Mtangazaji wa kipindi cha kumepambazuka katika Televisheni ya Zanzibar Calbe(ZCTV) Ndg.Homoud Abdallah(kulia),akiongoza kipindi cha kumepambazuka wakati akiwa na wageni kutoka Maktaba kuu Zanzibar ambao ni Mkurugenzi wa Bodi ya Huduma za Maktaba Zanzibar Ndg.Ulfat Abdul-Aziz Ibrahim(wa pili kulia),pamoja na Mkuu wa Divisheni ya Maktaba Zanzibar Ndg.Mahfudha Abdallah(kushoto) leo tarehe 27/02/2023.
*************************
NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
WAZAZI na walezi nchini wameshauriwa kuwapeleka watoto wao katika maktaba mbalimbali nchini ili wajifunze masuala mbalimbali ya kitaaluma.
Ushauri huo umetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Huduma za Maktaba Zanzibar Bi.Ulfat Abdul-Aziz Ibrahim,katika kipindi maalum kinachorushwa mbashara na Kituo cha Televisheni ya Zanzibar Cable(ZCTV) iliyopo Migombani Zanzibar.
Amesema maktaba kuu nchini imeweka mazingira rafiki ya kuwajengea uwezo watoto mbalimbali ili wapate nafasi ya kujifunza mambo mbalimbali kwa mujibu wa vipaji vyao.
Amesema vipindi hivyo vinajumuisha watoto kuanzia ngazi za nasari hadi kitado cha sita na kwamba hata watoto ambao umri wao bado sio wa kwenda skuli wanapata nafasi ya kujumuika na wenzao kwa nia ya kujifunza.
“Kila siku ya ijumaa tuna kipindi maalum cha watoto kunakuwa na huduma ya kusoma vitabu mbalimbali,michezo hata vipindi vya masomo vya elimu kwa njia ya luninga kwani mtoto kama hawezi kusoma basi atajifunza kwa njia ya Televisheni kupitia katuni na njia nyingine za kisasa”, alieleza Ulfat.
Akizungumzia mipango ya taasisi hiyo kuwa kwa mujibu wa maelekezo ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020/2025 kuwa imeelekeza wajenge maktaba tatu za kisasa kwa Unguja na Pemba ili kuimarisha huduma za taasisi hiyo.
Bi.Ulfat, alisema wanajipanga kuhamia katika teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA), ili wananchi pamoja na wadau wengine waliopo nje ya nchi wapate huduma za taasisi hiyo kwa wakati.
Katika maelezo yake Mkurugenzi huyo Ulfat,alieleza kuwa wana dhamira ya kwenda na mabadiliko ya sayansi na teknolojia kwa kuhakikisha maktaba zote za Zanzibar zinakuwa na vituo maalum ya ubunifu utakaowawezesha wanachama wa maktaba na wananchi kwa ujumla kuibua vipaji vya fani mbalimbali sambamba na kuendeleza vipaji hivyo.
Naye Mkuu wa Divisheni ya maktaba Zanzibar Mahfudha Abdallah,alisema kuwa taasisi hiyo itaendelea kutoa huduma nzuri na rafiki kwa wananchi wote.
Alisema lengo la serikali ni kuhakikisha machapisho,vitabu na taarifa mbalimbali za kitaaluma vinapatikana kwa wakati ili wanafunzi na wadau mbalimbali wanapata fursa ya kusoma na kujifunza mambo mbalimbali ya kitaaluma,utamaduni,sayansi na saikolojia.
Akizungumzia changamoto zinazowakabili katika maktaba kuu nchini kuwa ni udogo wa eneo la ofisi hiyo haliendani na mahitaji yao kwa sasa.
“Wananchi wengi bado wana dhana ya kuwa maktaba zipo kwa ajili ya wananchi jambo ambalo sio sahihi kwani taasisi hiyo ipo kwa ajili ya watu wote kulingana na mahitaji wanayotaka kujifunza”, alisema Mkuu huyo wa Divisheni ya Maktaba nchini bi.Mahfudha.
Bi.Mahfudha, alisema kwa sasa wananchi wengi wameanza kuelewa umuhimu wa maktaba na kwamba wamekuwa wakijitokeza kwa wingi kupata huduma za kusoma machapisho ya vitabu na nyaraka.
0 Comments