Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akishiriki katika kiapo sambamba na wanachama wapya aliowakabidhi kadi katika Maadhimisho ya miaka 46 ya CCM yaliyofanyika kimkoa kwenye uwanja wa CCM Biharamulo mkoani Kagera, Februari 5, 2023.Kulia ni Mwenyekiti wa CCVM wa Mkoa huo, Nazir Karamagi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiteta na mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Kagera na Mkuu wa Mkoa huo, Albert Charamila katika Maadhimisho ya miaka 46 ya CCM yaliyofanyika kimkoa kwenye uwanja wa CCM Biharamulo mkoani Kagera, Februari 5, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa , Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea kutoka kwa Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Kagera, Nazir Karamagi, ngao ya pongezi iliyotolewa na CCM mkoa huo katika Maadhimisho ya Miaka 46 ya CCM yaliyofanyika kimkoa kwenye uwanja wa CCM Biharamulo, Februari 5, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Wapenzi na wanachama wa CCM wakimsikiliza Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa , Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza katika Maadhimisho ya miaka 46 ya CCM yaliyofanyika kimkoa kwenye uwanja wa CCM Biharamulo mkoani Kagera, Februari 5, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
********************
MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wana-CCM na wananchi kwa ujumla waendelee kuiamini Serikali yao kwa sababu watendaji wake wamejipanga kuwatumikia kwa weledi, uadilifu na uaminifu wa hali ya juu.
Pia, Waziri Mkuu amesema Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na Mwenyekiti wa CCM Taifa amefanya maboresho makubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo ya uwekezaji lengo likiwa ni kukuza uchumi wa Taifa na wa mwananchi mmoja mmoja.
Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo (Jumapili, Februari 5, 2023) wakati wa maadhimisho ya Sherehe za Miaka 46 ya CCM Mkoa wa Kagera. Maadhimisho hayo kimkoa yamefanyika katika Uwanja wa CCM wilayani Biharamulo.
Amesema Serikali imeboresha mazingira ya uwekezaji na kuvutia uwekezaji kwenye sekta za madini, kilimo na viwanda ikiwa miongoni mwa mikakati ya Serikali ya kupambana na changamoto ya ajira hususan kwa vijana.
"Mheshimiwa Rais Dkt Samia amejikita katika kutatua changamoto ya ajira nchini kwa kupanua wigo wa uwekezaji na kuwakaribisha waje wawekeze nchini wajenge viwanda. Uwekezaji katika kilimo, viwanda ndio jibu la tatizo la ajira."
Pia, Mheshimiwa Majaliwa amewasisitiza watendaji wa halmashauri wahakikishe vijana wanapatiwa maeneo ya kilimo na hati pamoja na kuwapa kipaumbele katika utoaji wa mikopo itokanayo na asilimia 10 ya mapato yao ya ndani.
Akizungumzia kuhusu maslahi ya wtumishi wa umma, Waziri Mkuu amesema CCM imeielekeza Serikali isimamie ipasavyo maslahi yao ikiwa ni pamoja na kulipa madeni na malimbikizo mbalimbali pamoja na upandishwaji wa madaraja, hivyo amewataka waendelee kuwa na imani na Serikali yao.
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwashukuru Watanzania kwa kuiunga mkono CCM katika utekelezaji wa ilani yake ya uchaguzi ya 2020 ambayo imeainisha mambo mbalimbali ya maendeleo yanayotekelezwa nchi nzima ukiwemo na mkoa wa Kagera.
Kwa upande wake, Mbunge wa jimbo la Biharamulo, Mhandisi Ezra Chiwelesa ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuidhinisha fedha nyingi ambazo zinatumika katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi ikiwemo shilingi bilioni 1.8 zilizotumika kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 91 katika shule za sekondari pekee.
0 Comments