Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira Mhe. Jackson Kiswaga,akizungumza Mei 6,2023 baada ya kupokea Wasilisho la hali ya Bwawa la Mtera,Kamati hiyo ilipofanya ziara.
Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso , akizungumza mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira wakati wa ziara ya Kamati hiyo ilipotembelea Bwawa la Mtera Mei 6,2023.
Waziri wa Maji Mhe.Jumaa Aweso (kulia ) akiteta jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya MajiSafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) Mhandisi Aron Joseph (Kushoto),wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira ilipotembelea Bwawa la Mtera Mei 6,2023.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira wakiendelea na ziara yao katika Bwawa la Mtera lengo ni kukagua na kujua maendeleo ya Bwawa hilo,ziara hiyo imefanyika Mei 6,2023.
Waziri wa Maji Mhe.Jumaa Aweso (mbele),akiambatana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira katika ziara ya kutembelea Bwawa la Mtera kujionea hali ilivyo katika Bwawa hilo.
Na Okuly Julius-Dodoma
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira Mhe. Jackson Kiswaga amesema ili Mradi wa kutoa Maji Bwawa la Mtera kuleta Jijini Dodoma ufanikiwa ni vyema sekta zote husika zishirikiana katika utunzaji wa vyanzo vinavyopeleka maji katika Bwawa hilo.
Pia amewataka watu wa Mazingira kuhakikisha wanatekeleza Sheria ya kuwaondoa wananchi wanaolima kandokando Mwa Bwawa hilo kwa sababu ni kinyume na Sheria na kusema kuwa hao hawana tofauti na Wavamizi.
Mhe.Kiswaga ameyasema hayo Mei 6,2023 wakati Kamati hiyo ilipotembelea Bwawa la Mtera kwa lengo la kujiridhisha iwapo maji hayo yanatosha kuanzisha mradi wa huo ambao utasaidia kuongeza uzalishaji wa maji kwa ajili ya kuhudumia Jiji la Dodoma.
Kamati hiyo imeambatana na wataalamu kutoka Wizara ya Maji na Sekta mtambuka ikiwemo Wizara ya Nishati, Wizara ya Fedha na Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira ambao walishirikiana katika kutoa wasilisho juu ya maendeleo ya Bwawa la Mtera.
"tumetembelea maeneo mbalimbali ya bwawa hili tumeangalia na kupitia taarifa mbalimbali za watalamu, na tutakaa tena pamoja tujadiliane ili maamuzi tutakayofanya yasiathiri shughuli nyingine za kijamii na kiuchumi,"
Na kuongeza kuwa "tunatambua umuhimu wa bwawa hili katika kuzalisha nishati ya umeme na pia tunatambua mahitaji makubwa ya maji katika jiji la Dodoma ambalo ni makao makuu ya nchi lakini tunawajibu pia wa kuhakikisha uamuzi utakaofanyika hauathiri eneo lolote,"amesema Mhe.Kiswaga
Kwa upande wake Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso amepongeza kamati hiyo kwa kuamua kutembelea eneo hilo ili kuwa na wazo la pamoja ambalo litasaidia kuondoa adha ya huduma ya maji kwa wananchi.
Amesema Wizara ya Maji inaendelea na hatua mbalimbali ikiwemo kupata ushauri wa Mtaalamu mshauri ili maamuzi yatakayo fanyika yasiathirii shughuli nyingine za kijamii.
Amesema mahitaji ya jiji la Dodoma ni lita za ujazo milioni 133 kwa siku ambapo kwa sasa jiji linazalisha lita za ujazo milioni 68 kwa siku.
Kiwango kitakachochukuliwa katika mradi huo ni lita za ujazo milioni 130 kwa siku.
Amesema bado Wizara ya Maji inaendelea na mipango mbalimbali kuhakikisha jiji la Dodoma linaondokana na changamoto ya huduma ya maji.
0 Comments