madiwani kuingilia taaluma ya uuguzi, ikiwa ni pamoja na kuwatolea maneno ya kukatisha tamaa, kumdhihaki wakati mwingine hata kumdhalilisha muuguzi, hali hii inavunja morali ya ufanisi wa kazi, pia inawaumiza sana wauguzi" amesema
Njopa amebainisha kwamba mbali na hilo, pia Mkoa una upungufu wa wauguzi ikilinganishwa na wingi wa wagonjwa, ambapo kwasasa wapo wuguzi 1,267 sawa na asilimia 39.3, pungufu ya wauguzi ni 2,024 asilimia 60.7 na mahitaji ni wauguzi 3,224, hivyo kufanya wauguzi kuhudumia wagonjwa kwa masaa ya ziada.
"Tunaomba tuwe tunapewa kipaumbele katika ulipwaji wa stability mbalimbali ikiwemo nauli za likizo, malipo ya saa za ziada, kupandishwa madaraja na kubadilishwa vyeo baada ya kutoka shule kwani haya yanaongeza molari na ufanisi wa kazi kwa wauguzi" amesema Njopa.
Mbali na kero hizo, amefafanua kuwa kwa mwaka 2022 wauguzi wamefanikiwa kuokoa vifo vya akina mama wakati wa kujifungua na kyweza kuzalisha akina mama 67,741.
0 Comments