Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akifungua Mkutano wa Tathmini ya Utekelezaji wa Programu ya Extended Credit Facility kwa awamu ya kwanza, ulio wakutanisha wataalam kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Tanzania, jijini Dodoma.
Kiongozi wa Timu ya Wataalam kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ambaye ni Mshauri wa masuala ya Uchumi na Fedha wa Shirika hilo – Idara ya Afrika, Bw. Charambos Tsangarides, akizungumza jambo wakati wa ufunguzi kikao cha Tathmini ya Utekelezaji wa Programu ya Extended Credit Facility kwa awamu ya kwanza, ulio wakutanisha wajumbe kutoka Tanzania na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), kulia ni Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) na katikati ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Natu Mwamba.
Kiongozi wa Timu ya wataalam kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ambaye ni Mshauri wa masuala ya Uchumi na Fedha wa Shirika hilo – Idara ya Afrika, Bw. Charalambos Tsangarides, akizungumza jambo wakati wa ufunguzi wa kikao cha Tathmini ya Utekelezaji wa Programu ya Extended Credit Facility kwa awamu ya kwanza, ulio wakutanisha wadau kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Tanzania, jijini Dodoma. Kushoto ni Mwakilishi Mkazi wa IMF nchini Tanzania, Bw. Jens Reinke.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akiwa katika mazungumzo na Kiongozi wa Timu ya wataalamu kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa ambaye ni Mshauri wa masuala ya Uchumi na Fedha wa (IMF) – Idara ya Afrika, Bw. Charalambos Tsangarides, Mwakilishi Mkazi wa IMF nchini Tanzania, Bw. Jens Reinke (kulia), jijini Dodoma. Wa pili kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Natu Mwamba na wa kwanza kushoto ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba.
Kiongozi wa Timu ya wataalamu kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ambaye ni Mshauri wa masuala ya Uchumi na Fedha wa Shirika hilo – Idara ya Afrika, Bw. Charalambos Tsangarides, (katikati), akizungumza jambo wakati wa ufunguzi wa Kikao cha Tathmini ya Utekelezaji wa Programu ya Extended Credit Facility kwa awamu ya kwanza, jijini Dodoma, kulia ni Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb).
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WFM, Dodoma)
******************
Na Benny Mwaipaja, Dodoma
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amelihakikishia Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kwamba Serikali inaendelea kuzingatia makubaliano yaliyoingiwa kupitia program ya Extended Credit facility (ECF) mwezi Julai 2022 pamoja na kuchukua hatua mbalimbali za kisera za kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara nchini ili kuchochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya nchi kwa ujumla.
Dkt. Nchemba amesema hayo jijini Dodoma, wakati akifungua rasmi kikao cha timu ya wataalamu kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), ikiongozwa na Mshauri wa Uchumi na Fedha anayesimamia Idara ya Afrika kwenye Shirika hilo, Bw. Charalambos Tsangarides.
Ujumbe huo upo nchini kwa lengo la kufanya tathmini ya utekelezaji wa awamu ya kwanza ya program ya Extended Credit Facility (ECF).
Itakumbukwa kuwa tarehe 18 Julai 2022, Bodi ya wakurugenzi ya IMF iliidhinisha mkopo nafuu wenye thamani ya dola za Marekani milioni 1,046.4 ambazo zinatolewa katika awamu saba (7) kwa ajili ya kuimarisha uchumi na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kupitia programu ya Extended credit Facility (ECF) ikiwa ni matokeo ya athari mbaya za UVIKO 19 na Vita vya Urusi na Ukraine.
Dkt. Nchemba alisema kuwa kupitia program hiyo ya miezi 40, tayari Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) limetoa dola za Marekani milioni 151.7, mwezi Agosti mwaka jana, ambazo zilielekezwa kwenye maeneo ya miradi iliyokusudiwa kutekelezwa ikiwemo kuimarisha uchumi, kuimarisha biashara, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, na kujenga uchumi jumuishi kwa wananchi.
Aidha, takribani dola za marekani milioni 152 za awamu ya pili zinatarajiwa kutolewa mwezi Machi 2023 baada ya kukamilika kwa tathmini hiyo.
Dkt. Nchemba ameiambia timu hiyo kuwa uchumi wa nchi unaendelea kuimarika licha ya kuwepo kwa athari za UVIKO 19 na Vita baina ya Urusi na Ukraine ambapo Serikali ilifanikiwa kuweka ruzuku kwenye mbolea na mafuta hatua ambayo imechangia kudhibiti mfumuko wa bei.
Kwa upande wake Mshauri wa masuala ya uchumi na fedha na kiongozi wa ujumbe wa IMF, Bw. Charalambos Tsangarides, alisema kuwa timu yake itaangalia masuala mbalimbali ikiwemo sera ya uchumi na fedha pamoja na utekelezaji wa usimamizi wa uchumi mpana, sekta ya fedha na miradi mbalimbali ya maendeleo.
Aidha, Bw. Tsangarides alisema kuwa tathimini hiyo itapitia pia mwenendo wa uandaaji wa Bajeti mpya ya Serikali ili kuhakikisha inachangia ukuaji wa uchumi, kuendeleza watu kijamii kwa kuwainua kimaisha watu wasio na uwezo pamoja na maendeleo ya sekta binafsi.
Timu hiyo ya wataalam kutoka IMF itakutana na wataalam kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Benki Kuu ya Tanzania, Ofisi ya Takwimu ya Taifa, Mamlaka ya Mapato Tanzania na wadau wengine mbalimbali.
0 Comments