Afisa Kilimo wa Kata ya Sigili Halmashauri ya Wilaya ya Nzega mkoani Tabora, Samwel Mwanji akitoa maelezo kwa Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Khamis Hamza Khamis kuhusu mradi wa kilimo cha shamba darasa unatokelezwa kupitia Mradi wa kurejesha ardhi iliyohabarika na kuongeza usalama wa chakula katika maeneo kame Tanzania (LDFS) wakati wa ziara yake mwisahoni mwa wiki.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Khamis Hamza Khamis akiuliza jambo wakati alipokuwa akikagua mradi wa shamba darasa la zao la mahindi kutoka kwa Afisa Kilimo wa Kata ya Sigili wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa Mradi wa kurejesha ardhi iliyohabarika na kuongeza usalama wa chakula katika maeneo kame Tanzania (LDFS) unaotekelezwa katika Kijiji cha Sigili, Kata ya Sigili Wilaya ya Nzega mkoani Tabora mwishoni mwa wiki.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhe. Khamis Hamza Khamis akimpa maelekezo Kaimu Mwenyekiti wa Kijiji cha Bulambuka, Biswalo Masumbuko wakati wa ziara yake ya kukagua Mradi inayotekelezwa kupitia Programu ya LDFS na kuratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.
(PICHA NA OFISI YA MAKAMU WA RAIS)
************************
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Khamis Hamza Khamis amewataka viongozi na watendaji wa halmashauri zote nchini zinazotekeleza Mradi wa Kurejesha Ardhi iliyoharibika na Kuongeza usalama wa chakula (LDFS) kutoa taarifa na kutangaza kwa umma utekelezaji wa miradi hiyo kwa wananchi ambao ndio wanufaika na walengwa.
Ametoa rai hiyo wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya LDFS inayofadhiliwa na Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) na kuratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais katika Halmashauri ya Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora.
Mhe. Khamis amesema Serikali imekuwa ikipeleka fedha nyingi za miradi ya maendeleo ya wananchi katika halmashauri hizo na hivyo ni wajibu wa wasimamizi wa miradi hiyo kutoa kutoka taarifa za hatua mbalimbali za mafanikio na changamoto zilizopo katika miradi ili wananchi ambao ndio wanufaika na walengwa wa miradi hiyo waweze kujulishwa.
Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais inatekeleza Mradi wa LDFS katika halmashauri tano nchini ambao unagusa maslahi ya wananchi na jamii kwa ujumla, natoa rai kwa wasimamizi wakiwemo viongozi na watendaji wa miradi kuweka utaratibu wa kutoa taarifa za miradi hii kwa wananchi na jamii inayowazunguka” amesema Mhe. Khamis.
Mhe. Khamis amesema Serikali Rais haitaki kuona usiri wa upatikanaji wa taarifa za utekelezaji wa miradi hiyo pindi zinapotakiwa na viongozi na wananchi pindi wanapotembelea miradi hiyo kwa kuwa inagusa maslahi ya jamii na kuziagiza Menejimenti za Halmashauri kuweka utaratibu wa rahisi kwa wananchi kupata taarifa pindi zinapohitajika.
Akizungumzia utekelezaji wa Mradi wa LDFS Wilayani Nzega, Mratibu wa mradi Hassan Mtomekela amesema una jumla ya walengwa 672 ambao wamepatiwa mafunzo mbalimbali katika usimamizi wa miradi ya mashamba darasa, utunzaji na uhifadhi wa misitu, uvunaji wa maji ya mvua, ufugaji nyuki.
Mtomekela amesema Mradi wa LDFS unaotekelezwa katika Kata ya Sigili ulianza mwaka 2018 ambapo kiasi cha sh.milioni 844 zimepokelewa na halmashauri hiyo na sh.milioni 674 tayari zimetumika katika jumla ya miradi tisa.
“Halmashauri inatoa shukrani kwa Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuendelea kutupatia fedha za utekelezaji wa mradi huu unaokwenda kupunguza changamoto zitokanazo na mabadiliko ya tabia nchi ikiwa ni pamoja na kuwaongezea kipato” amesema Mtomekela.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Nzega, Henerico Kamoga awali mradi huo uligubigwa na usiri mkubwa kutoka kwa viongozi na watendaji kwani hakuwepo na uwazi kuhusu matumizi ya fedha za miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa ghala la mashine ya kuchakata mpunga iliyopo katika Kijiji cha Bulambuka.
“Tunakushukuru Mhe. Naibu Waziri kwa kufanya ziara katika Mradi huu wa ujenzi wa ghala la kuchakata mpunga. Hivi karibuni tuliunda kamati ndogo ya fedha kwa ajili ya kukagua mradi huu, lakini hadi sasa viongozi na watendaji wamekuwa wazito na hawana ushirikiano katika utoaji wa taarifa zinazotakiwa” amesema Kamoga.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Magu, Naitapwaki Tukai amesema Ofisi yake itafanyika kazi changamoto zote zilizobainika katika baadhi ya miradi hiyo ili kuhakikisha kuwa malengo yaliyowekwa katika mradi wa LDFS na Serikali yanafakiwa.
Mhe. Khamis timu ya wataalamu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais amefanya ziara ya kutembelea na kukagua mradi wa LDFS katika wilaya ya Nzega unatekelezwa katika vijiji vya Sigili, Bulambuka, Bulende, Lyamalagwa na Ibola.
0 Comments