Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Wakili Anna Henga akizungumza na waandishi wa habari leoMachi 28,2023 katika ofisi za LHRC Jijini Dar es Salaam.
**************************
KITUO Cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimeendelea kupendekeza umri wa kuolewa kwa mtoto wa kike kuwa miaka 18 huku wakiiomba Serikali kurekebisha vifungu vya 13 na 17 vya sheria ya ndoa vinavyoruhusu mtoto kuolewa akiwa na chini ya umri huo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 28,2023 Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Wakili Anna Henga amesema sheria ya ndoa ya mwaka 1971 inaruhusu ndoa kwa mtoto wa kike katika umri wa miaka 14 na 15 kabla ya kubatilishwa na mahakama ambapo inapingana na sheria nyingine ikiwemo ya mtoto inayotaka mtoto kutokujihusisha na vitendo vya ngono hadi atakapofikisha miaka 18.
Aidha amezitaka mamlaka na wadau kutumia nafasi zao kuunga mkono juhudi za kupambana dhidi ya mila kandamizi zinazomnyima mtoto wa kike haki zake za msingi.
Amesisitiza kuwa ndoa za utotoni zina madhara makubwa kwa watoto wa kike na Taifa kwa ujumla na kuendelea kulisababishia Taifa hasara kubwa ambazo ni pamoja na kupoteza fursa za Elimu na ujuzi wa kazi, kupata maambukizi ya Virusi vya Ukimwi na Magonjwa mengine ya zinaa.
Kwa upande wake Afisa Mwandamizi Jinsia LHRC, Bi.Getrude Dyabere ameitaka serikali iondoe sheria kandamizi zote na kuhakikisha ulinzi wa mtoto kisheria unapatikana katika sheria zote za msingi katika ulinzi wa mtoto.
Amesema Sheria ya Elimu inatakiwa kuangalia upya kutokana kuwa kikwazo kwa mabinti kuendelea na masomo endapo wataamua kurudi Shule baada ya kuolewa.
0 Comments