Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya Biashara wa Marekani Bi. Marisa Lago, akipokea zawadi ya moja ya vivutio vinavyopatikana nchini Tanzania (Mlima Kilimanjaro), kutoka kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) na Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), jijini Dodoma
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akielezea jitihada za Serikali kuboresha mazingira ya ukusanyaji wa mapato, wakati wa Mkutano na Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya Biashara wa Marekani, Bi. Marisa Lago, jijini Dodoma. Kulia ni Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb).
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Natu Mwamba, akifurahia jambo na Naibu wake, Bi. Amina Khamis Shaabani, kabla ya Mkutano kati Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) na Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya Biashara wa Marekani, Bi. Marisa Lago (hawapo pichani), jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (wa nne kushoto), na Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji(Mb) wakiwa katika picha ya pamoja na Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya Biashara wa Marekani, Bi. Marisa Lago (wa tatu kulia), jijini Dodoma. Wengine ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Natu Mwamba (kulia), Naibu wake, Bi. Amina Khamis Shaabani (wa pili kushoto) na Afisa Mwandamizi wa Biashara katika Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania, Bw. Ken Walsh, jijini Dodoma.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikali, WFM)
**************************
Na. Peter Haule, WFM, Dodoma
SERIKALI imesema imefungua milango ya ushirikiano wa kibiashara na kiuchumi kati ya Tanzania na Marekani kupitia Sekta Binafsi ili kuchochea biashara kupitia uwekezaji ikiwa ni utekelezaji wa mazungumzo kati ya Marais wa nchi hizo mbili yaliyofanyika hivi karibuni mjini Washington DC.
Hayo yamesemwa Jijini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba na Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji, walipokutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya Biashara wa Marekani, Bi. Marisa Lago.
Dkt. Nchemba amesema kuwa Tanzania ina maeneo mengi yenye fursa za uwekezaji ikiwa ni Pamoja na viwanda, kilimo, madini, uchakataji ngozi, nyama, madini lakini pia vifaa tiba, utalii, uchumi wa blue na mengine.
“Tumekuwa na majadiliano mazuri hususani katika masuala ya uwekezaji kati ya Tanzania na Marekani, tumeahidi ushirikiano kwa sekta binafsi za nchi hizi mbili katika kuongeza biashara na uwekezaji wenye tija”, alieleza Dkt. Nchemba.
Akizungumzia suala la ukusanyaji wa mapato ya Kodi Dkt. Nchemba alimwahidi Katibu Muu huyo kuwa Serikali inaendelea kuboresha mifumo ya ukadiriaji na ukusanyaji kodi kwa njia ya kidigitali ili kutenda haki, kuweka taratibu bora za ununuzi zinazozingatia pia haki ili kukuza biashara na uwekezaji hapa nchini.
“Serikali itaongeza jitihada za kupunguza mawasiliano ya ana kwa ana katika ukadiriaji wa kodi ili kupunguza makadirio ambayo hayana uhalisia” aliongeza Dkt. Nchemba
Dkt Nchemba ameishukuru Serikali ya Marekani kwa msaada wake kwa Tanzania katika Sekta ya Elimu, afya demokrasia, utawala bora na ukuaji wa uchumi, kwa kipindi cha zaidi ya miaka 50
Kwa upande wake Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dkt. Ashatu Kijaji alisema kuwa kuna miradi 271 iliyowekezwa na wafanyabashara kutoka Marekani yenye thamani ya dola za kimarekani milioni 4.8 ambayo inachochea ukuaji wa uchumi wa nchi.
Alisema kuwa Sekta ambazo zimepewa kipaumbele katika uwekezaji huo ni pamoja na Maliasili na Utalii ambapo kuna miradi 68 iliyosajiliwa katika Kituo cha Uwekezaji Tanzania na pia miradi ya 66 ya kilimo ambayo inajishughulisha na uongezaji thamani ya mazao.
“Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassani amekuwa akisisitiza sana kuwa ni wakati wa wawekezaji kuja kuwekeza na kuongeza thamani ya mazao yetu na rasilimali nyingine ambazo tumekuwa tukizisafirisha zikiwa ghafi ambapo kwa kuongeza thamani ya rasilimali katika Taifa letu tutaongeza ajira na kukuza uchumi wetu” alisema Dkt. Kijaji.
Aidha Dkt. Kijaji amewaalika tena wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Marekani kuendelea kukaa na kufanya mazungumzo na Serikali kwa kuwa Serikali ipo tayari kuhakikisha kuna wekezaji wa kutosha na wenye tija.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa masuala ya Biashara wa Marekani, Bi. Marisa Lago aliihakikishia Tanzania kuwa Marekani iko tayari kuimarisha zaidi masuala ya biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili ikiwa ni hatua ya kuunga mkono dhamira ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kukuza uchumi wa nchi kwa faida ya watu wake.
Alisema kuwa Sekta binafsi ya Marekani iko tayari kuwekeza nchini na kuishauri Serikali kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara ikiwemo kuimarisha mifumo ya kodi, mifumo ya ununuzi pamoja kuweka vivutio mbalimbali kwa wawekezaji.
Aidha, aliipongeza Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kukuza uchumi na kuimarisha Maisha ya wananchi wake na akaahidi nchi yake itaendelea kumuunga mkono ili kufanikisha dhamira hiyo.
0 Comments