Ticker

6/recent/ticker-posts

WANANCHI TANGA WAONYWA MATUMIZI BORA YA VYANDARUA VYENYE VIUATILIFU

Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe.Omari Mgumba katikati akikata utepe ishara ya kuzindua zoezi la ugawaji vyandarua kwa wanafunzi wa shule za msingi mkoani humo.


Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe.Omari Mgumba akikabidhi robota la vyandarua kwa mwalimu wa shule ya msingi Mwenge jijini Tanga.


Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe.Omari Mgumba akimkabidhi mwanafunzi wa shule ya msingi Mwenge chandarua chenye viuatilifu kwa msaada wa serikali.


***********************
Na Hamida Kamchalla, TANGA.




KUTOKANA na mazoea ya wananchi kwa Mkoa wa Tanga kujenga mazoea ya matumizi yasiyo rasmi katika matumizi bora ya vyandarua vya misaada kutoka serikalini, onyo kali limetolewa kwa wananchi hao.


Mkuu wa Mkoa wa Tanga Omari Mgumba ametoa onyo kwa wananchi mkoani humo kuacha tabia ya kubadili matumizi ya vyandarua vya msaada vinavyotolewa na serikali katika jitihada za kupambana na ugonjwa wa malaria kwa kufungua kuku au kuvulia samaki.


Mgumba ametoa onyo hiyo wakati wa uzinduzi wa zoezi la ugawaji wa vyandarua kwa wanafunzi wa shule za msingi mkoani Tanga ambapo shule zote 1083 katika Wilaya zote nane zitafikiwa.


"Napenda kuwaagiza viongozi wote wa serikali, dini na jamii kusimamia matumizi sahihi ya vyandarua hivi, jamii ielimishwe umuhimu na matumizi sahihi ili kuepuka matumizi yasiyotarajiwa kama tlivyoshuhudia kwenye mazoezi mengine yaliyopita,


"Walimu mashuleni kwa kushirikiana na wataalamu wa afya mtoe elimu na kusisitiza matumizi sahihi ya vyandarua hivi kwa wanafunzi wakati wa ugawaji shuleni" amesisitiza Mgumba.


Mgumba amebainisha kwamba ili kuhakikisha kiwango cha maambukizi ya malaria kinapungua hadi kufikia asilimia 0 ifikapo mwaka 2030, serikali kupitia Wizara ya Afya na OR - TAMISEMI imeandaa zoezi la ugawaji wa vyandarua vyenye viuatilifu kwa wanafunzi hao kuanzia darasa la kwanza hadi la saba.


"Katika zoezi hili jumla ya vyandarua 529,641 vinatarajiwa kugawiwa kwa wanafunzi katika shule zote 1083 za msingi katika Mkoa wetu, usambazaji mashuleni utatekelezwa kwa muda wa siku 45, tumeanza leo kwa jiji la Tanga na utaendelea kwatika halmashauri zote za Korogwe, Muheza, Pangani, Handeni, Kilindi, Lushoto na Bumbuli" amesema.


"Kwahiyo bado tunalo jukumu kubwa kwa kuchukua hatua mbalimbali za kudhibiti ugonjwa wa malaria hadi kutikomeza kabisa kabla ya mwaka 2030 na hii inahitaji ushirikiano mkubwa kwa wananchi kwa kuwapa elimu juu ya athari ya ugonjwa huu na matumizi Bora ya vyandarua hivi" amefafanua.


Naye Meneja wa Bohari ya Dawa (MSD) Mkoa wa Tanga Siti Abdulrahman amebainisha kuwa serikali imewapa jukumu la kusambaza vyandarua hivyo kwa mikoa ipatayo mitano ya Iringa, Dodoma, Manyara, Kilimanjaro na Tanga.


Amesema kwa Mkoa wa Tanga wamepatiwa vyandarua 529,641 ambavyo vina thamani ya sh bilioni 2.6 vtakavyogawiwa kwa shule zote za msingi kuanzia mwanafunzi wa darasa la kwanza hadi la saba.


"Tumekabidhiwa jukumu la ugawaji wa vyandua hivi, serikali ikiwa na lengo la kupunguza maambukizi ya malaria kutoka asilimia 7.5 ya mwaka 2017 hadi kufikia kiwango cha chini cha asilimia 3.5 ifikapo 2025 na hatimaye kutikomeza kabisa ugonjwa huu ifikapo mwaka 2030" amesema.


Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Tanga Hashimu Mgandilwa amesema kwa nafasi yake ana uwezo wa kuingia mahali popote akishirikiana na viongozi wengine wa serikali kuhakikisha wananchi hawaendi kinyume na matakwa yaliyowekwa, hivyo ikibidi kufanya msako wa chumba kwa chumba.

Post a Comment

0 Comments