Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt. Angeline Mabula akisikiliza kero za wakazi wa jiji la Dodoma waliokuja kwa ajili ya kupata huduma za sekta ya ardhi katika Ofisi za Halmashauri ya jiji la Dodoma.
Baadhi ya wakazi wa jiji la Dodoma waliokuja kwa ajili ya kupata huduma za sekta ya ardhi katika Ofisi za Halmashauri ya jiji la Dodoma.
**********************
Na. Hassan Mabuye, Dodoma
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt. Angeline Mabula amewataka maafisa wa sekta ya ardhi nchini kuwafuata na kuwahudumia wananchi katika mitaa yao ili kutoa huduma za ardhi kwa ufanisi.
Waziri Mabula ameyasema hayo wakati alipofanya ziara ya kushtukiza leo tarehe 20 Aprili 2023 katika ofisi za Halmashauri ya Jiji la Dodoma zinazotoa huduma za ardhi kwa wananchi ambapo alikuta msongamano mkubwa usiofuata utaratibu unaosababisha kero nyingi kutoka kwa wananchi ambao walimfikishia kero hizo.
“kuanzia wiki ijayo sitaki kukuta watu hapa, fanyeni Cliniki za ardhi kwa muwafuate kwenye mitaa yao wanako husika na mimi ntapita kwenye maeneo hayo halafu nikute hamjaenda ntachukua hatua stahiki kwa sababu kama ni huduma ya kuanzia kwenye maombi mpaka mtu anapata hati kwa nini mrundikane hapa wakati unaweza kuifanya katika mitaa yao huko huko” Amesema Dkt. Mabula.
Dkt. Mabula amewataka maafisa wanaohudumia wananchi kuongeza muda wa kazi kuanzia saa 2 kamili asubuhi hadi saa 12 kamili jioni badala ya muda wa awali ambao walikuwa wanamaliza saa tisa alasiri jambo ambalo wananchi wengi wamelilalamikia na kuomba kuwe na utaratibu mzuri wa utowaji huduma bila upendeleo.
“kama mikoa mingine wameweza kufanya utaratibu wa kuwafuata wananchi katika mitaa yao kwanini Dodoma isifanyike?, Dar es salaam wanawafuata wananchi mitaani na kuwahudumia, Mwanza wanafanya hivyohivyo kila siku, Shinyanga wanawafuata wananchi kila siku na hata mkoa wa Mara wanawafuata wananchi kila siku mitaani na kuwahudumia, kwanini sisi hapa Dodoma tupo ofisini tu na kuwasumbua wananchi hapa?” Alihoji Dkt. Mabula.
Aidha, Waziri Mabula amekemea tabia inayofanywa na maafisa wa sekta ya ardhi ya umilikishaji wa kiwanja kimoja kwa watu wawili au zaidi unaojulikana kama Double Allocation ambao kwa jiji la Dodoma unaonekana kushamiri na kusababisha malalamiko na migogoro mingi ya ardhi.
“Ntawachukulia hatua watu wote wanaosababisha Double Allocation sababu kesi kama hizi zimekuwa nyingi sana kwa jiji la Dodoma ambapo maafisa wanamilikisha watu zaidi ya mmoja katika kiwanja kimoja na mimi ni shahidi wa hilo. Kwa hiyo Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Dodoma anza kuorodhesha kwa kuigawa migogoro inayofanana kwa makundi ili huduma zitofautiane” Ameongeza Dkt. Mabula
Dkt. Mabula ametumia fursa hii kuwafahamisha wananchi kuwa kwa sasa Wizara yake ipo katika kuboresha mfumo wa taarifa za ardhi kwa kutoa huduma kwa njia ya mtandao wa simu ambapo wananchi watafanya miamala ya huduma za sekta ya ardhi kupitia simu zao.
0 Comments