Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MKUU: SHERIA ZA TANZANIA ZINAKATAZA VITENDO VYA ULAWITI

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitoa maelezo kuhusu hoja mbalimbali za wabunge wakati alipohitimisha hoja ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa Mwaka 2023/2024. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Mawaziri Jenista Mhagama , Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) na Profesa Joyce Ndalichako, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) wa pili kulia wakati Bunge lilipokuwa katika maandalizi ya kuwa Kamati ya Matumizi baada ya Waziri Mkuu kutoa maelezo kuhusu hoja mbalimbali za wabunge wakati alipohitimisha hoja ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa Mwaka 2023/2024. Kulia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Patrobas Katambi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

***************

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema sheria za Tanzania zinakataza bayana vitendo vinavyokinzana na tamaduni, mila na desturi na zimeweka adhabu mbalimbali kwa makosa ya namna hiyo na yale ya udhalilishaji kwa watoto ikiwemo ulawiti.



“Ninapenda kuliarifu Bunge lako kuwa sheria zetu hapa nchini, zinakataza bayana vitendo hivyo na zimeweka adhabu mbalimbali kwa makosa ya namna hiyo na yale ya udhalilishaji kwa watoto ikiwemo ulawiti. Pia, sheria zinakataza kuweka kwenye mitandao maudhui yanayochochea mahusiano ya jinsi hiyo au maonesho ya sanaa yanayochochea vitendo vinavyoashiria mmomonyoko wa maadili yetu,” amesema.



Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Aprili 13, 2023) wakati akihitimisha hoja zilizotolewa na Wabunge wakati wakijadili Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2023/2024.



Amesema uwepo wa matukio yanayokinzana na tamaduni, mila na desturi za Kitanzania, umehatarisha uimara na ustawi wa familia na mustakabali wa Taifa kwa ujumla.



Waziri Mkuu amezitaja baadhi ya sheria hizo kuwa ni Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 ya Sheria za Tanzania, ambayo inatamka bayana kuwa vitendo vya mapenzi ya jinsia moja au kinyume na maumbile, iwe kwa faragha au kwa makubaliano ni kosa la jinai.



“Sheria hiyo pia inakataza udhalilishaji wa watoto kwenye matendo yanayofanana na hayo pamoja na kuweka adhabu kwa kosa la kujaribu kufanya vitendo vilivyokatazwa chini ya sheria husika,” amesema.



“Kanuni za Maudhui ya Mtandaoni chini ya Tangazo la Serikali Na. 538 la mwaka 2020, zinakataza kuweka mtandaoni maudhui yenye kuonesha mahusiano ya jinsia moja sambamba na adhabu zake na Sheria ya Makosa ya Kimtandao, Sura ya 22, inazuia kutangaza au kusababisha machapisho ya ngono au matusi kupitia mfumo wa kompyuta au mfumo mwingine wowote wa kiteknolojia,” ameongeza.



Waziri Mkuu amesema Kanuni za Baraza la Sanaa la Taifa za mwaka 2018, zinaweka masharti kwamba hakuna kazi ya sanaa itakayopelekwa sokoni kwa walaji kabla ya kupewa kibali cha kuthibitisha kuwa maudhui yamezingatia maadili. “Baraza katika kuhakiki maadili ya maudhui litajiridhisha kuwa kazi ya sanaa haishawishi wala kuhamasisha vitendo vya ngono, ushoga, usagaji au matumizi ya dawa za kulevya,” amesisitiza.



Amesema Serikali imepokea hoja na michango iliyowasilishwa na itaielekeza Tume ya Marekebisho ya Sheria izipitia sheria hizo, kuzifanyia utafiti wa kina na wa kitaalamu ili kubaini mapungufu yanayojitokeza katika utekelezaji na kufanya maboresho.



Pia Waziri Mkuu ametoa nitoe wito kwa taasisi zote zilizo na wajibu wa kusimamia sheria, kanuni na taratibu mbalimbali kama vile Jeshi la Polisi, BASATA na TCRA kutosita kuchukua hatua kwa yeyote atakayebainika kukiuka misingi ya taratibu zetu zilizojiwekwa.



Wakati huohuo, Waziri Mkuu amewataka wazazi na walezi waimarishe uhusiano na urafiki na watoto wao ili waweze kupata taarifa za viashiria na uwepo wa vitendo vya ukatili dhidi ya watoto. “Jengeni utamaduni wa kutenga muda wa kuwasikiliza watoto ili kujua kinachoendelea katika maisha yao ya nyumbani, mtaani na shuleni na kuchukua hatua stahiki ikiwemo za kisheria inapobidi,” amewasihi.



Amewaomba viongozi wa dini waendelee kuwakumbusha waumini wao wazingatie maadili na kushiriki kikamilifu kuwalea watoto kiroho, kuwahimiza wawe waadilifu na kuepuka vitendo visivyokubalika katika jamii.



Amewaomba Wabunge waendelee kuiunga mkono Serikali katika suala la ulinzi wa mtoto wa Kitanzania na usimamizi wa maadili. “Sote kwa nafasi zetu tuendelee kuihimiza jamii na kuwa mfano katika kutekeleza sheria tulizozitunga sisi wenyewe na kutunza mila, desturi na tamaduni zetu,” amesisitiza.



Kwa upande mwingine, amezitaka Wizara za kisekta zisimamie kikamilifu sheria, kanuni na miongozo iliyopo pamoja na kuchukua hatua za kisheria kwa wote watakaobainika kufanya vitendo kinyume cha sheria na maadili ya Taifa.



Amezitaka Asasi za Kiraia zitekeleze majukumu yao kwa mujibu wa vibali vyao vya usajili. “Kwa taasisi zitakazobainika kwenda kinyume na malengo ya usajili ikiwemo kuhamasisha mmomonyoko wa maadili na vitendo vinavyokinzana na mila, tamaduni na desturi zetu, zitachukuliwa hatua za kisheria.”

Post a Comment

0 Comments