NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimetoa Mapendekezo ambayo Rasimu ya Sera ya Elimu haijazingatia ikiwemo baadhi ya Taasisi kama vile Maafisa Elimu Utamaduni, Maafisa Elimu TEHAMA na Maafisa elimu wengine kutotambuliwa na rasimu ya sera licha ya nafasi hizo kuwepo katika mfumo wa elimu nchini hivyo basi wanapendekeza nafasi hizo zitambuliwe.
Akizungumza na Waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Wakili Anna Henga amesema rasimu ya sera itoe ufafanuzi wa kina juu ya dhana ya elimu isiyo katika mfumo rasmi ni elimu ya namna gani ili kuondoa mchanganyiko uliopo mpaka sasa.
Amesema rasimu ya sera ielekeze ni namna gani wanafunzi waliopatia katika mkondo wa elimu isiyo rasmi watatambuliwa kwenye mfumo wa elimu rasmi.
"Rasimu ya Sera ya elimu ifungamanishwe na sera nyinginezo zinazoongelea kwa namna moja ama nyingine ujuzi na maarifa kama vile sera ya sayansi na teknolojia, sera ya viwanda vidogovidogo ili kuwa na zao la wahitimu wenye ujuzi na maarifa zaidi". Amesema Wakili Anna.
Aidha Wakili Anna amesema dhana ya elimu bila malipo iwekwe bayana kutokana na ukweli kwamba lugha iliyotumika katika rasimu inaashiria dhana ya elimu bila malipo kutokuwa bure kiuhalisia, lugha iliyotumika inaashiria dhahiri shahiri kuwa elimu haitokuwa bure bali kutakuwa na michango kadhaa.
Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Wakili Anna Henga akizungumza na waandishiwa ha habari leo Mei 11,2023 katika ofisi za LHRC Jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Wakili Anna Henga akizungumza na waandishiwa ha habari leo Mei 11,2023 katika ofisi za LHRC Jijini Dar es Salaam
0 Comments