Ticker

6/recent/ticker-posts

MBETO AWATAKA WAFANYABIASHARA NCHINI KUSHUSHA BEI  BIDHAA ZA VYAKULA 

KATIBU wa Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Khamis Mbeto Khamis( wa pili kulia),Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi RC. Idrissa Kitwana(kushoto) na Msimamizi wa Ghala la Kampuni ya Ever Green Said Salum wakikagua bidhaa ya mchele katika ghala lililopo maeneo ya Kwa Abasi Hussein Zanzibar leo Tarehe 01/02/2023. KATIBU wa Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Ndg. Khamis Mbeto Khamis(kulia),Mkurugenzi wa Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC) Mhe. Nahaat Mohammed Mahfoudh(wa pili kulia) na Mkuu wa Mkoa Mjini Magharib Mhe. Idrissa Kitwana (kushoto) wakikagua makontena mbalimbali yenye bidhaa za chakula katika bandari ya Malindi Zanzibar.

KATIBU wa Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Ndg. Khamis Mbeto Khamis(aliyevaa shati la rangi ya kijani) akiwa na ujumbe wake akikagua kontena la bidhaa ya Mchele baada ya kutaka lifunguliwe ili ajiridhishe kama ni bidhaa hiyo iliyomo ndani.

*****************************

NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.

KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Ndg. Khamis Mbeto Khamis,amewataka Wafanyabiashara nchini kushusha bei ya bidhaa ya vyakula na kufuata bei halali na elekezi ya Serikali

Amesema wananchi wengi wanashindwa kumudu gharama za chakula kutokana na bei ya chakula kuwa juu huku kipato chao ni cha kawaida.

Maelekezio hayo ameyatoa leo katika ziara yake ya kutembelea na kukagua maghala ya kuhifadhi bidha za Chakula pamoja na Gati ya bandari ya kushusha makontena ya bidhaa hizo huko Malindi Jijini Zanzibar.

Kupitia ziara hiyo pia ametoa wiki mbili kwa uongozi wa Shirika la Bandari Zanzibar kuhakikisha wanamaliza tatizo la kushusha bidhaa za vyakula ili wananchi wapate huduma hiyo kwa wakati.

Alisema kwamba Chama Cha Mapinduzi kikiwa ndio msimamizi mkuu wa Serikali hakitowavumilia baadhi ya watendaji wanaosababisha kupanda kwa bei za vyakula huku wananchi wakiishi kwa mateso na wengine kushindwa kumudu gharama za kununua chakula.

Alisema lengo la ziara hiyo ni kujionea uhalisia wa sababu zinazokwamisha kupanda kwa bei za vyakula ambazo ni kinyume na bei elekezi ya serikali.

Alieleza kwamba licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali za kiutendaji kwa upande wa bandari na wafanyabishara, bado changamoto hizo sio kigezo cha kupandisha bei za vyakula kinyume na utaratibu uliowekwa na serikali.

Alieleza kwamba bidhaa hizo zikishushwa kwa wingi zikaingia mitaani na bei isiposhuka basi tatizo litakuwa ni kwa wafanyabishara wanaodai kuwa mchele mwingi bado haujashushwa upo bandarini.

Mbeto alisema kuwa wananchi wamekuwa wakilalamikia kupanda kwa bei za vyakula hasa mchele wa aina mbalimbali huku serikali ikitoa matamko ya kuwataka wafanyabiashara kumaliza changamoto hiyo suala ambalo bado halijatafutiwa ufumbuzi wa kudumu.

Alifafanua kuwa haiwezekani bei za vyakula kupanda mara kwa mara wakati kila siku meli za mizigo zinashusha bidhaa hiyo.

Katika maelezo yake Mbeto, alieleza wazi kwamba CCM ndio yenye dhamana ya kusimamia utekelezaji wa Ilani yake ya Uchaguzi ya mwaka 2020/2025, hivyo haiwezi kuvumilia kuona wananchi walioipa ridhaa ya kuongoza wanateseka.

“ Chama Cha Mapinduzi kipo kwa ajili ya wananchi wakati wa kampeni tulienda nyumba kwa nyumba tukinadi sera zetu na hatimaye nyinyi wananchi mkatupa ridhaa yenu, natumia nafasi hii kukwambieni kuwa bidhaa za vyakula zipo na bei itashuka hivi karibuni.

Pia natumia nafasi hii kuwataka watendaji wa umma na wafanyabisha wanaohusika moja kwa moja katika sekta ya biashara nchini kuwa na uadilifu na endapo tukibaini mtu yeyote anatukwamisha nasi tutamchukulia hatua za kinidhamu ama kisheria.”, alisisitiza Mbeto.

Pamoja na hayo alikemea tabia ya baadhi ya Wafanyabishara nchini wanaohujumu na kufanya uhalifu wa magendo ya kusafirisha na kuuza bidhaa za Chakula nje ya Zanzibar na Tanzania kwamba wakibainika watanyang’anywa leseni kasha kushitakiwa kwa usaliti huo.

“ Tunazo taarifa za kuaminika kuwa kuna baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu wanashusha bidhaa za vyakula katika Bandari yetu ya Malindi baadae wanazisafirisha kwa njia ya magendo kuuza nje ya mipaka ya Zanzibar, wakati sisi chakula bado kinahitajika kwa wingi.”, alisema Mbeto.

Katibu huyo wa NEC Mbeto , alisema ametembelea Maghala kadhaa pamoja na bandarini kujionea harakati za kushusha bidhaa za vyakula na kuhakikisha kuwa bidhaa hizo zipo hivyo zinatakiwa kuonekana mitaani zikiwa na bei nafuu ambayo ni elekezi iliyowekwa na serikali.

Naye Mkuu wa Mkoa Mjini Magharib Mhe. Idrissa Kitwana, alikipongeza Chama Cha Mapinduzi kwa maamuzi yake ya kutafuta ufumbuzi wa kudumu juu ya tatizo la kupanda kwa bei ya vyakula Zanzibar.

Aliwataka Wafanyabishara nchini kuhakikisha bidhaa za vyakula zikiwemo mchele,unga wa mahindi,mafuta ya kula,unga wa ngano na sukari vinapatikana kwa wingi mtaani na vinauzwa kwa bei halali iliyowekwa na Serikali.

Alisema kwamba akiwa ni Mkuu Mkoa huo hatoweza kuendelea kuona baadhi ya Wafanyabishara wanapinga maelekezo ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi pamoja na Chama Cha Mapinduzi.

Alisema Serikali imekuwa ikiweka mazingira rafiki kwa wafanyabisha kuhakikisha wanafanya shughuli zao bila usumbufu hivyo na wao wanatakiwa kuwa wazalendo ili wananchi waondokane na tatizo la kupanda kwa bei ya vyakula nchini.

“Kilio hiki hata Rais wetu mpendwa Dk. Hussein Ali Mwinyi, ametumia busars kubwa kuwaita wafanyabishara juzi akazungumza nao kwa upole ili kutafuta ufumbuzi wa tatizo hili la kukosekana kwa chakula na kupanda kwa bei.”, alisema RC.Kitwana.

hilo.

Alisema kuwa bidhaa hizo zinatakiwa kurudi katika bei halali kabla ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwani baadhi ya wafanyabishara hutumia mwezi huo kujinufaisha wenyewe.

Naye Mkurugenzi wa Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC) Mhe. Nahaat Mohammed Mahfoudh, alisema wanaendelea kufanya kazi kwa bidhii kuhakikisha makontena yote yenye bidhaa za chakula yanashusha mizogo hiyo kwa wakati.

Alieleza kuwa tayari wameshusha kontena 250 na zingine 250 zinaendelea kushushwa ili kuhakikisha bidhaa hizo za vyakula zinachukuliwa na wafanyabisha ambao ndio wamiliki wa bidhaa hizo.

Aliahidi kuyafanyia kazi kwa haraka maelekezo yote yaliyotolewa na Rais wa Zanzibar Dk.Mwinyi pamoja na Chama Cha Mapinduzi ili kumaliza changamoto zinazowakabili wananchi katika masuala ya kupanda kwa bei za vyakula.

Naye msimamizi wa Ghala la kampuni ya Ever Green Ndg. Said Salum Khalfan, alisema katika ghala lake tayari kuna mchele tani 500 na nyingine inaendelea kushushwa bandarini.

Alisema kwamba mchele huo wanauza mfumo mmoja wa Kg 50 wanauza kwa shilingi 82,600/= na Kg 25 wanauza kwa shilingi 43,000/= bei ambayo ni ya kawaida.

Mapema juzi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, alizungumza na wafanyabisha wa bidhaa za vyakula na kuwataka kushusha bei kwani wananchi wanaumia.

Sambamba na hayo aliwashauri kushirikiana kwa kuagiza meli kubwa zenye uwezo wa kuleta makontena mengi yatakayofikisha tani 30,000 ili kukidhi mahitaji ya wananchi wa Zanzibar wanaotegemea mchele kama chakula kikuu cha kila siku.

Post a Comment

0 Comments