Ticker

6/recent/ticker-posts

MADAKTARI BINGWA WAPONGEZWA KWA UTOAJI HUDUMA BORA.

Mwenyekiti wa Ccm Mkoa wa Tanga Abdalla Rajabu akiongea na waandishi wa habari baada ya kukagua kazi ya utoaji huduma kwa wagonjwa inayofanya na madaktari bingwa.
Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Mkoa wa Tanga Juma Ramadhani Juma kushoto akitoa maelezo kwa mwenyekiti juu ya huduma zinazotolewa.
Mkurugenzi msaidizi hospitali ya Benjamin Mkapa, ambaye ni daktari wa upasuaji wa mishipa ya fahamu na ubongo akieleza kuhusu mwitikio wa wagonjwa.

***************************


Na Hamida Kamchalla, TANGA


MADAKTARI bingwa kutoka hospitali ya Benjamin Mkapa wamepongezwa kwa huduma kwa jitihada na huduma bora wanazotoa kwa wananchi wa Mkoa wa Tanga tangu walipoweka kambi februari 27 mwaka huu hospitali ya rufani ya Bombo.


Chama cha mapinduzi CCM Mkoa wa Tanga kimetembelea hospitalini hapo na kujionea jitihada zinazofanywa na madaktari bingwa hao kukutana na wananchi na kutoa huduma za matibabu ya kibingwa ambazo baadhi ya wananchi wasingeweza kuzipata ikiwemo matibabu ya Moyo, Figo, pamoja na kusafisha damu.


Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga Abdalla Rajabu amesema huduma hizo ambazo zimetolewa kwa siku 5 kwenye hospotali ni sehemu ya jitihada inayofanywa serikali kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za afya.


Aidha amesema chama hicho kitaendelea kuwatia moyo madaktari hao kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kushughulika na magonjwa ya wananchi ambayo pengine yangekuwa chanzo cha jamii kupoteza maisha kwa kukosa matibabu.


“Tuliona ni vyema, sisi kama chama kufika hapa kwajili ya kuwapongeza kuwatia moyo kwa kazi kubwa wanayoifanya, tukifahamu kazi hii ya kuwatibu watu ni kazi ya wito na ndio maana hata Rais wetu Dkt Samia Suluhu Hassan amekuwa akiongea na madaktari na kuwatia moyo ya kwamba wanachokipata hakilingani na kazi wanazozifanya" amesema Mwenyekiti.


Amebainisha kwamba madaktari bingwa wabobezi kutoka hospitali ya Benjamini Mkapa mbali na kutoa huduma hiyo watawaongezea uwezo madaktari bingwa waliopo katika hospitali ya Bombo.


Kwa upande wake kaimu Mganga Mfawidhi wa hospitali ya rufani Bombo, Mkoa wa Tanga Dr. Juma Ramadhani Juma amesema wamepokea jumla ya wataalamu 12 ambao watawasaidia kwenye huduma mbalimbali ikiwemo mtaalamu wa upasuaji wa mishipa ya fahamu, mifupa, mfumo wa haja ndogo, magonjwa ya ndani, Figo, moyo, magonjwa ya watoto, macho, kinywa na meno pamoja na uzazi kwa wakina mama.


“Hawa madaktari bingwa wamekuja kutuongezea uzoefu hususani kwa madaktari bingwa ambao tuko nao kwenye hospitali yetu kiukweli wananchi wa Mkoa wa Tanga wameonyesha mwitikio mkubwa sana wamekuja kupata huduma kwa wingi kila siku, kwaniaba ya hospitali ya Bombo tunamshukuru Mheshimiwa Ummy mwalimu mbunge wetu na waziri wa afya kwa kutuletea wataalamu hawa, “amesema Juma


Naye Daktari wa upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu Dr. Henry Humba ambaye pia ni Mkurugenzi msaidizi katika Hospitali ya Benjamini Mkapa amesema kuwa mpaka sasa wamepokea wagonjwa wengi wenye matatizo ya macho ambapo takribani watu 194 ambao kati yao 19 wamebainika kuwa na matatizo yanayohitaji upasuaji.


“Kusema ukweli mwitikio umekuwa mkubwa wengine waliokuja kwa wingi ni wenye matatizo ya mifupa na viungo mpaka jana takribani wagonjwa 64 na katika hao wagonjwa 15 wanahitaji kubadilishiwa viungo kama nyonga na magoti na pia wagonjwa wenye matatizo ya ubongo na kichwa tumepokea wagonjwa 25 na katika hao tumepata wagonjwa 3 ambao tayari yumeshawafanyia upasuaji" amesisitiza.


Baadhi ya wananchi Mkoani Tanga waliopatiwa huduma ya matibabu wamesema huduma hiyo imekuja kwa wakati muafaka na kwamba wengi walishindwa kufuata madaktari hao kutokana na kutokuwa na gharama za matibabu.


Huduma hiyo mpaka sasa imewezesha kuhudumia wagonjwa zaidi ya 400 tofauti na matarajio ya kuhudumia wagonjwa 200 ambao walitarajiwa kupatiwa huduma ndani ya muda wa siku 5.

Post a Comment

0 Comments