KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Khamis Mbeto Khamis(kushoto),akibadilishana mawazo na kada wa zamani wa CCM toka enzi za ASP, Ali Salum Ali(kulia) alipomtembea hapo nyumbani kwake Mtoni Wilaya ya Dimani kichama Zanzibar leo tarehe 12/04/2023.
**********************
NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) kimesema kitaendelea kufanya ziara mbalimbali za kujiimarisha kisiasa na kijamii ili kubaini na kuibua changamoto zinazowakabili wananchi.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Khamis Mbeto Khamis,katika mwendelezo wa ziara zake za kuwafariji wazee wa Chama Cha Mapinduzi katika Wilaya ya Mfenesini Kichama.
Katibu huyo Mbeto, akizungumzia lengo la ziara hiyo kuwa ni kuwafariji na kuwapatia futari wazee wa CCM na wagonjwa wa muda mrefu ikiwa ni sehemu ya kuendeleza utamaduni wa waasisi wa Chama cha ASP nchini.
Alisema ziara za kuwafuata wananchi katika maeneo wanayoishi zinaongeza ufanisi wa kiutendaji kutokana na kubaini changamoto zinazoikabili jamii kwa muda mrefu na kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu.
Katibu Mbeto,alieleza kuwa wazee wa CCM hususani waliostaafu katika utumishi wa umma na binafsi,wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazotakiwa kutafutiwa ufumbuzi wa haraka na viongozi wa kuanzia ngazi za matawi,shehia hadi mikoa kabla hazijafika ngazi ya Taifa.
Katika maelezo yake Mbeto, alisema viongozi na watendaji wa ngazi mbalimbali za chama na serikali wanatakiwa kubadilika kiutendaji kwa kuhakikisha wanatoa kipaumbele katika kutatua changamoto za kundi la wazee ili waishi kwa amani na furaha.
Pamoja na hayo alisema Chama Cha Mapinduzi kinasimamia kwa vitendo maelekezo yote ya kulinda maslahi ya wazee yaliyotajwa katika Katiba na Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025.
“Kila mwana CCM anatakiwa kuhakikisha wazee wetu hawa wanakuwa na usalama,upendo,amani na utulivu wa kudumu kwani waitoa mbali nchi toka katika mikono ya tawala za kikoloni, hivyo nasi tutekeleze wajibu wetu kwa kuwasaidia mahitaji yao ya kila siku”, alieleza Mbeto.
Naye Mwenyekiti wa CCM Jimbo la Mfenesini Kesi Mashaka Ngusa, alimshukru Katibu huyo Mbeto, kwa maamuzi ya kufanya ziara ya kuimarisha uhai wa Chama kwa upande wa kukagu hali za wazee.
Pamoja na hayo amewatembelea wazee wa wilaya ya mfenesini wakiwemo Bi.Saida Mapacho Ameir,Bi.Mwanakombo Vuai Haji,Ndg.Ali Salum Ali na Bi.Kifenesi Juma Mbarouk ambao wote ni makada wa zamani wa CCM.
Katibu huyo ametoa futari mbalimbali zikiwemo mchele,mafuta ya kula,sukari,tambi na unga wa ngano.
0 Comments