* Walimkataza kutoka nje kuhofia watu watamkimbia au kumpiga kutokana na ugonjwa wake
* Alihangaika sana na kukata tamaa, sasa amshukuru Rais Samia kwa kuokoa maisha yake
Na Mwandishi Wetu
"Nilisikia Rais Samia anapita Nyakanazi na mimi kwetu ni pale pale Nyakanazi. Wazazi walinikataza, wewe usiende na hali hiyo uliyokua nayo watu wanakukimbia. Unaenda kufanya nini, watakupiga."
Hayo ni maneno ya Hamimu Mustapha Baranyikwa (15), mkazi wa kijiji cha Nyakanazi, Biharamulo, Mkoani Kagera, akisimulia tukio la tarehe 16 Oktoba, 2022, ambalo kamwe hatalisahau katika maisha yake.
"Kaka yangu akaniambia wewe nenda, itakavyokuwa itakuwa. Ninachojua (Rais) anaweza kukusaidia. Mimi kweli niliamka usiku sana ili wazazi wasinione, maana kama wangeniona wangenikataza."
Hamimu, ambaye wazazi wake walihangaika kumpeleka kwa waganga wa kienyeji na hata kuuza mali za familia bila mafanikio, alikuwa amekata tamaa kama angekuja kupona ugonjwa wake wa ajabu
Ngozi yake ilikuwa imeharibika, uso wake ukawa hautazamiki hadi watu wazima na watoto wakawa wanamkimbia na alishindwa hata kukunja na kukunjua vidole vya mikono yake kutokana na maradhi hayo.
Wahenga wanasema penye nia pana njia. Rais Samia Suluhu Hassan alipofika Nyakanazi wakati wa ziara yake ya mkoa wa Kagera, alimuona mtoto huyo amekaa pembeni ya barabara akiwa amenyong'onyea akawatuma wasaidizi wake waende kuongea naye wajue tatizo lake ni nini.
"Nilipofika nikakaa pembezoni mwa barabara. Ule msafara wake (Rais Samia) ulipofika, yale magari yake wakaniona. Waliokuwa wanaongozana naye (Rais) wakaniuliza maswali... Kuna mmoja aliyekuwa ameongozana nao ni dokta, akanishika ngozi yangu," alisema Hamimu.
Kwa mujibu wa kijana huyo, daktari aliyekuwepo kwenye msafara wa Rais Samia akasema kuwa akipelekwa Muhimbili wanaweza kujua chanzo cha ugonjwa wake wa ngozi na kumpatia matibabu sahihi.
Kufuatia ushauri wa daktari, Samia aliagiza mtoto huyo asafirishwe haraka kutoka Nyakanazi hadi hospitali ya Taifa ya Rufaa ya Muhimbili iliyopo Dar es Salaam kwa uchunguzi na matibabu.
Siku chache baada ya maagizo ya Rais, Hamimu akaanza kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Muhimbili tarehe 21 Oktoba, 2022.
Hamimu alilazwa Muhimbili kwa matibabu kwa muda wa miezi sita kwa msaada wa Rais Samia.
Ilipofika tarehe 19 Aprili 2023, madaktari wake wakajiridhisha kuwa sasa mtoto huyo amepona na anaweza kurudi nyumbani kwao mkoani Kagera.
Kabla ya kurudi kwao Kagera, Hamimu ameomba aonane na Rais Samia kumpa shukrani zake uso kwa uso.
"Rais (Samia) natamani nimuone kwa macho, yeye analinganaje. Yaani naomba kabisa, mnisaidie nimuone. Kwa sababu jinsi maisha yetu yalivyo, mimi sidhani kama ningefika huku," alisema Hamimu.
"Sidhani kama ningepona. Ilifika hatua nikasema, mniache nife. Kwa jinsi nilivyohangaika kupona ilishashindikana. Isingekuwa yeye (Rais Samia) mimi mpaka muda huu sidhani kama ningekuwa hai."
Hamimu anasema kuwa baada ya wazazi wake kuhangaika kumtibu kwa waganga bila mafanikio, walimwambia kuwa wamefikia mwisho hawawezi kumsaidia tena, ndipo alipoamua kuufuata msafara wa Rais Samia kuokoa maisha yake.
Mtoto huyo amewashukuru pia kwa dhati madaktari na manesi wa Muhimbili kwa kumhudumia kwa upendo hadi alipopona.
0 Comments