Ticker

6/recent/ticker-posts

WELLWORTH WASONONESHWA NA UPOTOSHAJI WA MBUNGE



Na Selemani Msuya


KAMPUNI ya Wellworth inayojihusisha na uwezekezaji katika sekta ya hoteli za kitalii nchini imeeleza kusikitishwa na tuhumu za kuwa wameshindwa kuendeleza Hoteli ya Embassy, Kunduchi Beach na Mikumi Lodge kwa miaka 14.


Kauli hiyo ya kusikitishwa imetolewa na Ofisa Sheria na Utawala wa Wellworth, Saimon Nguka, wakati akijibu tuhuma zilizotolewa na Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Katavi Taska Mbogo, alizozitoa Februari mosi Bungeni jijini Dodoma.


Nguka ambaye alikuwa akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, amesema kampuni yao imesikitishwa na taarifa walizodai ni za uongo zilizotolewa na mbunge huyo na kutoa rai kwa wabunge na viongozi wengine wa umma kutafuta taarifa sahihi kabla hawajatoka hadharani kuzungumza.


“Februari mosi Mbunge wa Viti Maalum, Taska Mbogo alitolea mfano hoteli zetu za Embassy, Kunduchi Beach na Mikumi Lodge, kwamba tangu zibinafsishwe ni takribani miaka 14 sasa, lakini hakuna shuguli inayoendelea.


Aliendelea kudai kiwa ndani kila kitu kimeharibika na kwamba mwekezaji aliyepewa hoteli hizo ni mmoja, hivyo amevunja mkataba wa ubinafsishaji na haoni sababu ya Serikali kuendelea kumbembeleza, bali aandikiwe barua ya kuja mezani kwa maridhiano,” alinukuu maneno ya Mbunge.


Ofisa huyo alisema taarifa hiyo ambayo ametoa mbunge huyo Februari mosi ilikuwa ya uongo na wao kama kampuni wameandika barua mara mbili kumueleza Spika kuwa mbuge huyo amepotosha umma na kumueleza ukweli ulivyo, ila hawajapata majibu, hivyo wamelazimika kujitokeza na kuelezea hali halisi.


Nguka amesema Kampuni ya Wellworth haijatelekeza hoteli yoyote na taarifa kuwa wamekaa miaka 14 bila kuendeleza ni uongo wa mchana kweupo akitolea mfano kuwa Januari 6, 2018 ndio walipata barua ya kibali namba NaTNP/HQ/P.30/17 cha ujenzi wa Mikumi Wildlife Lodge.


Lakini wameingia mkataba Januari 30,2021 na sio kama anavyodai Mbunge Mbogo.


“Tunapenda kuwajulisha kwamba pamoja na zoezi la kusaini mkataba miaka miwili iliyopita, ila shughuli za ukarabati zinaendelea, baada ya kukamilisha taratibu zote za kisheria na matarajio yao ni mapema mwaka 2024 tutaanza kutoa huduma na kuajiri zaidi ya watanzania 96,” amesema.


Akifafanua kuhusu Hoteli ya Embassy, Nguka amesema Kampuni ya Wellworth imenunua jengo kutoka kwa Kampuni ya Enterprise Tanzania Limited na sio kwamba imebinafsishiwa kama alivyodai mbunge huyo na kwamba kuchelewa kwa ujenzi kunatokana na kesi ambazo zipo mahakamani.


“Tulinunua jengo hilo kutoka kwa muuzaji na sio Serikali kwa utaratibu wa biashara ya kawaida, ila kuna kesi zimefunguliwa makamani, hivyo zikiisha tutaendelea na uwekezaji kwani tulishakamilisha michoro ya ujenzi ili Embassy Hoteli iwe ya nyota tano.


Tulikamilisha taratibu za kupata mkopo wenye thamani ya dola za Marekani milioni 23 kutoka mabenki mbalimbali, ili kujenga jengo lenye ghorofa 13, hivyo nia ya kuendeleza ipo, tunadhani mbunge hakuwa na taarifa sahihi,” amesema.


Aidha, Nguka amesema Hoteli ya Kunduchi Beach kwa sasa wanaendelea na ukarabati ili iwe na hadhi ya nyota tano ambapo ikikamilika itakuwa inasimamiwa na kampuni kubwa ya uendeshaji wa hoteli za kimataifa.


Ofisa huyo amesema hoteli hiyo ikikamilika itaweza kutoa ajira za moja kwa moja kwa watu zaidi 220, hivyo kuwezesha Wellworth kuajiri zaidi ya watu 800.


Amesema ukarabati wa Kunduchi Beach umechelewa kutokana na urasimu wa utoaji kibali unaofanywa na baadhi ya maofisa wa Serikali.


“Bila msaada wa Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) na Ofisi ya Msajili wa Hazina, hadi sasa kungekuwa hakuna ukarabati, ila kwa sasa kazi inaendelea kama anavyotaka Rais Samia Suluhu Hassan na matarajio yetu 2024 huduma zitaanza kutolewa,” amesema.


Naye Ofisa Masoko Mwandamizi wa Wellworth, Josephine Makundi amesema kampuni hiyo kwa sasa inamiliki hoteli 22 ambazo zinaweza kulaza watu zaidi 1,000 kwa siku.


Makundi amesema iwapo biashara ya hoteli hasa za kitalii itaendelea kuimarika wataweza kutoa ajira kwa watanzania wengi na kuchangia pato la taifa.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Kundi la Makampuni ya Wellworth, Zulfikar Ismail amesema wamejipanga kuongeza uwekezaji ili kuunga mkono juhudi za Rais Samia katika kukuza uchumi.


“Sisi tunaataka siku chache zijazo tuwe kampuni ya wazawa ambayo inaongoza katika sekta ya hoteli nchini, na hili linawezekana kwani kwa sasa tuna hoteli 22 ambazo zina uwezo wa kuchangia zaidi Sh.bilioni 6 kwenye pato la taifa kwa mwaka, tunaomba wasaidizi wa Rais wasiwe kikwazo,” amesema.


Ismail amesema hadi sasa wamewekeza zaidi ya dola milioni 200 za Marekani ambazo ni takribani bilioni 500, hivyo wamedhamiria kuipaisha sekta hiyo kwa kujenga mahoteli ya kisasa ambayo yatavutia watalii kote duniani.

Post a Comment

0 Comments