NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa imeielekeza Serikali kuchukua hatua thabiti kwa wahusika wote waliobainika kuhusika katika ukiukaji wa sheria na kusababisha ubadhirifu wa mali na rasilimali za nchi.
Ameyasema hayo leo Aprili 1,2023 Jijini Dar es Salaam, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa -Itikadi na Uenezi Mhe.Sophia Mjema mara baada ya Kamati kukutana katika kikao chake cha kawaida leo chini ya Mwenyekiti wa CCM, ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. SAMIA SULUHU HASSAN.
Amesema Kamati imetoa maelekezo kwa Serikali kuwafuatilia watu wote wanaotumia dhamana za uongozi vibaya na kushindwa kuweka maslahi ya nchi na uzalendo mbele katika nafasi walizoaminiwa kutumikia watu, badala yake wanaweka maslahi binafsi.
Aidha amesema Kamati Kuu imepokea na kujadili kwa kina masuala mbalimbali ya kitaifa, ikiwemo Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taarifa ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kwa mwaka wa fedha 2021/22, zilizowasilishwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan, hivi karibuni.
Mhe.Mjema amesema katika taarifa zote mbili ilibainika kuwepo kwa maeneo ambayo taarifa zote mbili zimeonesha kuwa Serikali imeboresha na kuendelea kuimarisha kasi ya utoaji wa huduma kwa wananchi, ikiwemo udhibiti na umakini katika matumizi ya fedha za umma, ambapo katika taasisi zilizokaguliwa, asilimia 96 zimepata hati safi.
"Katika mjadala huo wa kina, Kamati imesikitishwa na kuwepo baadhi ya maeneo mengine ambayo bado yanatakiwa kufanyiwa kazi ili kuondoa mapungufu/udhaifu uliobainishwa, ikiwa ni pamoja na mifumo ya malipo na ukusanyaji wa mapato kutokusomana, kuwepo kwa baadhi ya watumishi wa umma wasiokuwa waadilifu". Amesema
Hata hivyo amesema Kamati imeipongeza Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kwa kufanya kazi zao kwa weledi na kuendelea kutimiza wajibu wao kwa taifa, kwa kuonesha maeneo ambayo Serikali imeyaboresha na kubainisha madhaifu yanayohitaji kufanyiwa kazi, kwa lengo la kulinda mali, rasilimali kwa maslahi ya taifa.
Hata hivyo amesema Kamati Kuu, imeipongeza Serikali kwa kuratibu na kufanikisha vema ziara ya Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Harris Kamala aliyetembelea nchi yetu kwa siku tatu.
"Ziara hiyo imeongeza uimara wa ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani na kufungua milango zaidi ya mahusiano yenye faida kwa maendeleo na ustawi kwa pande zote mbili, hususan katika maeneo ya teknolojia ya habari na mawasiliano, kukabiliana na magonjwa, uchumi, uwekezaji na ajira". Ameeleza
0 Comments