Mhe. Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akizungumza katika kikao na Menejimenti ya Benki ya CRDB-Burundi alipotembelea benki hiyo mjini Bujumbura nchini Burundi, ambako Benki hiyo inatoa huduma za kibenki kwa miaka kumi sasa.
Meneja wa benki ya CRDB nchini Burundi Bw. Fredrick Siwale akizungumza wakati alipotembelewa na ugeni kutoka Tanzania uliongozwa na Mhe. Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb).
****************************
Na. Ramadhani Kissimba – Bujumbura Burundi
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ameitaka Benki ya CRDB kuharakisha matumizi ya mfumo wa malipo ya Serikali kwa njia ya kieletroniki (GePG) ili kuongeza na kuharakisha shughuli za kiuchumi kati ya Tanzania na Burundi.
Mhe. Dkt. Nchemba alitoa maagizo hayo alipotembelea na kufanya kikao na Menejimenti ya Benki hiyo mjini Bujumbura nchini Burundi, ambako Benki hiyo inatoa huduma za kibenki kwa miaka kumi sasa.
Mhe. Nchemba alisema kwamba amefarijika kusikia mchakato wa kuanza kwa matumizi ya ‘’control number’’ kwa ajili ya malipo ya ushuru kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na uondoshaji mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam upo katika hatua za mwisho.
Alisema kuwa kukamilika kwa matumizi ya mfumo huo wa malipo ya Serikali kwa njia ya kieletroniki kutasaidia kupunguza usumbufu na hasara wanayopata wanafanyabiashara wa Burundi wanapotaka kulipia mizigo yao inayopita katika Bandari za Tanzania.
‘’Nimefarijika sana niliposikia hilo la ‘contorl number’ kuwa litafanyika huku huku Burundi kwa sababu litawezesha na kuharakisha shughuli za kiuchumi na hicho ndicho kitu kikubwa ambacho Viongozi wetu wamekuwa wakikitaka na kukitamani kifanyike haraka’’ alisema Mhe. Dkt. Nchemba.
Aliongeza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Burundi Mhe. Evariste Ndayishimiye wamekuwa wakihimiza urahisishaji wa ufanyaji biashara kati ya nchi hizi mbili, hivyo ni vema matumizi ya ‘control number’ yakaanza haraka ili kurahisisha ukuaji wa uchumi wa pande zote mbili.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Lawrence Tax ambaye aliongozana na Mhe. Dkt. Nchemba kwenye ziara hiyo, aliipongeza Benki hiyo kwa hatua waliyoichukua ya kutoa huduma za kibenki nje ya Tanzania jambo ambalo linaitangaza Tanzania na kurahisisha ufanyaji wa biashara kwa Watanzania wanaokuja Burundi na Warundi wanaofanya biashara na Tanzania.
Mhe. Dkt. Tax ameisihi benki hiyo kupanua huduma zao ili zienee kote nchini Burundi na kuvuka mipaka hadi katika nchi ya Jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na si kuishia katika jiji la Bujumbura pekee.
Awali akizungumza katika Mkutano huo Meneja wa Benki ya CRDB nchini Burundi Bw. Fredrick Siwale, alisema kuwa pamoja na kufanya shughuli za Kibenki nchini Burundi pia wamekuwa wakifanya siasa ya Kidiplomasia ya Uchumi ili kuwavutia wawekezaji kutoka Burundi kwenda kuwekeza nchini Tanzania na pia kuwahimiza Watanzania kuangalia fursa za uwekezaji zinazopatikana nchini Burundi.
Bw. Siwale alisema kwamba katika kutekeleza suala zima la uwekezaji nchini Tanzania wamekuwa wakiwapatia mikopo baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wa Burundi ili kutumia mikopo hiyo kuwekeza nchini Tanzania ambapo wafanya biashara hao wamewekeza kwa kujenga kiwanda cha Mbolea Jijini Dodoma, kiwanda cha kutengeneza saruji mjini Kigoma na ujenzi wa hotel ya kitalii mjini Tanga.
Mhe. Dkt. Nchemba na ujumbe huo pia walipata fursa ya kutembelea ofisi ya Shirika la Ndege Tanzania (ATC) na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) zilizopo nchini Burundi.
Katika ziara hiyo Mhe. Dkt. Nchemba aliambatana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt Stergomena Lawrence Tax, Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi – Sekta ya Ujenzi Mhe. Mha. Godfrey M. Kasekenya, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Geoffrey Mizengo Pinda na Balozi wa Tanzania nchini Burundi Mhe. Dkt. Jilly Maleko.
Mhe. Dkt. Nchemba na baadhi ya Mawaziri kutoka Tanzania wapo nchini Burundi kuhudhuria Mkutano wa Kawaida wa 43 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ambapo katika Mkutano huo agenda mbalimbali zinatarajiwa kujadiliwa kuhusu mtangamano wa Jumuiya hiyo.
0 Comments