Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amesema Serikali inatarajia kuanzisha Mfuko wa Taifa wa Dhamana ya Hifadhi ya Mazingira.
Akijibu swali la Mbunge wa Donge Mhe. Mohammed Jumah Soud bungeni leo Februari 08, 2023, Mhe. Khamis amesema lengo la kuanzishwa kwa mfuko huo ni kusaidia katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Amesema kutokana na kupitishwa kwa Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 2021, Serikali kwa sasa inafanya mapitio ya Sheria ya Mazingira, Sura ya 191 ikiwemo taratibu za kuanzisha Mfuko huo.
Amesema pamoja na kuwepo kwa changamoto ya uharibifu wa mazingira katika maeneo mbalimbali nchini, Serikali imeendelea kutenga fedha za ndani kwa ajili ya shughuli za mabadiliko ya tabianchi.
Akiendelea kujibu swali hilo naibu waziri alifafanua kuwa Serikali inaendelea kunufaika na Mifuko ya kimataifa kwa ajili ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Serikali inatambua umuhimu wa kuwepo kwa vyanzo vya fedha vya uhakika ili kuimarisha jitihada za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa lengo ili zisaidie wananchi katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,” amesema.
Aidha, Mhe. Khamis amesema Serikali inaendelea kunufaika na Mifuko ya kimataifa kwa ajili ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo Mfuko wa Mabadiliko tabianchi, Mfuko wa kuhimili mabadailiko ya tabianchi, Mfuko wa nchi zinazoendelea na Mfuko wa mazingira wa Dunia.
“Vilevile, Serikali imeendelea kutenga fedha za ndani kwa ajili ya shughuli za mabadiliko ya tabianchi na lengo ni kuwa na fedha za kutosha ili zisaidie katika kukabiliana na changamoto za kimazingira,” amesisitiza.
0 Comments