Afisa Maadili Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kanda ya Kaskazini – Arusha Bw. Baraka Mgimba akitoa mada kuhusu Uadilifu katika mafunzo kwa viongozi na watumishi wa umma kutoka Chuo cha Usimamizi wa Wanyama Pori –Mweka. Mafunzo hayo yalifanyika tarehe 24 February, 2023 chuoni hapo mkoani Kilimanjaro
Afisa Maadili Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kanda ya Kaskazini – Arusha Bw. Musiba Magoma akitoa mada kuhusu Hati ya Ahadi ya Uadilifu katika mafunzo kwa viongozi na watumishi wa umma kutoka Chuo cha Usimamizi wa Wanyama Pori –Mweka. Mafunzo hayo yalifanyika tarehe 24 February, 2023 chuoni hapo mkoani Kilimanjaro.
Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kanda ya Kaskazini- Arusha imetoa mafunzo kuhusu Uadilifu kwa Viongozi na watumishi wa Umma kutoka Chuo cha Usimamizi wa Wanyama Pori -Mweka mkoani Kilimanjaro na kuwaasa kuwa waadilifu katika Utumishi wa Umma.Mafunzo hayo yalifanyika chuoni hapo tarehe 24 February, 2023.
Akitoa mada kuhusu Uadilifu, Afisa Maadili kutoka Sekretarieti ya Maadili kanda ya Kaskazini- Arusha Bw. Baraka Mgimba alieleza kuwa Viongozi na watumishi wote wa Umma wanapaswa kutenda kazi kwa uadilifu wa hali ya juu ikiwa ni moja ya misingi ya maadili katika utumishi wa Umma.
Bw. Mgimba alieleza kuwa uadilifu ni hali ya kufanya jambo sahihi katika wakati sahihi hata pale ambapo hakuna mtu anayekuona “uadilifu huanza nafsini mwa mtu mwenyewe ndipo unaanza kuonekana kwa wengine.”alisema.
Bw, Mgimba alielezea sifa za mtu muadilifu kuwa ni pamoja na; kujali wengine, kujitolea kusaidia watu wenye uhitaji, kuwa msikivu, kujizuia na tamaa, kuwa mnyenyekevu, kuwa mwaminifu katika hali zote pamoja sifa nyingine nyingi ambazo binadamu yeyote anapaswa kuwa nazo.
Aidha Bw. Mgimba aliendelea kusema kuwa kiongozi ama mtumishi wa Umma anapaswa kutenda kazi kwa kufuata kanuni misingi na miongozo mbalimbali iliyowekwa ili kuleta tija katika utendaji kazi wao ‘‘ Misingi hii pamoja na kanuni na miongozo mbalimbali iliyowekwa nchini ikifuatwa vizuri itakuza hali ya uadilifu kwa viongozi na watumishi wote nchini ”
Kwa mujibu wa Bw. Mgimba alieleza kuwa Serikali kupitia Sekretarieti ya Maadili imedhamiria kukuza hali ya uadilifu nchini kwa kutoa mafunzo mbalimbali kwa viongozi na watumishi wa umma nchini lengo likiwa ni kuwakumbusha jinsi wanavyotakiwa kuenenda katika utendaji kazi wao.
Pamoja na hayo Bw. Mgimba aliongeza kuwa kiongozi na mtumishi yeyote ni kioo cha jamii inayomzunguka hivyo anapaswa kuishi maisha yatakayoipa jamii imani juu serikali yao kwani kiongozi na mtumishi wa Umma anafanya kazi kwa niaba ya serikali ‘‘ Kiongozi na mtumishi wa umma anapokua muadilifu na kutenda kazi katika hali ya uadilifu anajenga imani ya wananchi kwa serikali yao’’
Aidha akitoa mada nyingine iliyohusu Hati ya Ahadi ya Uadilifu kwa Viongozi na watumishi wa umma Bw. Musiba Magoma ambaye ni Afisa maadili kutoka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kanda ya kaskazini –Arusha alieleza kuwa kila kiongozi na mtumishi yeyote wa umma mara tuu anapoteuliwa ama kuajiriwa anapaswa kukiri Ahadi ya Uadilifu ambayo itampa dira ama mwongozo wa ni yapi anapaswa kufanya ama kutokufanya katika nafasi ama wadhifa wake .
Bw. Magoma alifafanua kuwa Ahadi ya Uadilifu kwa Viongozi na watumishi wa umma ina lengo la kuwahamasisha na kuwafanya kuwa na mwenendo unaofaa, inatoa nafasi kwa kiongozi na mtumishi wa Umma kujitathmini mwenyewe kutokana na kile alichoahidi na pia kuhamasisha viongozi na watumishi wa umma kuzingatia misingi ya maadili katika utendaji kazi wao.
Pamoja na hayo Bw. Magoma alieleza kuwa ipo misingi ya Ahadi ya Uadilifu inayomuongoza kiongozi kama vile Uwazi, uwajibikaji, uzingatiaji wa sheria kanuni na taratibu, kutoa huduma bora bila upendeleo, kuwa na matumizi sahihi ya taarifa pamoja na nyingine nyingi.
Katika hatua nyingine Bw. Magoma alifafanua kuwa zipo athari mbalimbali zinazotokana na kukiukwa kwa Ahadi ya Uadilifu kama vile wananchi kupoteza imani kwa serikali yao, kiongozi kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa kanuni sheria na taratibu,kiongozi ama mtumishi kusimamishwa kazi na nyingine nyingi ambazo zitaathiri hali ya kiongozi ama mtumishi wa umma, familia jamii na hata serikali kwa ujumla.
Akielezea umuhimu wa mafunzo hayo kwa watumishi hao, Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Wahab Kimaro alisema kuwa mafunzo kama hayo ni muhimu kwa viongozi na watumishi wa Umma na ni vyema yakatolewa mara kwa mara kwani yanaongeza ufanishi katika utendaji kazi wao wa kila siku.
“Tumepata watumishi wapya, wapo waliohamia pia kwa hiyo ni vyema wakapata mafunzo haya ya uadilifu ili sote tuzungumze lugha moja katika kutekeleza majukumu yetu” alisema.
Pamoja na hayo Pro. Kimaro alifafanua kuwa kiapo cha Ahadi ya Uadilifu kwa viongozi na watumishi wa Umma ni moja ya silaha muhimu ya kuwafanya kuwa waadilifu kwani binadamu yeyote huwa muadilifu ikiwa kuna mahala atapaswa kujieleza ama kuchukuliwa hatua na pia kinamfanya awe na hamasa ya kutekeleza kile alichoapa.
Prof. Kimaro aliongeza kuwa kiapo cha Ahadi ya Uadilifu kinasaidia sana kukuza nidhamu kwa viongozi na watumishi wa umma “ Kiapo hiki ni muhimu sana kwani mtumishi wa umma anapokwenda kinyume na taratibu na sheria zilizowekwa anachukuliwa hatua kwa kile alichosema kwamba atatekeleza katika kiapo chake” alisema.
Mafunzo hayo ya Siku moja yaliandaliwa na Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori –Mweka mkoani Kilimanjaro.
0 Comments