Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Mhe. Said Mkumba (katikati) akikata utepe ishara ya kuzindua rasmi Benki ya CRDB Tawi la Bukombe Mkoani Geita
Na Mwandishi Wetu - Malunde 1 blog
Benki ya CRDB imefungua Rasmi tawi jipya Wilayani Bukombe mkoani Geita ambapo wananchi na wadau wote wa maendeleo wameombwa kuchangamkia fursa za maendeleo zinazotolewa na Benki ya CRDB na kwa kuzingatia kuwa mkoa wa Geita unasifika kwa uchimbaji wa madini Benki ya CRDB imeahidi kuendelea kujikita zaidi katika kutoa mikopo kwa wachimbaji kuwawezesha kununua vifaa na mitambo bora ya kufanikisha shughuli zao.
Sherehe za ufunguzi rasmi wa Tawi la Benki ya CRDB Bukombe zimefanyika leo Alhamisi Aprili 20,2023 ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Mhe. Said Mkumba.
Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Mhe. Said Mkumba amewasihi wananchi na wadau wote wa maendeleo kuchangamkia fursa za maendeleo zinazotolewa na Benki ya CRDB ikiwemo usalama wa fedha za wateja, urahisi wa upatikanaji wa mikopo kwa ajili ya biashara na malengo binafsi na urahisi wa kufanya malipo kupitia mifumo ya kidijitali.
“Nitoe rai kwa Wananchi wote wa hapa Bukombe na maeneo ya jirani kuchangamkia fursa hizi zinazotolewa na Benki ya CRDB, ikwamo kujitokeza kwa wingi kufungua akaunti. Vilevile, nitumie fursa hii kuwahakikishia wananchi na taasisi zote za umma, pamoja na Serikali, kwamba Benki ya CRDB ni mdau mkubwa wa Serikali yetu na tuendelee kushirikiana nao kwenye biashara zetu”,amesema.
“Ni furaha kubwa kwetu sisi wana Bukombe kuona Benki yetu ya kizalendo ya CRDB ikiishi kwa vitendo kaulimbiu yake isemayo “Benki inayomsikiliza Mteja” kwa kuyafanyia kazi mahitaji halisi ya wateja wake kwa kuendelea kusogeza huduma zake karibu zaidi na wateja na Watanzania kwa ujumla. Napongeza sana juhudi hizi kwani hii ni ishara tosha kuwa Benki ya CRDB imejipanga vilivyo katika kuunga mkono jitihada za Serikali katika kufanikisha mipango yake ya kujumuisha Watanzania wengi zaidi katika mfumo rasmi wa fedha yaani “financial inclusion”, amesema Mkumba.
“Benki ndicho chombo kikuu cha kutolea huduma za kifedha kwa wananchi. Benki zinatakiwa zizingatie mahitaji ya wananchi na ziweze kuwahamasisha wananchi kutambua umuhimu wa kutumia huduma za benki kwa maendeleo Binafsi na ya taifa letu kwa ujumla wake. Kipekee kabisa niipongeze sana Benki ya CRDB kwa kuwa mstari wa mbele katika kufanikisha hili, ni dhahiri kuwa mmekuwa mkiishi kaulimbiu yenu ya “Ulipo Tupo” kwa vitendo kupitia mkakati madhubuti wa kusogeza na kuongeza wigo wa huduma kwa wananchi, na leo hii mmedhihirisha hapa kwetu Bukombe”,amesema Mkuu huyo wa wilaya
Aidha ametoa wito kwa Watanzania wote kujenga mazoea ya kuweka akiba zao benki na kutumia benki kwa shughuli zao halali za kifedha na kwa wale ambao wana mpango wa kukopa, iwe mikopo binafsi au ya biashara watambue kuwa kurejesha kwao mikopo ndio kunaleta uendelevu wa Benki.
Ameipongeza Benki ya CRDB kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya ya kufikisha huduma za kibenki kwa wananchi na kusisitiza kuwa Serikali ipo nanyi bega kwa bega na benki hiyo katika kazi ya kuijenga nchi ya Tanzania.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Mikopo wa Benki ya CRDB, Xavery Makwi amesema kwa upande wa Mkoa wa Geita, Benki ya CRDB ina jumla ya matawi nane ambayo ni Mbogwe, Runzewe, Katoro, Chato, Geita, Geita Gold, Nyang'wale na tawi jipya la Bukombe hapo Ushirombo.
“Benki ya CRDB pia imekuwa ikitoa huduma kupitia CRDB Wakala, na wilayani Bukombe tunao jumla ya CRDB Wakala 32. Mawakala hawa hutoa huduma zao “in real time,” nikimaanisha kuwa miamala hufanyika moja kwa moja katika akaunti za wateja wetu ndani ya wakati husika. Kupitia CRDB Wakala, wateja wanapata huduma karibu zote kama ilivyo katika matawi ya Benki yetu. Niwaombe wananchi mjitokeze kwa wingi kupata huduma katika Benki ahadi yetu ni “Tupo Tayari” kuwahudumia”,amesema.
“Kwa kuzingatia kuwa mkoa huu wa Geita unasifika kwa uchimbaji wa madini, Benki ya CRDB pia imejikita zaidi katika kutoa mikopo kwa wachimbaji kuwawezesha kununua vifaa na mitambo bora ya kufanikisha shughuli zao. Tayari vikundi 12 vya wachimbaji wadogo vimefungua akaunti kwenye Benki yetu pamoja na wachimbaji binafsi zaidi ya 250. Tangu mwaka 2021 mpaka sasa tumekopesha zaidi ya Shilingi Bilioni 70 kwa wachimbaji wa mkoa mzima wa Geita. Licha ya mikopo, Benki pia hutoa dhamana za biashara (business guarantees) pamoja na barua za mikopo yaani “letter of credit” ambazo ni mahsusi kwa ajili ya kuwezesha biashara za usanifu (mali kauli) na zile za kimataifa”, amesema Makwi.
Ameeleza kuwa kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wateja na mahitaji, Benki ya CRDB imeona kuna umuhimu wa kuboresha huduma ili kuendana na mahitaji yaliyopo na ya baadaye.
“Hivyo basi, baada ya kufanya utafiti wa kina, Benki ya CRDB iliamua kujenga tawi litakalowahudumia wana Bukombe wa hapa mjini na maeneo ya jirani. Tawi hili jipya lina nafasi ya kutosha kuhudumia wateja wengi na litatoa huduma za kisasa zaidi. Pamoja na uhakika na usalama wa huduma watakaoupata wateja wetu kupitia tawi hili, Benki pia imejipanga kikamilifu kuhakikisha wanapata huduma zote za kibenki ikiwamo utunzaji wa amana kupitia akaunti”,ameongeza Makwi.
“Benki yetu ya CRDB ina akaunti zinazokidhi mahitaji ya makundi yote ya wananchi ikiwamo; Akaunti ya Akiba, Akaunti ya hundi kwa ajili ya biashara, Malkia kwa ajili ya Wanawake, Scholar kwa ajili ya Wanafunzi, Junior Jumbo kwa ajili ya Watoto, Akaunti ya Pensheni kwa ajili ya Wastaafu, Niamoja kwa ajili ya Vikundi, Akaunti za Uwekezaji za Muda Maalum, pamoja na Fahari Kilimo maalum kwa ajili ya Wakulima",amesema.
"Aidha, pindi mteja anapofungua akaunti anaunganishwa na mifumo SimBanking, Internet Banking, pamoja na TemboCard Visa/MasterCard/UnionPay. Mifumo hii inasaidia kurahisisha upatikanaji wa huduma popote walipo. Akaunti hizi zote pia zinaweza kufunguliwa kupitia dirisha letu la “CRDB Al Barakah Banking” kwa wateja ambao wangependa kupata huduma zinazofuata misingi ya sharia ya dini ya kiislam, ikiwamo akaunti ya Fahari Kilimo kwa ajili ya wakulima”,amesema Makwi.
Ameeleza kuwa Benki ya CRDB ni benki kubwa na ya kizalendo inayoongoza kwa wingi wa amana za wateja, rasilimali na utoaji mikopo nchini ambapo katika kipindi cha miaka 27 sasa tangu kuanzishwa kwake, Benki ya CRDB imekua na kutanua mtandao wake wa huduma kutoka matawi 19 yaliyokuwepo mpaka zaidi ya matawi 250 kote nchini, na kampuni tanzu nchini Burundi, na hivi karibuni inatarajia kuingia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Hata hivyo Makwi amesema licha ya idadi kubwa ya matawi yanayopatikana nchi nzima, Benki ya CRDB pia imekuwa ikibuni na kuingiza sokoni mifumo na njia mbadala zinazorahisisha huduma kwa Watanzania.
Ameongeza kuwa ndani ya kipindi cha uhai wa Benki mambo kadhaa yamefanyika mfano tuna CRDB Wakala zaidi ya 25,000 nchi nzima, Mashine za kutolea fedha (ATMs) zaidi ya 550, Matawi yanayotembea (Mobile branches) 21, Mashine za manunuzi (POS) zaidi ya 6,000, Pamoja na mifumo ya kidijitali ya utoaji huduma ikiwamo; “SimBanking”, “SimAccount”, na “Internet banking”ambayo inatoa fursa kwa wateja kupata huduma popote pale walipo ndani na nje ya nchi. Hii ndio maana wanasema “Ulipo Tupo”.
Amefafanua kuwa akaunti ya “Fahari Kilimo” ni mwendelezo wa juhudi za Benki kuisaida serikali kuhakikisha wakulima wanatengenezewa mfumo madhubuti wa kupokea malipo yao huku akiongeza kuwa benki hiyo inatoa mikopo mingi ikiwamo ya uwekezaji na uendeshaji wa biashara, mikopo binafsi kwa ajili ya wafanyakazi wa sekta ya umma na binafsi, mikopo kwa wajasiriamali, mikopo ya vikundi, wanafunzi na wastaafu.
“Tumekuwa tukitoa mikopo ya pembejeo na zana za kilimo kwa wakulima wa mazao ya kimkakati ili kuweza kukuza uzalishaji hapa nchini. Kwa mwaka wa fedha wa 2021/22 Benki ya CRDB ilikopesha jumla ya TZS. 769 Bilioni kwa wakulima binafsi, vikundi pamoja na vyama vya Ushirika ambayo ni sawa na asilimia 43 ya mikopo yote ya kilimo iliyotolewa nchini”,ameeleza.
Akitoa salamu za ufunguzi Kaimu Meneja wa Kanda ya Magharibi ndg Jumanne Wambura Wagana amesema Benki ya CRDB ilianza kutoa huduma zake mwaka 2015 ikiwa ndani ya jengo la Halmashauri ya Bukombe lakini baada ya kupokelewa vizuri na wafanyabiashara , watumishi na wadau mbalimbali wilayani Bukombe imelazimika kuhamishia shughuli zake kwenye tawi kubwa na la kisasa zaidi.
Pia amesisitiza wafanya biashara kuchangamkia fursa ikiwemo mikopo ya kilimo ya yenye riba ya 9%, Mikopo kwa watumishi yenye riba ya 13% huku ikitolewa kwa hadi miaka 9. Vile vile huduma ya Mikopo kwa wadau wa madini bila kusahau Huduma za Al Barakah kwa wadau wenye imani ya kiislamu.
0 Comments