NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dk. Mohammed Said Mohammed 'Dimwa',akizungumza na wananchi katika mradi wa ujenzi wa tanki la lita milioni moja linalojengwa katika kijiji cha Bubwini Dundua, Wilaya ya kaskazini ‘’A’’.
**********************
NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dk. Mohammed Said Mohammed 'Dimwa',amesema kasi ya utekelezaji wa miradi ya maji safi na salama itamaliza changamoto ya upungufu wa nishati hiyo nchini.
Alisema serikali ya awamu ya nane chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar Dk.Hussein Ali Mwinyi,imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kumaliza changamoto hiyo kwa kutekeleza miradi mikubwa mbali mbali ya maji ili wananchi wa mijini na vijijini wapate huduma hizo kwa wakati.
Dk.Dimwa aliyasema hayo wakati akikagua ujenzi wa Tanki la Maji Bumbwini Dundua wilaya ya Kaskazini B mkoa wa Kaskazini Unguja ikiwa ni katika ziara yake ya kukagua utekeleza wa ilani ya CCM katika Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Alisema, sasa hivi Zanzibar kuna miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo ya ujenzi wa miundombinu mipya ya maji, inayotokana na jitihada za viongozi wakuu wa CCM akiwemo Mwenyekiti wa Chama hicho Dk. Samia na Makamu Mwenyekiti Dk. Mwinyi.
Alisema, viongozi hao wamejitahidi kwa nguvu zao zote kuifungua Zanzibar kimanedeleo hivyo alisema, yeye akiwa kama msimamizi wa sera na utekelezaji hao hataridhia kama mwanachama wake au kiongozi yeyote hatimizi wajibu wake ipasavyo.
"Naamini kuwa siku chache zijazo kupitia miradi hii ya maji inayojengwa katika maeneo mbali mbali nchini suala la upungufu wa maji litabaki kuwa historia katika nchini yetu ya Zanzibar.”alisema Dkt.Dimwa.
Aidha Dk. Dimwa alimpongeza mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Ndg.Ayoub Mohamed Mahmoud kwa jitihada zake za kuufanya mkoa huo kuwa na maendeleo na kutekeleza ilani ya Uchaguzi kwa kiwango kikubwa. Dk. Dimwa pia aliwataka wanachama na viongozi wa CCM kutojibu maneno madogo madogo ya wapinzani na badala yake wao watajibu kwa hoja na siyo mipasho.
"Chama cha Mapinduzi kinakwenda na amani wala hakitaki mifarakano ndiyo tukaleta serikali ya umoja wa kitafa, anotaka kuibeza sisi tunajua imo ndani ya katiba yetu, wao wakianza maneno ya choko choko sisi tunajibu kwa sera zetu, tunawajibu kwa miradi mikubwa ambayo ipo," alisema
"Hatujashindwa kujibu kwa hoja lakini kubwa tunataka uvumilivu wetu wa kisiasa uendelee, mshikamano wetu uendelee lakini na maridhiano tunayapenda sana Chama Cha Mapinduzi," alisema.
Alieleza kuwa, wanapenda kila mtu aishi kwa amani na ndiyo Chama cha Mapinduzi kinavyonadi sera zake wala hakipendi mifarakano.
Pamoja na hayo Dkt.Dimwa, alimtaka Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja kuhakikisha kuwa anaisimamia vizuri miradi hiyo ya maji kwa kuhakikisha kuwa wananchi wa mkoa huo wanapata huduma maji safi na salama kwa uhakika.
Aidha aliwapongeza Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) kwa kutekeleza vizuri mradi huo na kuwaambia kama watahitaji nguvu kazi basi taasisi yake itasaidia kwa namna moja au nyengine ili kuhakikisha mabomba yamelazwa kwa wakati.
Alisema, Chama cha Mapinduzi kina jukumu kubwa sana kwa wananchi kwani walikuja kutoa ahadi na kwa wananchi na kusema kuwa watatekeleza yale waliyoyaahidi.
Alisema, ameona Mapinduzi makubwa sana kwenye Jimbo la Bumbwini na Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa ujumla na hiyo ikiwa ni utekelezaji wa Ilani kwa asilimia kubwa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ayoub Mohammed Mahmoud alisema, Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Kaskazini Unguja kimetekeleza ilani ya CCM kwa mafanikio makubwa.
Alisema, kwa mujibu wa ibara ya 186 (A), inaeleza kwamba CCM imeiagiza serikali kuhakikisha kwamba inawapatia wananchi wote wa Zanzibar mijini na vijijini pamoja na maeneo ya visiwa vidogo wanapatiwa maji safi na salama ifikapo 2025.
Hivyo alisema, serikali ya awamu ya nane chini ya uongozi wa Dk. Hussein Ali Mwinyi imepokea agizo hilo na kwamba wasaidizi wake kwa ngazi ya mkoa wanayatekeleza na kusimamia kazi hiyo.
Hivyo alisema, mkoa huo wanaendelea na ujenzi wa matanki na uchimbaji wa visima takribani vinne ambapo vyote vimekamilka na eneo jengine ni ulazaji wa mabomba lengo likiwa ni upatikanaji wa maji katika mkoa huo uwe ni wa uhakika.
0 Comments