Ticker

6/recent/ticker-posts

TGNP YATUMIA MUZIKI WA KIRAGHBISHI KUPINGA VITENDO VYA UKATILI NCHINI


NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

LICHA ya kuhakikisha jamii inaelewa masuala ya jinsia kwa kufanya tafiti mbalimbali ambazo zimekuwa chachu ya elimu ya usawa wa kijinsia na kuondokana na masuala ya unyanyasaji wa kijinsia kwenye jamii zetu, TGNP imekuwa ikitumia mbinu mbalimbali kusambaza matokeo ya tafiti hizo, njia mojawapo ikiwa ni matumizi ya sanaa ya muziki.

TGNP imeona umuhimu wa kutumia muziki wa kiraghbishi ambao wasanii wanapitishwa katika mafunzo maalumu ya kiraghbishi ili kutengeneza tungo na miziki yenye maudhui ya kiraghbishi kwa lengo la kubadili mitizamo ya jamiii na kuleta maendeleo kwenye masuala ya kijinsia.

Hivi karibuni TGNP imewatumia wasanii chipukizi wahudhuriaji wa semina za Jinsia na Maendeleo, maarufu kama GDSS ambao walishiriki mafunzo na baadae walipewa kazi ya kutunga na kuweka sauti, kazi ambayo ilichuja washiriki hao na kupata washiriki watatu waliowezeshwa na TGNP kurekodi nyimbo hizo.

Akizungumza kuhusiana na mchakato huo, Afisa habari wa TGNP Bi. Monica John amesema miongoni mwa wasanii waliopitishwa ni pamoja na Anastazia Mgimba ambaye alikuja na wimbo wake uitwao 'Niache Niwahi' huku msanii mwingine akiwa ni Frank Charles na wimbo wake wa 'Kubwa Jinga'.

Aidha Bi.Monica amesema kupitia vilabu vya Jinsia Mashuleni, TGNP waliwanoa watoto wenye kipaji cha uimbaji na kuwawezesha kurekodi wimbo wao unaoitaka jamii kuwalinda watoto dhidi ya ukatili wa kijinsia.

"Lengo hasa la kufanya hivi ni kuibua vipaji na kusaidia vipaji hivyo kubadili mitizamo ya jamii na kuleta mabadiliko chanya hasa kwenye masuala ya usawa wa kijinsia," amesema Bi. Monica.

Pamoja na hayo Bi.Monica amesema wanaamini ikiwa wasanii hao wataelewa na kuweza kuendelea kutunga nyimbo zenye kuelimisha na kuitaka jamii kubadilika, watachangia kwa kiasi kikubwa kuwezesha kufikia kufikia usawa na maendeleo jumuishi na endelevu.

Kwa upande wake msanii Frank Charles amesema kupitia mafunzo maalumu ya kiraghbishi wameweza kupata uelewa mkubwa wa kufanya utunzi wa nyimbo mbalimbali zinazohamasisha jamii kuachana na masuala ya ukatili na baadae jamii iweze kupata uelewa na matukio ya ukatili kuweza kupungua kwenye jamii zetu.

Amesema matukio ya ukatili mara nyingi yanatokea kwenye jamiizetu kutokana na masuala ya imani potofu, visasi, ulevi lakini kupitia wimbo wake wa 'Kubwa Jinga' utaenda kutoa elimu na jamii nzima ifahamu namna ambavyo tunaweza kuondokana na masuala ya ukatili kwenye jamii.

Hata hivyo ameiomba Serikali kupitia vyombo husika kuhakikisha inatekeleza sheria zilizopo kuhakikisha wale ambao wamekutwa na hatia ya kufanya ukatili wapewe adhabu stahiki ili iwe fundisho kwa wengine ambao wamekuwa wakifanya vitendo hivyo mara kwa mara.

Nae Msanii Anastazia Mgimba amesema kupitia wimbo wake wa 'Niache Niwahi' utaenda kutoa somo kwenye jamii kuhakikisha wanatoa taarifa sehemu husika pindi wanapoona ukatili wa kijinsia umefanyika ili tatizo liweze kutatuliwa na muhusika kufikishwa kwenye vyombo husika.

Amesema ili kuhakikisha masuala ya ukatili yanapungua na baadae kuisha kabisa nchini atahakikisha anaendelea kutoa nyimbo kama hizo na jamii iweze kubadilika na kuachana na masuala ya ukatili wa kijinsia.

Nyimbo za wasanii hawa pia unaweza kuzipata na kusikiliza kupitia link hizi hapa Youtube 👇👇

Post a Comment

0 Comments