Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa ( kulia ) akiteta jambo na katibu Mtendaji Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) Dkt. Godwill Wanga (kushoto) wakati wa Mkutano wa majadiliano ya kisekta kati ya wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na Wadau wa Sekta Binafsi uliofanyika jana Jijini Dar es salaam lengo ikiwa ni kujadili changamoto zinazokumba sekta hiyo na kuibua fursa zitakazo leta tija kwa Taifa. katikati ni Mwenyekiti wa Sekta Binafsi nchini, (TPSF) Bi. Angelina Ngalula.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa ( kulia ) akizungumza na wadau wa sekta ya uchukuzi wakati wa Mkutano wa majadiliano ya kisekta kati ya wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na Wadau wa Sekta Binafsi uliofanyika jana Jijini Dar es salaam lengo ikiwa ni kujadili changamoto zinazokumba sekta hiyo na kuibua fursa zitakazo leta tija kwa Taifa. Kushoto ni katibu Mtendaji Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) Dkt. Godwill Wanga wapili kushoto ni Mwenyekiti wa Sekta Binafsi nchini, (TPSF) Bi. Angelina Ngalula na wapili kulia ni Katibu mkuu Bw. Gabriel Migire na kulia ni Naibu katibu mkuu wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Dkt. Ally Possi.
**********************
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
Serikali imeihakikishia sekta binafsi kuwa itazifanyia kazi kwa umakini mkubwa changamoto zote zinazokwamisha ustawi wa maendeleo ya sekta ya uchukuzi hapa nchini.
Akizungumza katika mkutano wa majadiliano ya kisekta ya wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na wadau wa sekta binafsi Jijini Dar Salaam jana,Waziri wa ujenzi na uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amewaambia wadau hao kuwa wizara yake itashughulikia changamoto na kuahidi kuzifanyia kwa wakati.
“Serikali itaendelea kuboresha mazingira mazuri ya kufanya biashara kwa sekta ya usafirishaji na usafiri sambamba na kuzifanyia kazi sheria na kanuni mbalimbali ambazo hazikidhi matarajio ya ukuaji wa sekta hiyo” Prof. Mbarawa.
Katika mkutano huo ulioratibiwa na Baraza la Taifa la Biashara kwa maagizo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Prof. Mbarawa alisema kuhusu suala la udhibiti mwendo (VTS) aliahidi kulifanyia kazi kwa kumuelekeza LATRA kulifanyia kazi kwa kushirikiana na TBS haraka.
Prof. Mbarawa aliwaambia wadau kuwa Serikali ya awamu ya sita itaendelea kuimarisha miundombinu ikiwemo ujenzi wa njia nne kutoka Bandari ya Dar es Salaam, Morogoro Road, Mbeya hadi Tunduma.
Naye Katibu Mtendaji wa TNBC, Dkt. Goodluck Wanga aliwapongeza wadau kuwa wazi na kueleza changamoto wanazokabiliwa nazo.
“Mikutano hii ya kisekta ni muhimu sana kwani inasaidia serikali kutafuta suluhisho la kudumu kwa changamoto ,vilevile kuimarisha mazingira ya kufanya biashara.
Dkt. Wanga amesema Baraza ambalo Rais ndiyo Mwenyekiti wake litaendelea kuratibu mikutano ya kisekta kwani inatoa nafasi kubwa ushiriki wa wadau mbalimbali katika sekta.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa sekta binafsi nchini (TPSF), Bi Angelina Ngalula mbali ya kuishukuru serikali alisema sekta ya uchukuzi inasaidia kupunguza gharama ya bidhaa zinazozalishwa hapa nchini.
“Naiomba serikali iendelee kuboresha miundombinu ikiwemo reli na barabara kwani itasaidia sana kupunguza gharama”, alisema.
Bi. Ngalula sekta ya usafiri na usafirishaji ni nguzo muhimu sana katika kukuza na kujenga uchumi imara sambamba na kupunguza gharama ya bei za bidhaa.
“Wakati serikali inapitia sera na sheria za usafiri na usafirishaji ni lazima kuangalia ushindani sokoni”, alisema.
Alisema ukuaji wa sekta ya uchukuzi, itasaidia katika kupunguza gharama za bidhaa zinazozalishwa nchini hasa za kilimo, utakuta bidhaa kutoka China inauzwa gharama kuliko inayozalishwa hapa nchini, hii ni kutokana na gharama kubwa katika usafirishaji.
“Nchi yetu ni ya kimkakati na ina fursa nyingi sana, katika sekta hii tutambue sisi ni wanachama wa SADC, kwa hiyo tunapojadili Sera, mikakati na mambo madhubuti ya nchi, lazima tutunge Sera zinazoendana na ushindani wa soko, zikiwa ni Sera tofauti sisi ndio tutakaopoteza zaidi,” alisema Bi. Angelina.
0 Comments