Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2023 Kitaifa Abdallah Shaib akizindua mradi wa Maji baada ya Mwenge wa Uhuru kukagua na kupitia nyaraka za mradi huo wenye thamani ya shilingi milioni 800.5.
Meneja wa RUWASA Wilaya ya Mtwara Mhandisi Hamisi Mashindike akitoa maelezo ya Ujenzi wa Mradi Kwa timu ya Wakimbiza Mwenge wa Uhuru 2023 kitaifa.
KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2023 Abdallah Shaib amewapongeza Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Mtwara kwa usimamizi bora wa ujenzi wa mradi wa maji wilayani humo.
Shaib ametoa pongezi hizo baada ya Mwenge wa Uhuru kutembelea, kukagua na kuzindua mradi huo wenye thamani ya shilingi million 800.5 katika kijiji cha Mwindi Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara mkoani Mtwara.
"Ninampongeza sana Meneja, na Mamlaka yote kwa usimamizi mzuri, mmejitahidi sana katika ujenzi wa mradi huu, tumeona kazi kubwa na nzuri mmefanya,". Amesema.
Kiongozi huyo amesema Mwenge wa Uhuru umekagua nyaraka zote za maelezo ya mradi na kujiridhisha kuwa yanaendana na uhalisia wa mradi kuanzia kwenye thamani ya mradi, miundombinu kulinganisha na fedha iloyotolewa.
"Tumekagua mradi kuangalia miundombinu na maelezo yaliyotolewa kwenye nyaraka kama yanaendana, tumejiridhisha," amesema.
Awali akitoa maelezo kuhusu ujenzi wa mradi huo, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Mtwara Mhandisi Hamisi Mashindike amesema mradi umekamilika na sasa unatoa huduma ya Maji safi na salama kwa wananchi 3465 katika vijiji vya Mwindi na Mbawala Halmashauri hiyo ya Mtwara.
Serikali ilianzisha mradi huu kwa lengo la kusongeza na kuongeza kiwango cha huduma ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wake katika Halmashauri hiyo.
Amesema serikali kupitia wizara ya Maji chini ya Mpango wa kupambana na UVIKO-19 na ustawi wa Jamii ilitoa fedha hizo (Zaidi ya milioni 800) Kwa ajili ya kujenga mradi huo.
Ujenzi wa mradi ulianza tarehe 19 Januari 2022 na kukamilika tarehe 25 Machi 2023 chini ya Usimamizi wa RUWASA. Ujenzi ulihusisha ujenzi matenki mawili yenye ujazo wa Lita 100,000 kwa kila moja.
Kwa sasa upatikanaji wa maji katika Wilaya ya Mtwara umefikia asilimia 57.6. Ilani ya CCM ya mwaka 2020 inaelekeza serikali kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya maji kwa asilimia 85 Vijijini na asilimi 95 mijini ifikapo mwaka 2025.
0 Comments