**************
NA Shemsa Mussa, KAGERA.
Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini RUWASA wameendelea kutekeleza azma ya Serikali ya kumtua mama ndoo kichwani ambapo kwa Kata ya Buyango, iliyopo Wilaya ya Missenyi, Mkoa wa Kagera ujenzi wa Mradi wa Maji Buyango unaotekelezwa na Mkandarasi Advanced Engineering Co. Ltd kwa gharama ya Tshs. million 792.3 utakaowahudumia jumla ya wakazi 3,912.
Akizungumza mara baada ya kukagua mradi huo, Mkuu wa Mkoa Kagera Mhe Albert John Chalamila Chalamila ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya sita imeendelea kutekeleza azma ya kumtua mama ndoo kichwani kwa kutekeleza miradi ya maji ili kuwaondolea wananchi usumbufu na kuwapa urahisi wa upatikanaji wa maji safi na salama.
“Hii miradi ya maji ambayo imetekelezwa kwenye Kata hii, ni miradi ya maji ambayo tunasema fedha zimetoka kwenye mfuko wa Uviko. Uviko maana yake wakati wa janga la korona linaendelea Rais Dkt. Samia alichukua jukumu la kutafuta fedha ili kukabiliana maradhi ya Uviko. Katika kutafuta fedha moja ya masharti ilikuwa moja ya masharti ilikuwa tunawapa fedha hizo ili muende mkafanye shughuli hizo za Uviko,”ameeleza Mhe. Chalamila.
Ameendelea kueleza kuwa Mataifa mengine walikwenda kununua barakao mavazi ya madaktari n.k. Rais Samia akasema nikinunua barakoa uwa zinachakaa na haziwezi kuacha alama ya kitu kizuri kilichofanyika akaamua mamilioni ya fedha hizo yatekeleze miradi ikiwemo miradi ya maji ili wananchi wapate huduma ya maji wanawe mikono yao ikiwa ni pamoja na kumtua mama ndoo kichwani.
Aidha miradi ya Uviko ilitekelezwa kwenye sekta ya elimu kwa kujenga vyumba vya madarasa lengo ikiwa ni kupunguza wingi wa watoto darasani na kuwapa nafasi ya kukaa wanafunzi 45 katika darasa moja hali ambayo itasaidia kuepuka maambukizi ya Uviko.
Kwa upande wake Diwani wa Kata Buyango Bi Regina Rwamuganga ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo elimu afya na maji.
Akisoma taarifa fupi ya utekelezaji wa mradi Mhandisi Andrew Kilembe ameeleza kuwa mradi huu umejengwa kwa kutumia vyanzo vya fedha viwili ambavyo ni fedha za UVIKO na fedha za P4R ambapo hadi sasa mradi upo katika hatua ya umaliziaji.
Kazi zilizofanyika ni kuchimba kisima kirefu na kufunga pampu ya kusukuma maji, ujenzi wa tenki la usambazaji lenye ujazo wa lita 150,000, kujenga tenki lenye ujazo wa lita 50,000, kujenga nyumba moja ya mtambo wa kusukuma maji, kujenga vituo 12 vya kuchotea maji, kuchimba mitaro na kulala bomba yenye rueful wa kilometa 15.4.
Kununua na kufunga solar panel kwenye mradi, kununua na kufunga transfoma na mfumo wa umeme, kujenga uzio kwenye eneo la tanki, sump tenki na nyumba ya mitambo na kujenga chemba kwenye vituo vya kuchotea maji na kwenye njia za kusambaza maji.
0 Comments