Ticker

6/recent/ticker-posts

TAX AONGOZA UJUMBE WA TANZANIAMKUTANO WA 42 WA BARAZA LA MAWAZIRIWA UMOJA WA AFRIKA


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akiongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 42 wa Baraza la Mawaziri la Umoja wa Afrika unaofanyika Addis Ababa tarehe 15 – 16 Februari 2023


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akisalimiana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Sudan Kusini, Mhe. Deng Dau Deng Malek katika Mkutano wa 42 wa Baraza la Mawaziri la Umoja wa Afrika unaofanyika Addis Ababa tarehe 15 – 16 Februari 2023


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia, Mhe. Demeke Mekonnen akijadili jambo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax kabla ya kuanza kwa Mkutano wa 42 wa Baraza la Mawaziri la Umoja wa Afrika unaofanyika Addis Ababa tarehe 15 – 16 Februari 2023


Sehemu ya ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax katika picha ya pamoja


Mawaziri mbalimbali walioshiriki Mkutano wa 42 wa Baraza la Mawaziri la Umoja wa Afrika wakiwa katika picha ya pamoja. Mkutano huo unaofanyika Addis Ababa tarehe 15 – 16 Februari 2023.

***************************

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) ameongoza ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano wa 42 wa Baraza la Mawaziri la Umoja wa Afrika unaofanyika Addis Ababa tarehe 15 – 16 Februari 2023.

Mkutano huu ni sehemu ya maandalizi ya Mkutano wa 36 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika utakaofanyika tarehe 18-19 Februari 2023.

Pamoja na mambo mengine, mkutano wa Mawaziri utajadili masuala ya kimkakati yanayohusu Bara la Afrika ikiwemo utekelezaji wa Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Afrika-AfCFTA, uhakika wa chakula, hali ya ulinzi na usalama, mabadiliko ya tabianchi, pamoja na masuala ya kiutawala na usimamizi wa rasilimali za Umoja wa Afrika.

Akichangia katika mkutano huo, Dkt. Tax alisisitiza umuhimu wa Kamisheni na Taasisi za Umoja wa Afrika kusimamia vyema rasilimali za Umoja wa Afrika kwa kuchukua hatua za kuondoa mapungufu yaliyobainika kwenye taarifa ya ukaguzi wa rasilimali za Umoja wa Afrika.

Mhe. Waziri pia alieleza hatua ambazo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inachukua katika kutekeleza Mikataba ya Uenyeji ya Taasisi za Umoja wa Afrika zilizopo Tanzania ambazo ni Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, Umoja wa Posta Afrika na Bodi ya Umoja wa Afrika ya Ushauri dhidi ya Rushwa.

Awali akiwasilisha hotuba yake ya ufunguzi, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC), Mhe. Moussa Faki Mahamat alisisitiza umuhimu wa Umoja wa Afrika kuendelea kutoa kipaumbele kwenye masuala yanayowagusa wananchi wa Afrika ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto mbalimbali za mabadiliko za kijamii, kiuchumi na kiusalama. Alisisitiza umuhimu wa Afrika kupunguza utegemezi wa chakula kutoka nje kwa kuongeza uzalishaji wa bidhaa za vyakula ndani ya bara la Afrika pamoja na kutumia fursa za mkataba wa AfCFTA katika kukuza Mtangamano wa Kiuchumi.

Bw. Faki aliongeza kuwa Umoja wa Afrika umeendelea kusimamia masuala ya amani na usalama katika bara la Afrika katika nchi za Ethiopia, Sudan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), na Libya ambapo jitihada zilizofanyika zimelenga zaidi kupata suluhisho la amani kwa mataifa hayo.

Kwa upande wake Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia, Mhe. Demeke Mekonnen amesema Ethiopia ameshukuru Umoja wa Afrika kwa mchango na ushirikiano wake ambao umewezesha kupatikana amani na utulivu nchini Ethiopia na kumaliza mgogoro uliodumu kwa muda wa miaka miwili. “Ethiopia inaamini kuwa kupitia Umoja wa Afrika amani, ulinzi na usalama vitailetea Afrika maendeleo zaidi,” alisema Mhe. Mekonnen.

Post a Comment

0 Comments