Meli kubwa ya Mzigo kutoka nchini Urusi yenye urefu wa mita 150 ikiwa imetia nanga katika Bandari ya Tanga mapema leo
Meli kubwa ya Mzigo kutoka nchini Urusi yenye urefu wa mita 150 ikiwa imetia nanga katika Bandari ya Tanga mapema leo
Na Oscar Assenga,TANGA.
Matunda ya uwekezaji wa Bandari ya Tanga yameanza kuonekana mara baada ya Meli kubwa ya Mzigo kutoka nchini Urusi yenye urefu wa mita 150 kutia nanga gatini katika Bandari hiyo
Hatua hiyo ni baada ya kukamilika kwa gati lenye urefu wa mita 300 ambao umeiwezesha meli hiyo kuweza kutia nanga gatini na kuandika historia kwa mara ya kwanza kupokea meli kubwa mpaka gatini na hivyo kuandika historia ya kipekee baada ya maboresho makubwa yaliyofanywa na Serikali.
Akizungumza leo wakati wa mapokezi ya meli hiyo ambayo ilikuwa imebaba shehena ya Mbolea kwa ajili ya viwanda ,Meneja wa Bandari ya Tanga Masoud Mrisha alisema ujio wa meli hiyo ni matunda makubwa ya uwekezaji ambao umefanywa na Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu kwenye Bandari hiyo.
Alisema kwamba meli hiyo ilikuwa imebeba mzigo wa tani 6909 unaokwenda nchini Kongo ambapo utapakuliwa kwa muda wa siku mbili kuanzia leo Jumatatu.
Aidha Meneja huyo aliwataka wafanyabiashara kwamba Bandari ya Tanga imeanza kufunguka kutokana na maboresho makubwa hali ambayo imepelekea huduma kuimarika zaidi.
Awali akizungumza Mkuu wa Kitengo cha Masoko wa Bandari ya Tanga Rose Tandiko alisema kwamba matunda ya ujio wa meli hiyo ni kutokana na uwekezaji mkubwa ambao umefanywa na Rais Samia Suluhu.
Alisema uwekezaji huo umewezesha kuandika histoiria katika Bandari hiyo kwa kuanza kuhudumia meli ya kichele gatini jambo ambalo awali lilikuwa halifanyiki.
Hata hivyo alisema kwamba wanamshukuru Rais Samia Suluhu kwa uwekezaji mkubwa uliofanyika katika Bandari hiyo na matokeo yake yameanza kuonekana .
0 Comments