Ticker

6/recent/ticker-posts

MRADI WA UFUGAJI NYUKI KUFAIDISHA VIJIJI VYA MWAMGONGO NA KIZIBA-KIGOMA


NA EDMUND SALAHO GOMBE, KIGOMA.

SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), kupitia idara ya Ujirani Mwema katika Hifadhi ya Taifa Gombe imekabidhi vifaa kwa ajili ya mradi wa ufugaji nyuki vyenye thamani ya shillingi millioni 31 kwa vikundi 3 (vikundi viwili kwa Kijiji cha Mwamgongo na kikundi kimoja katika Kijiji cha Kiziba) ambavyo vina jumla ya wanachama 73.

Awali, akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi,Yustin Richard Njamasi ambaye ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Gombe alisema

Mradi huu wa ufugaji nyuki ni mradi ulioibuliwa na wananchi wa vijiji viwili ambavyo ni Mwamgongo na Kiziba ukilenga utunzaji wa misitu ya Hifadhi ya kijijini inayopakana na Hifadhi ya Taifa Gombe pamoja na kuwapatia kipato wananchi. Mradi huu ulihusisha utoaji wa semina ya ufugaji nyuki kisasa,vifaa vya ufugaji na kununua mizinga (160), mashine(4) za kukamulia asali, malazi (16) ya ufugaji nyuki, pamoja na viti a moshi (4) kwa wanavikundi hao. 

Aidha, Kamishna Njamasi, alibainisha kuwa shughuli za ujirani mwema zimekuwa zikifanyika kwa miaka mingi tangu miaka ya tisini kwa ushirikiano mkubwa kati ya Hifadhi ya Taifa ya Gombe na vijiji jirani vinavyopakana moja kwa moja na Hifadhi pamoja na vile vinavyo changia Mfumo wa ikolojia moja na Hifadhi ya Taifa ya Gombe.

Akikabidhi mradi huo kwa wanakikundi hao, Mkuu wa Wilaya ya Kigoma ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo Mhe.Salum Abdallah Kalli, aliwaasa wananchi kushirikiana na Hifadhi katika kutunza rasilimali hizi kwa faida ya sasa na ya baadae

“Niwatake wananchi wote kushirikiana na Hifadhi katika maswala mazima ya ulinzi wa misitu na Wanyamapori hususani Sokwemtu pamoja na vyanzo vya maji pia mtunze mradi huu ili kuweza kuwapatia faida za kiuchumi na kimazingira”. alisema Mhe.Kalli.

Pia, Mhe.Kalli, alitoa rai kwa wananchi kujenga tabia ya kuzitembelea Hifadhi hususani Hifadhi ya Taifa Gombe ili kuweza kujionea vivutio lukuki vilivyomo katika hifadhi hizo pamoja na kuchangia pato la Taifa.

TANAPA kupitia idara ya Ujirani Mwema katika Hifadhi ya Taifa Gombe imetekeleza miradi mbalimbali iliyoibuliwa na wananchi ambayo imelenga katika utunzaji wa Mazingira kama Ufugaji nyuki, mfumo wa umeme jua kwa vikundi vya uvuvi kwa lengo la utunzaji wa fukwe na mazalia ya samaki kuzunguka fukwe za ziwa Tanganyika kuepusha matumizi ya mafuta ya taa ambayo husababisha uchafuzi wa ziwa.

Pamoja na utukelezaji wa miradi ya kimazingira TANAPA imetekeleza miradi ya kimaendeleo kama Ujenzi wa madarasa mawili katika shule ya msingi Bugamba, Ujenzi wa Madarasa matatu katika Shule ya Sekondari Bugamba, Ujenzi wa Madarasa mawili katika shule ya Msingi Mwamgongo, pamoja na ujenzi wa nyumba za walimu (Two in One)-katika Kijiji cha Mwamgongo, Miradi ambayo kwa ujumla wake imegharimu TANAPA zaidi ya shillingi millioni 230.


Post a Comment

0 Comments