Ticker

6/recent/ticker-posts

JE, WANAWAKE WA KITANZANIA WANA NAFASI GANI KATIKA SEKTA YA MAGARI NCHINI?


Norah Simkoko ambaye ni mmoja ya wasichana wanafunzi wa ufundi magari ambao wameshiriki mafunzo maalumu ya ufundi yaliyotolewa na kampuni ya CFAO Motors Tanzania akipokea cheti cha ushiri wakati wa hafla ya kusheherekea Siku ya Wanawake Duniani iliyofanyika Machi 7, 2023 katika ofisi za kampuni hiyo jijini Dar es Salaam. Anayemkabidhi cheti ni Mkurugenz Mtendaji wa CFAO Motors Tanzania, François Bompart.  
Wanafunzi wa ufundi magari kutoka VETA ambao wameshiriki mafunzo maalumu ya ufundi yaliyotolewa na kampuni ya CFAO Motors Tanzania wakiwa na vyeti vyao vya ushiri katika picha ya pamoja na wafanyakazi wanawake wa kampuni hiyo.
****

Kama ilivyo kwa sehemu nyingine za dunia, sekta ya magari nchini Tanzania imekuwa ikikua kwa kasi na kuwa sehemu muhimu ya uchumi wa nchi. Ripoti ya Tanzania Automotive Market, Size, Share, Outlook, and Growth Opportunities 2022-2030 inaonyesha kuwa soko la magari Tanzania linakua kwa kasi hasa baada ya Dunia kuondokana na mdororo na vikwazo vya usambazaji uliosababishwa na janga la UVIKO-19. Soko la magari Tanzania linatarajiwa kukua kwa kiwango cha kati cha ukuaji wa mwaka hadi mwaka (CAGR) kati ya 2023 na 2030.

Sekta ya magari inategemea sana uagizaji wa magari na vifaa vya magari kutoka kwa wazalishaji wakubwa duniani. Umuhimu wa magari unazidi kuongezeka hasa kwa kuzingatia kwamba magari ni kiini cha sekta muhimu ikiwemo sekta ya usafirishaji. Bila uwepo wa sekta ya usafirishaji yenye ufanisi, sekta muhimu kama kilimo, utalii, uchimbaji madini, na biashara haziwezi kujiendesha kwa ufanisi. Aidha, sekta za huduma kama afya, elimu, na huduma za kifedha zinahitaji usafirishaji  wenye ufanisi ili kufanya kazi vizuri. Huduma za usafirishaji, ambazo kwa kiasi kikubwa zinategemea magari, pia zina mchango mkubwa katika mizunguko ya kila siku ya binadamu.

Ni jambo lisilo na ubishi kuwa kwa muda mrefu, sekta ya magari imetawaliwa na wanaume hadi kufanya jamii kuamini kwamba sekta hiyo ni ya kiume na wanawake wanaonekana kutokuwa na uwezo wa kushiriki na kuwa na mchango. Ingawa hakuna takwimu rasmi zinazoonesha uwiano kati ya wanaume na wanawake katika sekta ya magari, hali halisi inaonesha kwamba wanaume ndio wengi zaidi katika mnyororo wa thamani wa sekta ya magari nchini Tanzania. 

Licha ya ukweli kwamba sekta ya magari kwa imedhibitiwa na wanaume, kuna sehemu kubwa ambayo wanawake wanachangia katika sekta hiyo hapa Tanzania. Kuna njia mbalimbali ambazo wanawake wa Kitanzania wanashiriki katika sekta hiyo na baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wa magari nchini wanafanya juhudi za makusudi kupunguza pengo la kijinsia katika sekta hiyo. 

Katika miaka ya hivi karibuni, sura za wanawake wanaoshiriki katika sekta hiyo zimeonekana wakichukua majukumu muhimu ikiwa ni pamoja na nafasi za mauzo na masoko, madereva, na hata mafundi wa magari. Mbali na jitihada binafsi za wanawake wachache, makampuni makubwa yanayojihusisha na biashara ya magari kama CFAO Motors Tanzania wamewapa wanawake fursa ya kuchangia katika sekta hiyo. Wanawake sasa wanashikilia nafasi muhimu kama vile wakurugenzi wa mauzo na masoko katika makapuni ya uuzaji wa magari. Hii inaonesha kwamba sasa wanawake hawashiriki tu katika sekta hiyo bali pia wanashikilia nafasi ambazo zinawawezesha kutoa mchango wao katika maendeleo ya sekta hiyo.


Mmoja wa wanawake wachache katika sekta ya magari Tanzania ambaye ana nafasi ya kimkakati katika kampuni kubwa ya usambazaji wa magari Afrika ni Bi. Tharaia Ally Ahmed, Mkurugenzi wa Mauzo na Masoko wa CFAO Motors Tanzania. Alipoulizwa kuhusu safari yake ya maisha na namna ambavyo amefanikiwa kuwa katika nafasi muhimu katika sekta ya magari, alikiri kuwa hata wanawake wachache ambao wana uwezo wa kiufundi na wanapenda kuwa katika sekta ya magari wanasita kuthubutu na kufanya maamuzi hayo kutokana na mitazamo inayobagua wanawake. Licha ya umakini na ujasiri wake, alikiri kwamba kuchagua njia hiyo haikuwa rahisi kwake. 

"Unajua jinsi ilivyo ngumu kuwashawishi wanaume na hata wanawake wengi kuwa mwanamke anaweza kuwa na ufahamu zaidi wa sekta ya magari kuliko wanaume wengi. Kwa hivyo, haikuwa rahisi; ilihitaji ujasiri, na ninashukuru CFAO Motors Tanzania kwa kuamini uwezo wangu bila kujali jinsia. Baada ya kufanya kazi hapa kwa muda, nimegundua kwamba kampuni inaelekea kwenye uelekeo sahihi linapokuja suala la kutoa fursa kwa wanawake. Bado idadi ya wanaume ni kubwa kuzidi wanawake lakini tuna idadi nzuri ya wanawake wanaofanya kazi katika nafasi za mauzo na nafasi nyingine za juu kama vile mameneja wa masoko na wengine. Miaka kadhaa iliyopita uwiano ulikuwa chini zaidi,” Bi. Tharaia alisema kwa tabasamu la kija.

Aliendelea kusema kuwa jitihada za makusudi za CFAO Motors ni muhimu katika kuziba pengo la kijinsia katika sekta hiyo.

CFAO Motors haitekelezi tu sera ya usawa wa kijinsia ndani ya kampuni, bali pia inachukua hatua nyigine muhimu za kuwawezesha wanawake katika sekta ya magari kwa ujuml. Kama sehemu ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, kampuni hiyo imezindua programu ya kuwajengea uwezo wanawake walio katika sekta ya magari prgram iliyopewa jina la “CFAO Motors Empower Her Future Initiative.” Kupitia programu hiyo, CFAO Motors wamefanya mafunzo kwa wanafunzi wanawake wanaosoma ufundi magari katika Mamlaka ya Mafunzo ya Ufundi Tanzania (VETA). Mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha mafundi wanawake kupata ujuzi unaohitajika ili kuendana na kasi ya mapinduzi ya teknolojia katika sekta ya magari. Huduma kwa wateja, ukaguzi wa magari, na utunzaji wa magari ni miongoni mwa mada zilizofundishwa na wakufunzi wenye hadhi ya kimataifa kutoka kampuni ya CFAO Motors. Pia, washiriki wa mafunzo hayo wamepatiwa vyeti vitakavyiwasaidia kutambulisha ujuzi wao. 

Norah Simkoko ambaye ni moja ya wanufaika wa mafunzo hayo ameishukuru CFAO Motors kwa kuwafanyia mafunzo ambayo amekiri yatawasaidia sana kuwa na ujuzi wa teknolojia za kisasa za magari na kuwaweza kukabiliana na ushindani mkubwa wa ajira katika sekta hiyo.

“Nimejifunza mambo mengi mapya ambayo hatufundishwi chuoni. Nimejifunza vitu vingi sana kuhusu mifumo ya kisasa ya magari ambayo mengi yanatumia mifumo ya umeme. Nawashukuru sana CFAO Motors kwa mafunzo haya kwani yatanisaidia binafsi kuongeza ufanisi wangu kama fundi wa magari.” Alisema Simkoko. 

Kwa ujumla, wanawake nchini Tanzania wana nafasi kubwa katika sekta ya magari. Ushiriki wa wanawake si tu unaleta mchango katika ukuaji wa sekta hiyo lakini pia unapunguza pengo la kijinsia katika sekta ambayo kiasili imetawaliwa na wanaume. Juhudi za CFAO Motors katika kushirikisha wanawake katika sekta ya magari ni mfano mzuri kwa wadau wa sekta hiyo nchini Tanzania kuwapa nafasi wanawake. Aina hii ya juhudi haitasaidia tu pengo la kijinsia lakini pia itachangia kukukuza sekta ya magari na uchumi wa nchi kwa ujumla.

Post a Comment

0 Comments