Sibtain Murji 43(Kishoto) na Zameen Murji 47 (Kulia) wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kabla ya kusomewa mashtaka matatu likiwemo la kukwepa kodi kiasi cha Sh. Bilioni sita jijini Dar es Salaam jana Februari 17,2023.
*************
WATU wawili, Sibtain Murji 43 na Zameen Murji 47 wamefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kukwepa kodi kiasi cha Sh. Bilioni sita.
Katika hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo na wakili wa serikali Sylivia Mitanto akisaidiana na wakili Emmanuel Medalakini imedai kuwa tarehe isiyojulikana kati ya Januari 2021 Desemba 2022 jijini Dar es Salaam washtakiwa walishindwa kupeleka tamko la Mapato la biashara iliyosajiliwa kwa jina la Murji Brothers na kupelekea kukwepa kodi ya Sh. 6,224,341983.09/=
Pia inadaiwa, siku na mahali hapo washtakiwa hao kwa pamoja kwa makusudi, walikwepa kodi kwa njia ya udanganyifu na kuisababishia Mamlaka ya Mapato (TRA) hasara ya kiasi cha fedha zaidi ya Sh. Bilioni 6/=
Katika shtaka la utakatishaji fedha inadaiwa, Siku na mahali hapo washtakiwa hao walijipatia kiasi hicho cha fedha cha sh. bln 6/- huku wakijua kuwa fedha hizo ni zao la kosa tangulizi la kukwepa kodi.
Hata hivyo washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.
Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika na kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 3, 2023.
0 Comments