Ticker

6/recent/ticker-posts

SERA NZURI ZA SAMIA KUHUSU UWEKEZAJI ZACHANGIA ONGEZEKO KUBWA LA WAAJIRI KUJISAJILI WCF-DKT. MDUMA

Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo jijini Dodoma Machi 2, 2023.

****************************

Na mwandishi wetu, Dodoma

KUMEKUWA na ongezeko kubwa la waajiri kujisajili na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya sita, Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma amesema.

Dkt. Mduma ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Idara ya Habari MAELEZO jijini Dodoma Machi 2, 2023 ambapo alidokeza kuwa katika kipindi cha kuanzia Mwezi Machi 2021 hadi Februari 2023 Waajiri wapya 5,250 wamejisajili WCF.

Alisema kwa taarifa zisizokaguliwa hadi kufikia Mwezi Februari 2023, WCF ilikuwa imesajili jumla ya waajiri 29,978,

Kati ya waajiri hao asilimia 99.27% ni waajiri wakubwa, huku asilimia 98.71% ni waajiri wa kati na waajiri wa chini ni asilimia 88.56%.

“Hatua za makusudi za Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wake Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, za kuweka vivutio vya kufanya biashara na kuondoa vikwazo vilivyokuwepo ikiwa ni pamoja na kupunguza viwango vya uchangiaji na kutoa msamaha wa riba vimechangia ongezeko hilo.” Alisisitiza Dkt. Mduma.

Alisema kwa sasa mwajiri amepunguziwa mzigo wa kuchangia kwenye Mfuko ambapo serikali ilipunguza kiwango cha mchango kwa Sekta Binafsi kutoka asilimia 1% ya hapo awali kabla ya maboresho ya kisera hadi asilimia 0.5% ya sasa na hivyo kuleta ulinganifu wa michango kuwa sawa na Sekta ya Umma.

“Niwahakikishie wafanyakazi kuwa mafao yanayotolewa na WCF yataendelea kutolewa kwa ubora ili kuendelea kuleta nafuu na faraja kubwa kwa wafanyakazi.” Alisema.

Lakini pia alisema Serikali iliendelea kuleta unafuu zaidi kwa waajiri kwa kupunguza kiwango cha kodi ya malimbikizo ya madeni ya michango ya nyuma kutoka asilimia kumi (10%) hadi asilimia mbili (2%).

“Hii yote inalenga kuhamasisha waajiri ambao hawajajisajili waweze kujisajili na watekeleze wajibu wao wa kulipa michango kwa ajili ya kulinda wafanyakazi wao dhidi ya majanga yatokanayo na kazi.” Aliongeza Dkt. Mduma.

ULIPAJI WA MAFAO

Kabla ya kuanzishwa kwa WCF, malipo ya fidia nchini kwa mwaka mzima yalikuwa chini ya shilingi milioni 200 lakini baada ya kuanzishwa kwa WCF malipo yanaongezeka mwaka hadi mwaka.

“Takwimu za hivi karibuni zinaonyesha toka kuanzishwa kwa Mfuko, idadi ya wanufaika wa Mfuko imefikia 10,454 ambao wamelipwa jumla ya shilingi Bilioni 49.44.

Akifafanua kuhusu Mafao, Mkurugenzi Mkuu alisema kuna Mafao ya aina mbalimbali ambayo Mfuko unatoa ikiwa ni pamoja na Huduma ya matibabu, Malipo ya ulemavu wa muda, Malipo ya ulemavu wa kudumu yanayotolewa kwa mfumo wa Pensheni ya kila mwezi, Malipo kwa anayemuhudumia mgonjwa (mfanyakazi), Huduma za utengamao, Msaada wa mazishi na Malipo kwa wategemezi endapo mfanyakazi atafariki.

FIDIA MTANDAONI

Kuhusu maboresho mbalimbali yaliyofanyika Dkt. Mduma alisema Mfuko umeendelea kusogeza huduma karibu na wadau wake na sasa huduma zote muhimu zinapatikana nchi nzima kwa njia ya mtandao.

Alizitaja huduma hizo kuwa ni pamoja na Usajili wa wanachama ambapo mwanachama wa Mfuko huu ni waajiri, kupata cheti cha Usajili, Kuwasilisha Michango ya kila mwezi, Mfuko unapokea michango kupitia Nambari ya Udhibiti (Control Number) ambayo hupatikana kwa njia ya mtandao.

Huduma zingine ni Kuwasilisha Taarifa za Michango, Kufanya mabadiliko ya taarifa za wafanyakazi wao, Kuwasilisha Taarifa ya Ajali, Ugonjwa au Kifo cha Mfanyakazi kilichotokana na kazi na Kufuatilia mwenendo wa madai.

Aidha Dkt. Mduma aliwakumbusha waajiri wote Tanzania Bara kuwa, Kwa mujibu wa sheria, Mwajiri ndiye mwenye jukumu la kuchangia kwenye Mfuko na ni kosa la jinai kwa mwajiri kumkata mshahara Mfanyakazi wake kwa ajili ya kuchangia WCF.

Pia alisisitiza kwamba kupungua kwa kiwango cha uchangiaji hakutaathiri utoaji wa Mafao kwani Mfuko umeshirikiana na wataalam wa uhimilivu na kujihakikishia kuwa WCF itabaki imara na kuwa endelevu.

UWEKEZJI

Kuhusu uwekezaji, Dkt. Mduma alisema Mfuko una jukumu la kuwekeza fedha za ziada (investable funds) kwa mujibu wa Sheria na Muongozo wa Uwekezaji kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii wa mwaka 2015 uliotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (The Social Security Schemes Investment Guidelines, 2015).

“Asilimia 89.76 ya uwekezaji wa Mfuko upo kwenye Hati Fungani za Serikali, lakini pia Mfuko umewekeza katika Kiwanda cha Chai Mponde kilichoko Wilayani Lushoto Mkoani Tanga.” Alibainisha

Aidha alisema hadi kufikia tarehe 30 Juni 2022, Mfuko umekusanya jumla ya Shilingi Bilioni 241.48 toka kwenye mapato yatokanayo na uwekezaji.

Post a Comment

0 Comments