Ticker

6/recent/ticker-posts

SERIKALI KUENDELEA KUZISAIDIA KAMPUNI KUKABILIANA NA ATHARI ZA UVIKO – 19

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb)

*************************

Na. Peter Haule, WFM, Dodoma.

Serikali imeeleza kuwa inaendelea kutekeleza hatua za kiutawala na kibajeti kusaidia Kampuni za Wazawa zenye Mikopo katika Taasisi za fedha kukabiliana na athari za shughuli zao zilizosababishwa na UVIKO-19.


Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mpendae Mhe. Taofiq Salim Turky, aliyetaka kujua mpango wa Serikali kusaidia Kampuni za Wazawa zenye Mikopo katika Taasisi za fedha kutokana na athari walizozipata kutokana na UVIKO-19.


Mhe. Chande alisema Serikali imeendelea kutekeleza hatua hizo kwa kuwa athari za UVIKO - 19 zilizojitokeza zilitokana na kuvurugika kwa mnyororo wa uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa bidhaa na huduma katika Nchi washirika wa kibiashara ikilinganishwa na soko la ndani ambapo shughuli zote za kibiashara ziliendelea kama kawaida.

“Hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuziagiza benki na taasisi za fedha kutoa unafuu katika urejeshwaji wa mikopo kwa kuongeza muda wa urejeshaji wa mikopo (loan rescheduling) ”, alisema Mhe. Chande.


Alitaja hatua nyingine zilizochukuliwa kuwa ni pamoja na kuishirikisha Sekta Binafsi katika zabuni za watoa huduma na wakandarasi wakati wa utekelezaji wa Mpango wa Kukabiliana na Athari za UVIKO 19 (TCRP) kwa lengo la kuiwezesha kutengeneza faida na kurejesha mikopo katika benki na taasisi za fedha.

Mhe. Chande alisema pia Serikali ilitoa kipaumbele kwa malipo ya malimbikizo ya madeni, madai na marejesho ya kodi yaliyohakikiwa ili kuongeza mzunguko wa fedha katika uchumi na kutoa unafuu wa kikodi, ikiwemo kodi ya kuendeleza ufundi stadi (SDL) kutoka asilimia 4.5 hadi asilimia 4.

Aidha, aliongeza kuwa Serikali ilipandisha kiwango cha chini cha idadi ya waajiriwa wanaotakiwa kulipiwa kodi na Kampuni kutoka wafanyakazi 4 hadi 10 ili kupunguza gharama za uendeshaji kwa waajiri ili kuwawezesha kurejesha mikopo kwenye benki na taasisi nyingine za fedha.

Post a Comment

0 Comments