Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge na Naibu Mtendaji Mkuu Hospitali ya King Faisal ya nchini Rwanda Frederic Ngirabacu wakisaini mkataba wa ushirikiano wa miaka mitatu wa kutibu wagonjwa wa moyo na kuwajengea uwezo wataalamu wa afya wa hospitali hiyo wa jinsi ya kuwatibu wagonjwa wa moyo. Mkataba huo umesainiwa leo jijini Dar es Salaam na kushuhudiwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge na Naibu Mtendaji Mkuu Hospitali ya King Faisal ya nchini Rwanda Frederic Ngirabacu wakionesha mkataba wa kutibu wagonjwa wa moyo na kuwajengea uwezo wa kuwatibu wagonjwa wa moyo wataalamu wa afya wa Hospitali hiyo. Mkataba huo umesainiwa leo jijini Dar es Salaam na kushuhudiwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe akizungumza namna ambavyo Tanzania imepiga hatua katika kutoa huduma za matibabu ya moyo wakati Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ilipokuwa ikisaini mkataba wa kutibu wagonjwa wa moyo pamoja na kuwafundisha wataalamu wa afya wa Hospitali za Taifa za moyo za nchini Rwanda na Zambia leo jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. William Mahalu akizungumza wakati Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ikisaini mkataba wa kutibu wagonjwa wa moyo na kuwajengea uwezo wa jinsi ya kuwatibu wagonjwa wa moyo wataalamu wa Hospitali za Taifa za moyo za nchini Rwanda na Zambia leo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akielezea namna ambavyo taasisi hiyo inapokea wagonjwa kutoka nchi mbalimbali za Afrika kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali wakati JKCI ilipokuwa ikisaini mkataba wa kutibu wagonjwa wa moyo na kuwajengea uwezo wa jinsi ya kuwatibu wagonjwa wa moyo wataalamu wa afya wa Hospitali za Taifa za moyo za nchini Rwanda na Zambia leo jijini Dar es Salaam.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Hospitali ya King Faisal ya nchini Rwanda, Hospitali ya Taifa ya Moyo ya nchini Zambia na Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart – SACH) la nchini Israel mara baada ya JKCI kusaini mkataba na nchi za Zambia na Rwanda wa kuwatibu wagonjwa wa moyo pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wa afya wa hospitali hizo.
Picha na JKCI
*********************
Na Salome Majaliwa – Dar es Salaam
20/04/2023 Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imesaini mikataba ya miaka mitatu ya makubaliano na Hospitali za Taifa za nchini Rwanda na Zambia kutibu wagonjwa wa moyo pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wa afya wa hospitali hizo wa jinsi ya kuwatibu wagonjwa wa moyo.
Mikataba hiyo imesainiwa leo katika Ukumbi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt. Peter Kisenge pamoja na Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya Moyo ya nchini Zambia Dkt. Shumba Chabwela na Naibu Mtendaji Mkuu wa Hospitali ya King Faisal ya nchini Rwanda Frederic Ngirabacu.
Akishuhudia utiaji wa saini wa mikataba hiyo Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe alisema JKCI inaaminika ndani na nje ya nchi kwa kutoa huduma bobezi za magonjwa ya moyo kutokana na Serikali kuwekeza vifaa tiba vya kisasa vya kutibu magonjwa ya moyo pamoja na kuwasomesha wataalamu wa afya waliopo katika Taasisi hiyo.
“Kitendo cha kutia saini katika mikataba ya kutibu wagonjwa wa moyo kutoka nchi za Rwanda na Zambia kunatekeleza dhana ya utalii tiba kama ambavyo Rais wa Serikali ya awamu ya sita Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hasan anavyosisitiza umuhimu wa utalii tiba hapa nchini”, alisema Dkt. Grace.
Dkt. Grace alisema kupitia wagonjwa watakaotoka nchini Rwanda na Zambia uchumi wa nchi utaongezeka si kwa ajili ya matibabu peke yake bali pia wagonjwa wanaweza kutumia fursa ya matibabu kuona vivutio mbalimbali vilivyopo Tanzania hivyo kuleta maendeleo katika sekta nyingine.
“JKCI inaenda kuifungua nchi na kuendeleza utalii tiba kwani kupitia wagonjwa kutoka nchi mbalimbali za Afrika wanaofika JKCI kwa ajili ya matibabu wanaweza kutembelea sehemu mbalimbali ikiwemo mbuga za wanyama na mapolomoko ya maji hii itawezesha nchi kuendelea kiuchumi”, alisema Dkt. Grace.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema makubaliano maalum waliyosaini na nchi za Rwanda na Zambia kutasaidia nchi hizo kutoa huduma za upasuaji wa moyo kwa wagonjwa wanaowahudumia.
Dkt. Kisenge ambaye pia ni Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alisema Taasisi hiyo iliyoanza wakati wa Serikali ya awamu ya nne imekuwa ikikuwa kwa kasi kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali za awamu ya nne, tano na sita hivyo kuifanya kuwa moja ya Taasisi kubwa zinazotoa matibabu ya moyo Afrika.
“Kupitia mafanikio hayo wenzetu wa Zambia na Rwanda wameona ni muhimu kushirikiana nasi ili kwa pamoja tuweze kuwasaidia wagonjwa wa moyo waliopo katika nchi hizo kwani wanatuhitaji”, alisema Dkt. Kisenge.
Naye mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. William Mahalu alisema utendaji kazi wa JKCI unaonekana hivyo ni imani yake kuwa kwa kusaini mkataba na nchi hizo mbili kutatoa motisha kwa nchi nyingine za Afrika kuona umuhimu wa kushirikiana na KCI.
“Juhudi na maendeleo ya JKCI yamesikika ndani na nje ya nchi ndio maana leo hii mikataba miwili imesainiwa hivyo kinachofuata sasa ni utekelezaji wa mikataba hiyo kwa pande zote mbili ili kupata maendeleo na kutambulisha huduma zetu duniani”, alisema Prof. Mahalu.
0 Comments