Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hajjat. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi kuendelea kudumisha amani na utulivu iliyopo Nchini ili kutoa fursa kwa Serikali kuweza kuwaletea maendeleo wananchi wake.
Rais Dkt. Samia ameyasema hayo katika Salamu zilizotolewa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla alipomuwakilisha katika Futari aliyoandaa kwa wananchi wa Mikoa Miwili ya Pemba iliyofanyika katika ukumbi wa ZSSF Tibirinzi Mkoa wa Kusini Pemba.
Amesisitiza kuendeleza Amani na mshikamano uliopo baina yao ili kujipatia maendeleo endelevu.
Aidha amewataka wazazi na walezi kuendelea kusimamia mila na Tamaduni za Kitanzania ili kuiweka jamii katika maadili yaliyo mema.
Amesema Tanzania ni nchi iliyobarikiwa ustaarabu ambapo Taifa linajivunia tunu hiyo.
Pamoja na hayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amewashukuru wananchi hao kwa kuitikia mualiko huo hatua ambayo inaonesha namna wananchi wanavyounga Mkono juhudi zinazofanywa na Serikali zao zote mbili.
Ameeleza kuwa mkusanyiko huo umedhihirisha mapenzi baina ya wananchi na viongozi wao kwa kufutari pamoja na kupata fadhila kutoka kwa mola wao hasa katika kipindi hichi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani ikiwa ni sehemu ya Ibada.
Akizungumzia kwa niaba ya wananchi wa Mikoa miwili ya Pemba Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mhe. Matar Zahor Masoud ameeleza faraja ya wananchi hao kwa fursa mbali mbali zilizoelekezwa kisiwani Pemba hatua ambayo inaonesha namna Serikalai inavyowajali wananchi hao.
Aidha ameeleza kuwa wataendelea kusimamia miradi mbali mbali ya maendeleo iliyoelekezwa Pemba ikiwemo ujenzi wa Hospitali za Wilaya, ujenzi wa Skuli za kisasa za msingi na sekondari, pamoja na ujenzi wa Miundombinu ya Barabara na uwanja wa ndege wa kimataifa.
0 Comments