Meneja Mkuu wa mradi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika ya Mashariki ( EACOP) Wendy Brown akipeana mkono na kiongozi wa kimila wa kabila la Wataturu Gesuda Masanja wakati wa zoezi la kusaini makubaliano na EACOP ili bomba la mafuta kuchepuka makaburi yao ya asili ili kuheshimu mila na tamaduni zao.
Jamii ya Wataturu wa kijiji cha Mwamayoka wilayani Igunga mkoani Tabora wakiwa katika sherehe ya kusaini makubaliano na mradi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki ( EACOP) ya kuchepusha makaburi yao ya asili ili kuendelea kulinda mila na tamaduni zao.
******************
Kampuni ya Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP Ltd) kwa kuheshimu mila na desturi za watu walioguswa na mradi (PAPs) imesaini mkataba wa kusimamia haki na kuheshimu tamaduni za Wazawa (FPIC) na jamii ya Wataturu wanaoishi katika kijiji cha Mwamayoka katika Wilaya ya Igunga, Tanzania kwa ajili ya kuchepusha njia ili kuyalinda makaburi yao ya kimila
Awali Wataturu hao walikuwa na wasiwasi wa kuathiriwa kwa makaburi yao yaliyopo eneo la Bung’enda na maeneo yao mengine kadhaa ya kuabudia endapo mradi ungeanza ujenzi.
Akizungumza wakati wa sherehe ya kusaini makubaliano hayo, Mkurugenzi Mkuu wa EACOP Tanzania Wendy Brown amesema baada ya majadiliano na jamii na viongozi wa kimila, EACOP ilifanya mapitio ya kiufundi na kukubali kupitisha bomba hilo katika njia mpya ili kutokuwa na athari yoyote katika maeneo yao muhimu ya mila na kiutamaduni.
Bi. Wendy Brown amesema, EACOP inaheshimu haki na mila za makundi yote ya kikabila yanayoguswa na mradi.
Hivyo, amesema EACOP itaendelea kushirikiana na jamii zote zilizoguswa na mradi pamoja na viongozi wao wa kimila ili kuhakikisha kuwa maoni yao yamezingatiwa wakati wote wa kupanga na kutekeleza mradi.
Mkataba huu wa FPIC ni wa pili kusainiwa na EACOP baada ya kusaini mkataba kama huo hapo awali na jamii ya Akie inayoishi Kanda ya Kaskazini.
Amesema kusainiwa kwa mikataba hii ni kielelezo tosha kuwa mradi wa EACOP unashirikisha makundi yanayoguswa katika ngazi zote za utekelezaji wake na kuheshimu mila, tamaduni na haki za jamii husika.
Ameongeza mradi wa EACOP unatekelezwa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya haki za binadamu, jamii na utunzaji wa mazingira.
Gesuda Masanja, ambaye ni chifu wa jumuiya ya Wataturu alipongeza hatua ya EACOP kwa kuzingatia mila zao, akisema kuwa mradi huo utasaidia kwa maendeleo ya jamii yake.
Akizungumza awali, Martha Bayo, ambaye ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Igunga, pia alipongeza hatua ya EACOP na kuitaka jamii ya Wataturu kuwa walinzi wa bomba hilo la mafuta ghafi litakapokamilika.
Lucas Bugota, ambaye ni Diwani wa Kata ya Igunga pia ameusifu mradi wa EACOP kwa hatua hiyo, akisema jamii ya Wataturu wameweka historia katika kulinda mila na tamaduni zao.
Nailejileji Tipap kutoka Jukwaa la Wafugaji lisilokuwa la Kiserikali (Pingos) alisema hatua ya kampuni ya EACOP kusaini mkataba wa FPIC inalinda maslahi ya jamii ya Wataturu hao.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo (DAS) Godlove Kawiche aliihakikishia kampuni ya EACOP juu ya dhamira ya serikali ya kutekeleza mradi wa bomba hilo la mafuta ghafi.
Pia aliipongeza timu ya wataalam wa EACOP kwa kushirikisha jamii zilizoathiriwa katika mchakato mzima wa ujenzi wa bomba hilo
0 Comments