Mgeni rasmi kwenye kongamano la kumbukizi ya miaka 117 wa mashujaa wa vita ya Majimaji wapatao 67 lililofanyika kwenye ukumbi wa Crasta mjini Tunduru ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Mkuu wa Wilaya ya Tunduru ambaye aliwakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Mheshimiwa Ngollo Malenya.Kila mwaka inafanyika kumbukizi ya mashujaa hao wa vita ya Majimaji waliouawa na wajerumani kwa kunyongwa Februari 27,1906 Baadhi ya wadau kutoka wilaya zote za Mkoa wa Ruvuma,watalaam kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na wahadhiri wa Chuo kikuu cha Dar es salaam wakiwa kwenye kongamano la kumbukizi ya mashujaa wa vita ya Majimaji kwenye ukumbi wa Crusta mjini Tunduru
***********************
MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi wa Makumbusho ya Taifa Tanzania Dkt. Oswald Masebo ameshauri matamasha ya kumbukizi yatumike kukemea vitendo viovu vinavyokwenda kinyume na mila na desturi ya mtanzania.
Dkt.Masebo ametoa ushauri huo kwenye kongamano la kumbukizi ya mashujaa wa vita ya Majimaji lililofanyika kwenye ukumbi wa Crasta mjini Tunduru.
Kongamano hilo ni sehemu ya kumbukizi ya miaka 117 ya mashujaa wa vita ya Majimaji waliuawa na wajerumani Februari 27,1906 kwa kunyongwa mashujaa 67 na wajeruamni katika eneo la Songea Klabu na kuzikwa ndani ya makumbusho yaTaifa ya Majimaji Mahenge Songea.
Mwenyekiti huyo wa Bodi ya Wakurugenzi wa Makumbusho amesema,hivi sasa Taifa lipo katika vita ya kupambana na watu wanaoharibu mila na desturi za mtanzania ambapo kumekuwa na mmomonyoko wa maadili kwa Watoto na vijana.
“Hivi sasa vitendo vya kishoga ambavyo ni kinyume na mila na desturi zetu vimekuwa tishio kubwa kwa vijana wetu,hivyo tunapofanya kumbukizi kama hii ya mashujaa wa vita ya Majimaji inatakiwa sote kukemea kwa nguvu zote ili kulinusuru Taifa kuingia kwenye janga kubwa la mmomonyoko wa maadili’’,alisisitiza Dkt.Masebo.
Akizungumza wakati wa ufungaji kongamano hilo ambalo lilishirikisha wadau mbalimbali kutoka mkoa wa Ruvuma ,Wizara ya Maliasili na Utalii na watoa mada kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam,mgeni rasmi Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mhe.Ngollo Malenya ameipongeza Wizara kwa kufanya kongamano hilo kwa mara ya kwanza katika wilaya ya Tunduru.
Mheshimiwa Malenya ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo amesema wilaya ya Tunduru ndiyo kiini cha ukombozi wa nchi ya Msumbiji kwa kuwa mipango yote ya harakati za ukombozi wa nchi hiyo zilifanyika katika Kijiji cha Masonya Tunduru ambapo hayati Baba wa Taifa Mwl.Julius Nyerere na Hayati Samora Michel wa Msumbiji walipanga mipango yote hadi nchi ya Msumbiji ilipopata uhuru wake mwaka 1975.
Mkuu wa Wilaya ametoa rai kwa vijana walioshiriki kwenye kongamano hilo kuacha mila na desturi za kigeni badala yake kufuata maelekezo ya wazee kwa kuzingatia maadili,mila na desturi ili kulinda utamaduni wa mtanzania.
Katika kongamano hilo mapendekezo mbalimbali yalitolewa ikiwemo mapendezo ya kurejeshwa hapa nchini malikale zote za Mkoa wa Ruvuma zilizopo nje ya nchi na wanafunzi katika shule za sekondari na vyuo kila mwaka kuhakikisha wanashiriki kikamilifu kwenye matamasha ya mil ana utamaduni ili kurithisha historia ya Tanzania.
Mada mbalimbali ziliwasilishwa zikiwemo kutoka kwa wahadhari wa chuo kikuu cha Dar es salaam na Wataalam wa Makumbusho ya Taifa zikiwemo nafasi ya ndumba katika vita,urithi na utamaduni wa wangoni na utamu wa historia ya Mkoa wa Ruvuma.
Kilele cha miaka 117 ya kumbukizi ya mashujaa 67 wa vita ya Majimaji kinatarajiwa kufanyika Februari 27,2023 katika Makumbusho ya Taifa ya Majimaji mjini Songea ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii.
Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Mkoa wa Ruvuma
0 Comments