Ticker

6/recent/ticker-posts

TTCL YATAKIWA KUTENGENEZA DASHIBODI YA KUFATILIA VITUO VYA MKONGO


Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye akizungumza wakati alipofanya ziara ya kukagua miundombinu katika Kituo cha Mkongo na hali ya huduma za Mawasiliano kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika Kituo cha Kutoa Huduma kwa Pamoja Mpakani (OSBP) cha Namanga kilichopo mkoani Arusha.Machi 5,2023.



Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Arusha

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye amelielekeza Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kushirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kuharakisha utengenezaji wa mfumo wa ufuatiliaji na usimamizi (Dashibodi) wa vituo vyote vinavyotoa huduma za Mkongo nchini.

Maelekezo hayo ameyatoa katika mpaka wa Namanga-Arusha Machi 5, 2023 alipozuru kukagua miundombinu katika kituo cha Mkongo kilichopo katika mpaka huo na hali ya huduma za Mawasiliano kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika Kituo cha Kutoa Huduma kwa Pamoja Mpakani (OSBP) cha Namanga.

"Kumekuwa na malalamiko ya kukosekana kwa huduma za mkongo au kasi ndogo ya mtandao katika baadhi ya maeneo, hivyo kukamilika kwa dashibodi hiyo kutawezesha TTCL kuona na kufatilia vituo vyote nchi nzima ", amesema Waziri Nape.

Ameongeza kuwa, "Tunataka mifumo ya TEHAMA ilete matokeo yaliyokusudiwa, uwepo wa dashibodi utasaidia kufatilia vituo vya Mkongo na kufahamu wapi kuna shida na chanzo chake ni nini ili kushughulikia na kurudisha huduma kwa wakati ".

Amesema kuwa lengo la Serikali ni kuongeza usimamizi ili kuondoa usumbufu na malalamiko ya wateja wa huduma za Mkongo na kuongeza mapato kwa Serikali.

Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Mhandisi Peter Ulanga amesema Shirika la TTCL pamoja na kutoa huduma za Mkongo pia linawashauri wateja wake hasa pale wanapopokea malalamiko ya kasi ndogo ya mtandao ambapo mara nyingi inasababishwa na matumizi makubwa kuliko kiwango cha huduma (capacity) ambayo taasisi inanunua kutoka TTCL.

Amefafanua zaidi kwa kuelezea tatizo la mfumo wa ndani wa taasisi husika pamoja na sehemu wanayohifadhia taarifa za mfumo (server) kuwa na uwezo mdogo husababisha kasi ya mtandao kuwa ndogo hata kama huduma ya Mkongo inawafikia vizuri.

Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano umeunganishwa kwenda nchi jirani ya Kenya kupitia mpaka wa Namanga, Horohoro na Holili.

Taarifa hii imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.


Waziri Nape akikagua kituo hicho.
Ukaguzi wa kituo hicho ukiendelea.
Waziri Nape (wa pili kushoto) akipata maelezo wakati alipotembelea kituo hicho.
Majadiliano yakifanyika wakati wa ukaguzi wa kituo hicho.

Post a Comment

0 Comments