Na. Mwandishi wetu
Wafanyakazi wanawake wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), wametembelea gereza la Segerea, jijini Dar es Salaam, kutoa msaada wa taulo za kike (pads) kwa wanawake wafungwa na mahabusu katika gereza hilo ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yanatakayofikia kilele chake tarehe 8 Machi.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo tarehe 6 Machi, 2023, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake NACTVET, Bi. Deborah Ngalemwa, amesema wanawake hao wameguswa kuwakumbuka wanawake wenzao wenye uhitaji kwa kutoa msaada. “Tunaamini kabisa kuwa wanawake wafungwa na mahabusu wa gereza hili ni binadamu ambao mifumo ya miili yao ni ya kawaida na wana haki ya kujihifadhi katika mazingira safi kimwili, hivyo tukaona kwa mwaka huu tuanze nao, lakini pia tuwe sehemu ya hamasa kwa watu wengine kusaidia makundi yenye uhitaji,” amesema Ngalemwa.
Aidha, Bi. Deborah ametoa wito kwa wanawake na watu mbalimbali kwenye jamii kuweka utaratibu wa kutenga kiasi kwenye kile wanachopata ili kusaidia jamii inayowazunguka hususan watu kwenye makundi mahsusi kama yatima, wajane na watoto wa mtaani, ili nao wajione wanathaminiwa kama watu wengine. Amewaomba wanawake walio gerezani watambue kwamba mahali walipo ni sehemu ya mafunzo ya muda ya kuboresha shughuli zao za kila siku.
Kwa upande wa uongozi wa gereza wametoa shukrani na pongezi kwa wanawake wa NACTVET kwa msaada huo kwani uhitaji ni mkubwa na kuwataka waendelee kusaidia makundi mengine yenye uhitaji bila kuwasahau Wafungwa wanaume ambao wamekuwa wanakumbukwa mara chache sana..
0 Comments