Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (kulia) akizungumza wakati wa ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (hayupo pichani) Wilayani Ilemela, Mkoani Mwanza. Katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Adam Malima
**********************
Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amewatoa hofu wananchi wa Jiji la Mwanza na viunga vyake kuhusiana na adha ya maji wanayopitia kipindi hiki kuwa Serikali inatambua na jitihada za makusudi zimechukuliwa kuhakikisha adha hiyo inashughulikiwa.
Waziri Aweso amesema hayo Aprili 12, 2023 mbele ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango wakati wa ziara yake kwenye Manispaa ya Ilemela Mkoani Mwanza.
“Naomba niwaambie ndugu zangu wana Ilemela kwamba baada ya dhiki sio dhiki baada ya dhiki ni faraja na faraja yenu ni Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mhe. Dkt Philip Isdor Mpango,” amesema Waziri Aweso.
Amebainisha kuwa Serikali inatambua upungufu wa huduma ya maji inayowakabili wananchi wa Jiji la Mwanza na viunga vyake na hususan maeneo ya Buswelu na Ilemela yote kwa ujumla na kwamba ufumbuzi umepatikana.
“Mahitaji ya maji Jiji la Mwanza ni lita milioni 160 za maji wakati mitambo yetu ya Capripoint uwezo wake ni kuzalisha lita milioni 90 maana yake ni kwamba kuna ongezeko la mahitaji ya maji ikilinganishwa na uzalishaji uliopo sasa,” amebainisha Waziri Aweso.
Hata hivyo, Waziri Aweso amebainisha hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ikiwa ni pamoja na ujenzi wa dakio lingine kubwa la maji (chanzo kipya cha maji) eneo la Butimba ambalo kwa awamu ya kwanza litazalisha lita milioni 48 za maji kwa siku.
“Baada ya kuona upungufu huu wa maji, ukienda eneo la Butimba tuna mradi wa maji wa zaidi ya shilingi bilioni 69 mradio huu uliukagua na ulitupa maelekezo baada ya kutuwekea jiwe la msingi,” amefafanua Waziri Aweso.
Amesema mradi huo wa Butimba upo katika hatua nzuri kwani tayari ujenzi wa matenki na machujio umekamilika na kwamba changamoto ilikuwa pampu ambazo ziliagizwa nje ya nchi hata hivyo nazo zimefika na hatua ya usimikaji wake inaanza hivi karibuni ili ifikapo Mwezi Juni mradi uwe umeanza kutoa maji.
Baada ya kubainisha hali halisi ya upatikanaji wa huduma ya maji Jijini Mwanza na hatua zilizochukuliwa na Serikali, Waziri Aweso ameielekeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) yenye dhamana ya kuwafikishia maji wananchi wa Jiji la Mwanza kuhakikisha wakati huu wa upungufu wa maji wahakikishe wanakuwa na migao ya maji yenye tija ili kila mwananchi anufaike.
“MWAUWASA pamoja na kwamba mnazalisha lita milioni 90 za maji lazima mgao uwe fair; maelekezo tunayotoa ni mgao kuwa wa haki sio hawa wapate siku nane wengine siku moja na wengine hawapati kabisa, hiki kilichopo lazima kisimamiwe ili wananchi wengine ikiwemo wanabuswelu wanapata maji safi na salama,” amesema Waziri Aweso.
Aidha, Waziri Aweso amesema Serikali kupitia Wizara ya Maji imetoa shilingi milioni 500 kwa ajili ya kutanua mtandao wa usambazaji maji Kata ya Buswelu Wilayani Ilemela na ameielekeza MWAUWASA kuhakikisha ndani ya Wiki Sita shughuli hiyo iwe imekamilika na wananchi wapate huduma.
0 Comments