Ticker

6/recent/ticker-posts

SERIKALI KUHAKIKISHA MIRADI INATEKELEZWA KWA VIWANGO



Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imesema itaendelea kuhakikisha miradi ya mazingira katika maeneo mbalimbali nchini inatekelezwa kwa kiwango kinachotakiwa ili iwanufaishe wananchi na kutatua changamoto za kimazingira.

Pia, imesema itashirikiana na Wizara nyingine za kisekta kuona namna namna bora ya kuvuna maji ili kudhibiti mafuriko yanaoyakumbuka maeneo mbalimbali nchini na kusababisha adha kwa wananchi.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis leo Aprili 19, 2023 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Serengeti Mhe. Jeremiah Mrimi.

Katika swali la msingi Mhe. Mrimi alitaka kujua mpango wa Serikali wa kudhibiti mafuriko katika Mto Mara kwa kuvuna maji yake kupitia mabwawa na kujenga skimu za umwagiliaji.

Akiendelea kujibu swali hilo Mhe. Khamis amesema kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais ina utaratibu wa kutembelea na kukagua miradi inayoratibiwa na Ofisi hiyo na kutoa maelekezo ikamilike kwa wakati na kwa kiwango.

Amebainisha kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais tayari imezindua Mpango Kabambe wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (2022-2032) ambao umeelezea mikakati na shughuli endelevu zinazoweza kufanyika ili kuhifadhi mazingira.

“Mheshimiwa Spika, Mto Mara ni moja ya mito mikubwa na muhimu nchini Tanzania. Hivyo, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais na Wizara nyingine za kisekta zitakaa na kuona namna bora ya kuvuna maji ili kudibiti mafuriko,” amesema.

Mhe. Khamis amefafanua kuwa Serikali itaimarisha usimamizi wa vyanzo vya maji na kuhakikisha uwepo wa mtiririko wa uhakika katika mito ikiwemo mito mbalimbali ikiwemo Mara, Kagera, Ruaha Mkuu, Momba, Lufurio, Wami na Ruvuma.

Aidha, Naibu Waziri huyo amesema pia Serikali itahamasisha matumizi sanifu kwa watumiaji wote wa mito hiyo pamoja na kuimarisha viwango vya maji katika vyanzo mbalimbali vya maji vilivyopo hapa nchini.

Ikumbukwe Mpango Kabambe wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (2022-2032) ulizinduliwa Juni 05, 2022 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa wakati wa kilele cha Siku ya Mazingira Duniani jijini Dodoma.

Post a Comment

0 Comments